MBUNGE wa Arusha mjini Godbless Lema amesema miongoni mwa wezi wa fedha
za kampuni ya kufua umeme IPTL yumo mbunge wa chama cha upinzani.
Lema alisema hayo jana alipokuwa akiwahutubia wakazi wa Kata ya
Miyomboni – Kitanzini uliofanyika katika uwanja wa mnada (well fair) katika
Manispaa ya Iringa.
Alisema magerezani wamejaa masikini wasio na hatia huku wezi wakubwa
wanaoifilisi nchi wakiwa ni wabunge na mawaziri ambao hawaguswi na kuachwa
kuendelea kula raha bungeni.
Alifafanua kuwa akiwa na mwenzake Mbunge Peter Msigwa, wametajiwa mbunge
wa chama cha upinzani ambaye alisaini fedha hizo kwa ajili ya matumizi yake
binafsi japo kuwa hakumtaja kwa jina na kwamba wanasubiri waziri mwenye dhamana
aliweke wazi bungeni ili aweze kushughulikiwa kama ambavyo mbunge yeyote
anashughulikiwa akiwa na tuhuma na makosa mbalimbali.
Alisema nchi inatia aibu kugeuka ombamba huku ikiwa na rasilimali nyingi
za kila aina ambazo zinawafaidisha wachache wasiona uchungu na nchi wanaoiba na
kulindwa kama dhahabu kana kwamaba ni watu muhimu huku masikini wakibambikwa
kesi za ajabu ajabu.
“Ndugu zangu, tunapopambana na CCM, tunapambana na wezi, majambazi,
mafisadi na wahuni. Unapokuwa na chama kinachouza ndovu, madini, misitu, na
ardhi, uhusiano wao na shetani ni wa karibu.
“Unapokuwa na chama kinachotoa sukari kiwandani kwa shilingi 1,000/= na
kutoza kodi hadi kufikia 2,000/= au ukiwa na chama ambacho sementi kiwandani
inatengenezwa kwa shilingi 4,000/= na kutoza kodi hadi kufikia shilingi
15,000/= ni chama cha mauaji” alisema Lema.
Pia alisema wapo wanasiasa ambao wamefirisika kimawazo na kutumia imani
za kidini kuwagawa watangania jambo ambalo wananchi wanatakiwa kuwapuuza
wanasiasa wa namna hiyo kwani hawana mawazo ya maendeleo.
“Anayewatenganisha kwa udini
ni muhuni tena hapaswi kusikilizwa kabisa. Jaribuni kuwahoji wanasiasa wa namna
hiyo kuwa kwani bungeni kuna kukusanya sadaka? Au bungeni kuna kufungisha ndoa?
Bungeni ndugu zangu ni kujenga hoja tu wala hakuna sadaka wala kufungisha ndoa”
alisema Lema.
Mbunge wa Iringa mjini Mch. Peter
Msigwa alisema ikiwa nchi yenye rasilimali nyingi kama Tanzania inategemea
asilimia 40 ya bajeti nzima kutoka kwa wahisani na wafadhiri mbalimbali, nchi
haina viongozi wenye uwezo wa kufiki jinsi ya kujitegemea.
Alisema cha kushangaza kuna
wabunge ambao wapo madarakani kwa miaka mingi lakini majimbo yao hayana
maendeleo kwa muda mrefu lakini kazi yao ni kuunga mkono bajeti hewa.
“Mipango yote inaandaliwa
kwa ajili ya matajiri na makampuni makubwa yanayokweta kulipa kodi pamoja na
kuiba rasilimali za umma au kuwaibia watanzania” alisema.
Alisema inapoonekana mmoja
anaonewa jamii inapaswa kupiga kelele kwa kuwa kuonewa kwa mtu mmoja ni kuonewa
kwa jamii nzimaa.
“Akionewa machinga, nesi
hapaswi kukaa kimya, akionewa mwalimu machinga hapaswi kukaa kimya. Watu wote
tunategemeana kwa kazi tunazozifanya” alisema.
Naye John Mwambigija maarufu
kwa jina la Mzee wa upako amewataka wananchi wa Mkoa wa Iringa wasivunjike moyo
na uchaguzi wa Kalenga bali uwe changamoto kwa chaguzi zijazo na kujipanga kwa
ajili ya kukabiliana nazo.
“Kazi ya mabadiliko siyo
rahisi lakini cha msingi tunatakiwa kuungana kwa pamoja ili tuwe na nguvu ya
pamoja.
“Umasikini tulionao
unasababishwa na mawazo mepesi walio nayo viongozi wasio na uwezo wanaotumia
nafasi zao kutuhujumu” alisema Mwambigija.

No comments:
Post a Comment