ZAHANATI ya kijiji cha Itimbo
Kata ya Rungemba Wilaya ya Mufindi katika Mkoa wa Iringa inahitaji daktari kwa
ajili ya kuwezesha utabibu kwa wagonjwa.
Akizungumza na mtandao huu
ofisini kwake, nesi na muuguzi wa zahanati hiyo Olesta Mahanga amesema daktari
anahitajika mapema kutokana na aliyekuwapo kuhamishwa bila kubadilishwa
mwingine.
Amesema daktari ananafasi yake
ndiyo maana anahitajika kwa haraka ili kuwezesha shughuli za utabibu kufanyika
kwa wagonjwa mbalimbali wanaofika kupata matibabu.
“Umuhimu wa daktari upo kwa
sababu ana nafasi yake. Daktari aliyekuwapo alihamishwa lakini hajabadilishwa
mwingine hata wa kuja kuripoti tu. Hivyo, kwa kweli daktari anahitajika” amesema
Mahanga.
Pamoja na uhitaji wa daktari
Mahanga amewataka wananchi kuwa waelewa kwa kile wanachoelezwa kuhusiana na
shughuli za afya kwa kuwa ni muhimu kwa ustawi wao na uwajibikaji mzuri wa
watendaji wao.
Akifafanua zaidi amesema wananchi
wamekuwa na kawaida kuwataka wahudumu kufanya kazi kwa muda wa masaa 24 bila
kupeana zamu jambo ambalo linahatarisha uwajibikaji kutokuwa mzuri.
“Uelewa wa watu bado ni mdogo.
Mtu anapofanya kazi anatakiwa kupumzika ili aifanye kazi vizuri lakini watu
wetu hapa wakimuona muhudumu mmoja tu wanaanza maneno na tumekuwa na kawaida ya
kupeana zamu ili kupata nafasi ya kupumzika.
“Wao wanataka muda wote hata
usiku tuwe kazini bila kupeana zamu. Kiafya siyo vizuri kufanya kazi bila
kupumzika na kibaya zaidi ukiwaeleza hali inavyokuwa wanaanza lawama na wengine
kutukana bila kujua ni nini wanakifanya. Tuwaombe tu kuwa na uelewa pale
tunapowapa maelekezo wajue” amesema.
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho
Abson Mangula alipotakiwa kutoa maelezo juu ya utendaji kazi wa wahudumu wa
zahanati hiyo amesema licha ya kuwa wawili tu, wamekuwa na utaratibu mzuri wa
kutoa huduma kwa kuhakikisha muda wote anakuwepo muhudumu.
Amekiri kuwepo na maneno ya watu
juu ya wahudumu hao kuwataka watoe huduma kwa muda wa masaa 24 bila kupumzika
na kusema kuwa hata wao ni binadamu ambao wanahitaji kupumzika kama wao
wanavyolala majumbani kwao na hivyo kuwataka wasiingilie mipango yao na kupokea
huduma kwa mhudumu ye yote watakayemkuta wakati wakihitaji huduma.
Alipoulizwa juu ya upatikanaji wa
dawa, Mahanga alisema dawa zipo za kutosha lakini tatizo lililokubwa ni kufanya
kazi katika giza nyakati za usiku.
“Tatizo lililokubwa ni nishati
kwa sababu nyakati za usiku anaweza kuja mgonjwa hasa akina mama wanapokuja
kujifungua lakini wanaweza wasije na taa na hapa hatuna taa za kutosha.
Tungetamani kama tungepata hata kasola ili tuweze kufanya kazi kwa urahisi.
“Tatizo lingine ni maji japo kuwa
sasa kisima kinachimbwa tunategemea kikiisha tunaweza tukajikomboa suala la
maji” amesema.
Wakati huo huo mkulima maarufu wa
miti katika Wilaya hiyo Gwelino Chang’a maarufu kwa jina la Matekeleza ameahidi
kusimamia suala la uchimbaji kisima cha maji katika zahanati hiyo ili
kurahisisha wagonjwa na wahudumu kupata maji kwa urahisi.
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho
Mangula amesema endapo Matekeleza atasimamia kama alivyokusudia, utakuwa ni
mwendelezo wa utekelezaji wake kwa kuwa hata zahanati hiyo alijenga mwenyewe
kwa kusaidiana na nguvu ya wananchi.
“Alipewa jina la “Matekeleza” kwa
kuwa ni mtu wa utendaji siyo ahadi. Zahanati hiyo pamoja na ofisi ya kijiji
alijenga mwenyewe kwa hiyo tunaimani kuwa atafanya wala hatuna wasiwasi naye
juu ya ahadi hiyo. Kila wakati yeye mwenye huwa ni mtu wa utekelezaji ndiyo
maana tulimpa jina hilo” amesema Mangula.
No comments:
Post a Comment