Mbunge wa jimbo la Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa
(CHADEMA) amevijia juu baadhi ya vyombo vya habari mkoani humo kutokana na kile
alicho kiita ni kutumika vibaya na baadhi ya wanasiasa wasiyo na mapemzi mema
na wananchi wa jimbo hilo.
Akizungumza katika mkutano wake na wananchi wa kata ya
Ruaha juzi, Msigwa ambaye pia ni waziri
kivuli wa mali asili na utalii alivitaja kwa majina vyombo hivyo (majina tunayo) aliwataka wananchi hao kuto
viamini vyombo hivyo na kwamba vimekuwa
vikitumika vibaya na chama tawala chama cha mapinduzi (CCM).
Katika kuonesha kwamba anavifahamu vizuri vyombo hivyo pamoja
na waandishi wao (siyo wa mtandao huu) Msigwa
alisema baadhi yao wamekuwa wakishiriki katika kampeni za chini kwa chini za
chama cha mapinduzi ikiwemo kuwarubuni vijana kwa fedha huku wengine wakishiriki katika mafunzo ya
ulinzi kwa vijana wa CCM maarufu kwa
jina la green gurd yanayoendelea kufanyika katika kambi ya Ihemi mkoani
Iringa.
Msigwa alisema watanzania wanatakiwa kukumbuka vita vya
wenyewe kwa wenyewe vilivyowahi kutokea nchini Rwanda kwamba kisa kilikuwa ni
vyombo vya habari ambavyo vilishindwa kutumia ipasavyo taaluma yao na hatimaye
kuliingiza taifa la Rwanda katika mapigano makubwa na ya kihistoria.
“Baadhi yenu waandishi na watangazaji wa radio hapa mkoani
mnatumika vibaya, nawaaambieni mtaiingiza nchi hii katika vita kubwa. Mimi niliaminiwa na wananchi wa jimbo la
Iringa sikupita kwa ngekewa kama mnavyosema waheshimu hawa walionichagua ”
alisema.
Katika hatua nyingine mbunge Msigwa amewaonya baadhi ya
waandishi hao kwa kuukejeli ubunge wake
mbele ya wananchi kwa kumwita mbunge aliyechaguliwa kwa ngekewa na kwamba
kitendo cha waandishi hao kugeuza vyombo vyao vya habari kuwa jukwaa la siasa
hata weza kulivumilia kamwe.
Siku za hivi karibuni mbunge huyo amekuwa akisikika
akilalamikia vyombo hivyo vya habari kushindwa kumtendea haki yeye pamoja na
wananchi wa jimbo hilo kwa kushindwa kuandika ukweli wajinsi utekelezaji wa ahadi zake ambazo aliahidi
katika kipindi cha kampeni za uchaguzi zilizopita mwaka 2010 jambo ambalo
alisema linalenga kumgombanisha na
wapiga kura wake.
Aidha Msigwa alisema baadhi ya waandhishi hao wamethubutu
kuwarubuni wananchi kwa kuwaambia kuwa msaada wake wa vitanda vya wagonjwa
ambavyo alivitoa mapema mwaka jana na kukabidhi uongozi wa hospitali ya Wilaya
iliyopo Frelimo haukukidhi haja kutokana
na vitanda hivyo kuonekana kuwa na madhara kwa wagonjwa jambo ambalo mtandao huu umefanya utafiti na kuthibitisha kuwa vitanda vinatumika na wananchi wanaotumia
hospitali hiyo bila madhara yoyote.
Akizungumza na mtandao huu hospitalini hapo, daktari ambaye
aliomba jina lake lisiandikwe alisema hakuna madhara yaliyotokea kwa
mtu yoyote kutokana na vitanda hivyo na kwamba uvumi wa kuwapo na madhara kwa vitanda
hivyo si wa kweli.
“Vitanda vilivyopo vinaendelea kutumika bila tatizo japo kuwa
nimesikia kuna baadhi watu wakisema kuwa vina madhara. Sisi wahudumu tuliopo
hapa hatujawahi kuyaona madhara yoyote na tunawaambia wananchi kuwa hakuna
tatizo ambalo inatokana na vitanda. Hayo ni maneno ya watu wasiopenda
maendeleo.
“Nawaombeni wanasiasa msiingilie taaluma za watu. Msijinadi kwa
kutumia uongo kuharibu taaluma za watu. Watu wanaotangaza uongo wanamna hiyo
siwapendi kwa sababu sisi tunataka huduma yetu iwe nzuri na ya kuheshimika. Isitoshe
wanaotangaa uongo huo si wale walioleta vita. Mimi nasema kama Mbunge angeweza,
alete vitanda vingine kama hivi kwa sababu vitanda vina hadhi” kilisema chanzo
chetu.
Malalamiko ya Mbunge huyo yanakuja kipindi ambacho chama cha
mapinduzi kinapigana kufa na kupona kutaka kulipokonya jimbo hilo ambalo
wananchi wa Iringa mjini mwaka 2010 waliamua kwa mapenzi yao kumchagua Msigwa
kama mwakilishi wao halali bungeni.
Hata hivyo Mch. Msigwa pamoja na kuwataka wananchi kuwapuuza
waandishi hao lakini pia ameendelea kuungwa mkono na akina mama, wasomi, wazee
pamoja na kundi la vijana katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya jimbo lake
la Iringa mjini.
Miongoni mwa ahadi ambazo mbunge Msigwa aliahidi na tayari
amekwisha onesha uwezo wa kuzitekeleza ni pamoja na kuwajengea wananchi uwezo
wa kujitambua na kutambua haki zao, kuboresha miundo mbinu ya barabara ambazo
zinaendelea kutengenezwa, pia aliahidi
kuwasha taa za baadhi ya barabara za mitaa ya mji wa Iringa zikiwamo za stendi kuu ahadi
ambayo imetekelezwa.
Pamoja na hayo Msigwa katika kipindi cha kampeni aliahidi
kutoendeleza utamaduni uliokuwa umejengeka kwa wananchi wa jimbo hilo wa kupewa
fedha kutoka kwa wabunge waliopita na kwamba yeye atawajibika kuwajengea uwezo
katika kutafuta riziki kuliko kuwategemezi .
Ahadi nyingine ambayo inakumbukwa sana na wapiga kura wake ni
ile ya kumwajili mwanasheria ambaye anajukumu la kuwasimamia wananchi katika
kutafuta na kudai haki zao pindi wapatapo matatizo yanayohusu utashi wa
kisheria jambo ambalo pia amelitekeleza.
Msigwa pia aliahidi kukomesha tatizo la ukosefu wa maji
ambapo hadi sasa jimbo la Iringa mjini linapata maji kwa asilimia tisini jambo
ambalo wananchi wa jimbo hilo wanajivunia ukilinganisha na majimbo mengine kama
Kilolo, Mufindi kaskazini, Isimani pamoja na Kalenga ambayo yote kwa pamoja
yanaongozwa na wabunge wa chama cha mapinduzi lakini upatikanani wa maji ni wa tabu.
Hata hivyo katika kuonesha nia yake ya kweli aliyowahi
kuahidi katika majukwaa ya kampeni za
uchaguzi uliopita mbunge Msigwa
ndiye mbunge pekee kuwahi kutokea
kupitia chama pinzani nchini na ambaye
amekuwa kivutio kwa wengi ndani na nje ya bunge hasa katika michango yake awapo
bungeni.

No comments:
Post a Comment