WANANCHI wa Kata ya
Ibumu Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa wamesema wanakaribia kutua mzigo na
kupunguza uchovu walionao ambao unasababishwa na utawala dhalimu wa kiimla
waliokuwa wakitawaliwa katani humo.
Wameyazungumza hayao
jana katika viwanja vya kijiji cha Kilala Kidewakatani humo katika uzinduzi wa
kampeni za kumnadi mgombea wa Udiwani kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) July Mpugula.
Mzee ambaye aliongea na
gazeti hili pembeni wakati mkutano ukiendelea akiomba jina lake lisiandikwe
alisema CCM imeanza kuagwa rasmi kutokana na viongozi wanaopitia chama hicho
kuwa ni viongozi wa matumbo na familia zao na kuwafanya wazee kuwa watumwa wao.
“Ndugu yangu anagombea
udiwani kupitia CCM lakini hata kwenye mikutano yake siwezi kwenda kwa sababu
namfahamu vizuri kuwa akiwa diwani huyo tutalia zaidi ya aliyekuwepo kabla.
Kweli nimeamini kuwa CCM wanataka watu wezi kwa sababu ndugu yangu huyu ni
mwizi wa kutupa kwenye vijiji vyetu lakini nimeshangaa chama kimemsimamisha
kuwa kugombea udiwani. Mimi mwenyewe ni CCM lakini kwa hapa! Haa! Siwezi kumpa
kura yangu” kilisema chanzo chetu.
Akimnadi mgombea Katibu
wa Chadema Mbeya mjini ambaye pia ni mkufunzi wa Chadema ni msingi Christopher
Mwamsiku alisema July amesimamishwa si kwa sababu ya urembo wake bali ni kwa
sababu ya uwezo wake na kuwataka wananchi kumuunga mkono ili autumie uwezo wake
kusimamia shughuli za maendeleo.
Akiongea kwenye mkutano
huo aliwataka Polisi kuacha vitisho kwa wananchi ambao wametulia kwenye
mikutano ya Chadema na kwamba chama kinalindwa kwa sababu ya umakini walio nao.
“Angalia sehemu zenye
tunu ndizo zinazolindwa kwa mfano angalia Benki zinalindwa, Madini yanalindwa,
taasisi za fedha na sehemu nyeti zote zinalindwa. Mikutano ya CCM Polisi
hamlindi na badala yake mmeelekeza nguvu kwenye mikutano ya Chadema. Kitu chochote
kinacholindwa ndicho cha maana zaidi” alisema.
Naye Mwenyekiti wa
Chadema Wilaya ya Kilolo Oliani Mkemwa alisema Wilaya ya Kilolo imekuwa shamba
la Bibi kutokana na kukosa usimamizi wa watu kutumia fursa hiyo kukwapua fedha
za maendeleo.
Alisema tatizo la wizi
katika Halmashauri ya Kilolo linatokana na kuwepo kwa madiwani wa chama kimoja cha
CCM ambao wote ni wapiga dili na kukosa meno ya usimamizi.
Patrick Ole Sosopi aliesema
kwa miaka 50 rasilimia za nchi zimeliwa na watu wachache ambao ni viongozi wa
CCM na kuwaacha wananchi wakihangaika bila sababu na kuwataka wananchi kuamka
na kutoa adhabu kwa watu wanaoiba rasilimali zao.
Alisema michango
imekuwa mingi licha ya wananchi kulipa kodi kila siku kwa sababu ya watu
kuwageuza wenzao kuwa chanzo cha kipato cha familia zao.
Mgombea udiwani kupitia
Chadema July Mpugula akijinadi alisema wananchi wamekuwa wakipigwa makofi kila
upande na viongozi wasio na huruma na kuomba wananchi wamchague ili aende
kuwatafuti kinachowapiga makofi.
“Naomba mnitume niende
nikawawakilishe kwenye Halmashauri ili niwajulishe nani amekuwa akitupiga
makofi kila kunapokucha tunaishi kama wakimbizi kutokana na watu kutufanya
watumwa.
“Siendi huko kwa sababu
ya kutaka kujinufaisha ila nataka kushirikiana nanyi kuleta maendeleo ambayo
watu wameyapeleka majumbani mwao. Wizi wa mali zetu nitahakikisha hakuna
anayetuibia kirahisi kama walivyokuwa wanafanya” alisema.
Katika mkutano huo
wanachama wa chama cha mapinduzi 46 walirudisha kadi za chama hicho na kujiunga
na Chadema huku wanachama wapya 102 wakijiunga na Chadema.
Kampeni za uchaguzi huo
zinakuja baada Kata hiyo kuwa wazi kutokana na aliyekuwa diwani wa kata hiyo
Jeremiah Ikanyagwa kufariki.
No comments:
Post a Comment