| Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Viziwi Iringa Alinanuswe Mwakosya akiongea na viongozi wa umoja wa akina mama wa madhehebu ya Kikristo katik Manispaa ya Iringa walioitembele shule hiyo. |
| Mbele ya wanafunzi ni umoja wa akina mama wa madhehebu ya Kikristo walioitembelea shule hiyo. |
| Akina mama wakiwa wamekaa mbele ya wanafunzi. |
| Watoto wenye ulemavu wa kusikia na kuona waliopo katika Shule ya Msingi viziwi Iringa. |
| Wanafunzi wakimtazama mwalimu aliyekuwa akizungumza nao kwa vitendo akifasili ujumbe kutoka kwa umoja wa akina mama wa madhehemu ya Kikristo walioitembelea shule hiyo na kutoa msaada. |
| Baadhi ya wanawake walioangua kilio ukumbini baada ya kupokea maelezo kutoka kwa walimu wa shule hiyo juu ya changamoto zinazo wakabili shuleni hapo. |
| Baadhi ya vyakula vilivyotolewa na umoja wa wanawake wa madhehebu ya Kikristo katika Manispaa ya Iringa kwenye Shule ya Msingi Viziwi Iringa. |
UMOJA wa wanawake wa madhehebu ya Kikristo katika Manispaa ya Iringa wameshindwa kujikaza na kujikuta wakiangua vilio katika shule ya msingi ya watoto wenye ulemavu wa kuona (viziwi) Iringa walipoitembelea shule kuwaona watoto na kutoa misaada.
Wanawake hao walijikuta wakiwa katika vilio baada ya kupokea maelezo ya Mwalimu Mkuu wa shule hiyo juu ya changamoto zinazowakabili shuleni hapo.
Akitoa maelezo kwa akina mama hao Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Alinanuswe Mwakosya alisema kuwahudumia watu wenye ulemavu wa kusikia kunahitaji moyo kwani ni watu wanaohitaji uangalizi wa karibu pamoja na faraja ili wajione ni miongoni mwa jamii.
Alisema waalimu wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kulazimika kutumia akiba zao kwa ajili ya kuwahudumia wanafunzi kutokana na baadhi ya wazazi kuwatelekeza watoto wao shuleni hapo.
“Kuna wazazi wengine wakileta watoto hapa wanakuwa kama wametua mizigo kwa sababu wakishawaacha wanakwenda moja kwa moja na hawakumbuki kuwatumia chochote. Hata unapofika wakati walikizo wakipigiwa simu wanauliza kwa nini mnafunga hebu kaa naye kama wiki moja hivi halafu nitakuja kumchukua. Hali hii inakuwa mzigo kwa walimu kwa sababu tunakuwa kama tumeziliwa mtoto” alisema.
Wakati akieleza hayo kwa hisia na uchungu, huku akina mama hao wakiona mazingira ya shule, hawakukawia kutoa machozi hali iliyosababisha vilio kwa kila mtu aliyekuwapo mahala hapo.
Mwakosya alisema watoto wanaopelekwa shuleni hapo wanatoka katika mazingira tofauti na licha ya kuwa wana ulemavu wa kusikia, wapo wengine ambao wana ulemavu wa kuona pia.
Hata hivyo alisema idadi ya walimu iliyopo haikidhi mahitaji kulingana na idadi kubwa ya wanafunzi waliopo shuleni hapo ambapo shule inaupungufu wa walimu wanne na walezi saba.
Alieleza changamoto nyingine kuwa baadhi ya watoto wanaopelekwa shuleni hapo wameonekana kutojua kama kuna vyakula mbalimbali ambapo wengine wanajua chakula kimoja tu hali inayofanya kukataa vyakula vingine.
“Kuna watoto wengine hawajui kama kuna vyakula vya aina nyingine duniani bali wanaochojua wao kuwa kuna wali tu! Hili linatupa ugumu sisi walimu kutumia muda mwingi kuwafundisha na kuwaelekeza kuwa hapa duniani kuna vyakula vya aina mbalimbali” alisema.
Kwa upande wake mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo Fidelisi Mushi alisema kazi ya kulea watoto wasio wako inahitaji uvumilivu.
Alisema walimu walimu wanaofundisha watoto wenye ulemavu inahitaji upendo wa hali ya juu kwani kwa mtu asiyekuwa na upendo wa dhati hawezi kuvumilia kutokana na mambo mbalimbali yanayojitokeza.
“Watoto hawa wana mambo mengi, unaweza ukawa unafundisha halafu ghafla unashangaa anataka kulala. Akishaamua kitu ameamua ila cha kufanya muache kwa muda fulani halafu uanze kuona ni namna gani unaweza kumbembeleza. Kwa maana hiyo kama huna upendo huwezi kabisa na wakati mwingine anaamua kujichafua alipokaa au aliposimama. Yataka moyo kwa kweli” alisema kwa uchungu.
Hata hivyo alisema kuwa wazazi wengine wamekuwa wagumu kuchangia hela kidogo na kusababisha walimu kujikuta katika wakati mgumu wakitumia fedha zao kuendesha shule huku familia zao zikikosa mahitaji ya licha ya kuwa mshahara wao haukidhi mahitaji yao binafsi.
Aliiomba serikali kuongeza shule za wenye ulemavu wa kusikia nchini ili kwani kumekuwa na watoto wanaoachwa majumbani kwa sababu ya shule kuwa chache.
Wakiwa kwenye vyumba vya kulala watoto shuleni hapo, Mwalimu Mushi aliwaeleza akina mama hao kuwa wanaupungufu wa magodoro ya kulalia watoto na kuomba wale wanaoguswa kuwasaidia watoto hao wajitoe ili kuwasaidia walimu kuiendesaha shule kwa urahisi.
“Kwa ujumla tuna matatizo katika upande wa malazi. Tuna ufungufu mkubwa wa magodoro ya kulalia watoto. Tunahitaji msaada wa hali na mali” alisema.
Mwenyekiti wa akina mama hao Emma Mwalusamba alisema kila jamii itambue kuwa jukumu la kulea watoto wenye ulemavu wa kusikia na kuona ni la kila mtu na kwamba jamii ikiwajibika ipasavyo watoto hao watapiga hatua mbele kwa kuwa hawatakuwa mzigo bali watajitegemea wenyewe kama watu wengine.
“Hawa watoto ni wetu. Kila mmoja atambue kuwa hata kama hakumzaa yeye, ni wetu sote. Naomba tuungane ili kuwasaidia watoto hawa kama ambavyo walimu wanajitahidi kwa kila wawezalo kuwahudumia watoto wetu.
“Watoto hawa hawakuomba kuzaliwa hivi bali walijikuta wamezaliwa wakiwa hivi. Kila anayezaa mtoto mwenye ulemavu hakupenda kumzaa mtoto wa namna hiyo ila tu inatokea amezaa jambo ambalo mimi na wewe linaweza kututokea wakati wowote. Inapotokea tusiwaache watoto kwamba hawawezi bali tuwapeleke shule wakasome kama watoto wengine” alisema Mwalusamba.
Mwalusamba alijikuta akitiririsha machozi na kushindwa kuendelea kuzungumza hali iliyosababisha akina mama hao kuanza kulia upya.
Naye mpishi wa shule hiyo Maria Mstaafa alishindwa kuzungumza pale alipopewa nafasi ili kupokea msaada wa akina mama hao na kuangua kilio kwa kusema kazi ya kulea watoto wasiosikia ni ngumu.
Kwa upande wake mwanafunzi Agata Muumba akiongea kwa niaba ya wanafunzi wenzake aliwashukuru akina mama hao kwa kuwakumbuka na kuwapelekea chochote na kuwaomba watu wengine kufanya hivyo kwa kuwa walimu wanakabiliwa na mambo mengi.
“Sisi wanafunzi tunashukuru sana na tunaamini walimu wamepunguziwa mzigo licha ya kuwa bado wanakabiliwa na mambo mengi yanayotuhusu sisi. Tunawaomba na watu wengine ambao wana moyo kama wenu watusaidie ili walimu wapate muda mzuri wa kutufundisha. Tunawakaribisha sana na Mungu awabariki” alisema Muumba.
Wanawake hao kutoka madhehebu mbalimbali ya Kikristo katika Manispaa ya Iringa ambao huwa na utaratibu wa kuwatembelea wenye shida mbalimbali walitoa msaada wa Mafuta ya kula lita 40, Sukari kilo 100, Mchele kilo 200, unga wa ngano kilo 100, Maharage kilo 100 na Dawa za meno pisi 200.
Mahitaji mengine ni Dawa za kufanyia usafi chooni lita 10, Chumvi katoni 2, Sabuni za kufulia boksi 12, Kalamu za wino na kalamu za mkaa 200, Madaftari pisi 300, Unga wa sembe kilo 300 na matunda.
Shule ya Msingi viziwa Iringa ambayo ipo chini ya Kanisa la Anglikana ilianzishwa na serikali mwaka 1993 lakini baadaye ikaomba mtu wa kuiendeleza na Kanisa la Anglikana likaichukua.
Hadi sasa ina jumla ya wanafunzi 124 ambapo kuna viziwi wa kawaida na viziwi ambao hawaoni ikiwa hadi sasa viziwi wasioona wapo tisa.
Je, wananchi wana maoni gani?
Zeno Kalinga amesema serikali iliyopo madarakani itoe kipaumbele kwenye vituo vya watoto yatima na wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kuwaongezea mshahara wahudumu wa vituo hivyo ili waweze kufanya kazi kwa majitoleo zaidi.
Amesema tofauti na ilivyo sasa serikali imekuwa ikiwa ikitoa mishahara mikubwa kwa baadhi ya watu na kuwaacha wale ambao hufanya kazi ngumu kwa kila siku wakipata babu.
“Hivi sasa tunaona wazi wapo watu wanafanya kazi hadi muda wa ziada wakitafuta laki moja na nusu wakati serikali inaweajali zaidi wajumbe wa Bunge la Katiba ambao hukaa kwa masaa machache tu.
“Serikali ibadilishe utaratibu huu kwa sababu wapo wanaoumia hawana kitu lakini wasiofanya kazi yoyote wanapata pesa nyingi. Hali kadhalika hata wajumbe wa Katiba wasiwe wabinafsi. Hebu waangalie kuwa kuna watu wanapata shida” alisema Kalinga.
Alisema kuwa hivi sasa kumekuwa na tabaka la makundi ya watu huku walio nacho wakiendelea kuwa nacho na wasio nacho wakiendelea kuteseka jambo ambalo linatia shaka kwa ustawi wa maisha ya wananchi.
Pia alisema ili nchi hii iweze kukua kiuchumi na kimaendeleo, ni lazima watu wakawa na uzalendo wa dhati badala ya watu wachache kujihodhisha mali za umma kwa matumizi yao binafsi.
Naye Belta Sangwa ameita serikali iliyopo madarakani isiwe na ubaguzi kwa baadhi ya makundi bali iwatazame zaidi watu ambao wanahudumia makundi maalum kama vile watoto yatima, wenye ulemavu na wazee.
“Kumlipa sawa mtu anayehudumia makundi maalum na mtu anayehudumia makundi ya kawaida si halali kwani mtu anayehudumia makundi maalum anatumia muda mwingi zaidi kuliko yule anayehudumia makundi ya kawaida.
“Serikali isitengeneze matabaka ambayo yanaumiza wananchi kwani kumekuwa na hali ya kuwakumbatia matajiri kuliko kuwakumbatia wale wanaofanya kazi na masikini ambao nao hulipa kodi sawa na matajiri” amesema Sangwa.
Aidha amesema serikali ikiweka usawa na kuelekeza nguvu kwa watu wenye ulemavu, jamii itaweza kuwajibika kwa umakini na kwa kujituma ili kuongeza uchumi wa Taifa kwani jamii nyingi zinatumia muda mwingi kuwahudumia watu wasiojiweza badala ya kufanya kazi zinazozalisha uchumi wa Taifa.
No comments:
Post a Comment