![]() |
| Rais Jakaya Kikwete. |
DIWANI wa Kata ya Ng’ang’ange Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa Namgales Msuva (CCM) ameingia katika kashfa ya kutoelewana na ndugu zake kwa kile kilichoelezwa kutumia cheo kupora ardhi na kufyeka miti iliyokuwa imepandwa.
Taarifa zilizolifiukia mtandao huu kutoka kwa mmoja wa familia hiyo zilielezwa kuwa diwani huyo ameanza kutoelewana na ndugu zake mara baada ya kupata madaraka na kutumia cheo chake kwa hila.
Licha ya kuwa taarifa zilitolewa kwa masherti ya kutotaka jina liandikwe mtandaoni, chanzo chetu kileeleza kuwa diwani huyo imefika mahala ambapo ameamua kufyeka miti ya mjomba yake Adriano Kikoti ambaye ni mtoto wa dada yake kwa lengo la kunyang’anya ardhi.
Pamoja na kuwa diwani huyo ni mjumbe wa baraza la ardhi kata ya Ng’ang’ange imeelezwa kuwa ni moja ya kigezo anachotumia kwa kuhakikisha anapata mali kwa mabavu.
“Tunashida kweli na huyu ndugu yetu. Sasa hivi amekuwa kama mkoloni ambaye hajali ndugu wala nini! Tunajiuliza kuwa udiwani wake aliambiwa afanye hivyo? Pia kuwa mjumbe wa baraza la ardhi anapaswa kutumia kwa kuwanyanyasa watu? Isitoshe, tunajiuliza kama sisi ndugu tunafanyiwa hivyo, je, watu wengine watapata haki?” kimeeleza chanzo chetu na kuhoji.
Alipotafutwa mjomba yake Adriano Kikoti kwa ajili ya kutolea maelezo suala hilo alikiri kuwepo mgogoro ndani ya familia ambao chanzo chake ni diwani.
Kikoti ambaye pia ni Katibu mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Ng’ang’ange amesema pamoja na kuwa yeye ni mwanachama wa chama hicho, vitendo anavyotendewa na diwani huyo si vya ubinadamu.
“Licha ya kuwa huyu ni mjomba yangu na pia ni diwani kupitia chama ambacho mimi ni mwenezi, huyu diwani hana busara. Ameacha kufanya kazi ambazo aliomba kura kwa wananchi na kutumia madaraka yake kwa mabavu.
“Sina nia ya kumsema vibaya mjomba yangu lakini kwa kweli amekuwa haramia mmo kitu ambacho ni kinyume na taratibu za uongozi. Kwa kuwa yeye ameshapata uongozi sasa anatumia mwanya huo kutumia nguvu kuwaonea wanyonge. Na hili si kwangu ama kwetu familia tu, bali ni kwa watu wote” amesema.
Pia amesema lengo lake ni kutaka kunyang’anya ardhi kwa kipindi ambacho yupo madarakani ili atakapotoka madarakani iwe mali yake.
“Amefyeka miti yangu 103 ambayo ina umri wa miaka 6. Miti haina kazi tena kwa sababu ni midogo hata kwa boriti haifai, lengo tu kutaka ardhi” amesema.
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho Aron Mwenzegule alipotafutwa kwa ajili ya kutoa ufafanuzi aemsema suala hilo analifahamu lakini halijamfikia kiofisi.
“Ni kweli naufahamu mgogoro huo kutoka kwa watu mbalimbali lakini halijafikishwa ofisini kwangu kwa ajili ya kutafuta suluhu ila likiletwa tutalifanyia kazi ili suluhu ipatikane” amesema.
Hata hivyo taarifa kutoka ofisi ya CCM Wilaya ya Kilolo zinaeleza kuwa diwani huyo anamatatizo tofauti na matarajio yaliyokuwepo.
Mmoja wa viongozi alitoa taarifa hizi kwa mashert ya kutotaka jina liandikwe kwa kuwa si msemaji na kwamba ilikuwa afadhari kuacha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuingia madarakani kuliko na tatizo lililopo sasa.
“Ni kweli Chadema ilikuwa inashinda kwa kishindo ila tulichokifanya tunafahamu wenyewe lakini sioni sababu ya kile tulichokifanya. Tulitumia gharama na nguvu nyingi kwa ajili ya huyu mzee lakini leo tunajuta kwa sababu imefika mahali anatutukana hata sisi viongozi wake wa Wilaya.
Katika hatua nyingine, diwani huyo alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa masuala hayo kwa njia ya simu alitumia lugha ya matusi kwa mwandishi na kusema kuwa analima shambani.
Hata hivyo alipotakiwa kuzungumzia chanzo cha mgogoro na familia alisema hawezi kuongea na mpumbavu.
“Siwezi kuongea na mpumbavu, mimi ni kiongozi huwezi kunifanya lolote. Sina ujinga wa kuongea na watu kama wewe na ukawaambie waliokuambia hivyo wote ni wajinga tu na wajue mimi ni kiongozi wao” akakata simu.

No comments:
Post a Comment