![]() |
| Rais wa Rwanda Paul Kagame |
Serikali ya Rwanda imetoa tamko linaloonesha
kutoielewa kauli ya Rais Jakaya Kikwete, iliyoamuru wahamiaji haramu kuondoka
nchini.
Rwanda kupitia waziri wake wa Mambo ya Nje, Louise
Mushikiwabo, alikaririwa akieleza kwamba hawatajibu mapigo agizo la Rais Jakaya
Kikwete ya kuwataka Wanyarwanda wote waliolowea Magharibi mwa Tanzania kuondoka
haraka.
Mushikiwabo alisema wako tayari kuwapokea na
kuwalinda wote waliofukuzwa Tanzania kwa kisingizio kuwa ni wahamiaji haramu,
akieleza kwamba anasikitishwa kwa kuwa Tanzania haikufanya jitihada yoyote
kuwasiliana na Rwanda kuhusu suala hilo kabla ya kuchukua uamuzi huo.
“Ni uamuzi ambao umeshachukuliwa, hatukushirikishwa
kwa namna yoyote na jukumu letu kama serikali na taifa ni kuwahakikishia ulinzi
wote wanaokuja, na hili ndilo suala tunalolishughulikia kwa sasa,” alisema.
Kwa mujibu wa gazeti la New Times, Mushikiwabo
aliwaeleza waandishi wa habari kwamba agizo hilo la Rais Kikwete pamoja na
ushauri wa kuitaka Serikali ya Rwanda kuzungumza na wanamgambo hasimu wa FDLR
waliopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hayatayumbisha uhusiano imara
baina ya Watanzania na Wanyarwanda.
“Sisi si majirani tu, tuna mfungamano imara baina ya
watu wetu pia, tuna mfungamano wa damu, wa kibiashara, na mengine mengi ya
kutufanya tuendelee kuwa pamoja,” alisema na kutumia fursa hiyo kuwakaribisha
Watanzania nchini Rwanda.
Watanzania wanaweza kuishi hapa kwa umri wowote
wanaotaka. Tunawachukulia kuwa ni watu wetu muhimu kwenye fungamano la Jumuiya
ya Afrika Mashariki,” alisisitiza.
Rais Kikwete wakati akihitimisha ziara yake mkoani
Kagera alitoa agizo la kuwataka wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na
wahamiaji haramu ama kuondoka au kuhalalisha ukazi wao, huku akitoa wiki mbili
kwa zoezi hilo kutekelezwa, kabla ya kuanza kwa operesheni ya kuwasaka watu
hao.
Kauli hiyo ilitokana na kushamiri vitendo vya
kihalifu katika eneo la Kanda ya Ziwa, Rais hakutaja jina la nchi ya wahamiaji
hao. Kwa ukanda huo Tanzania inapakana na Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na
DRC.
Pia, Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa
mwezi alizungumzia kusikitishwa na kauli za shutuma, kejeli na udhalilishaji
zilizotolewa na Rais Paul Kagame wa Rwanda dhidi yake.
Mvutano baina ya Rwanda na Tanzania ulianza kuwekwa
hadharani Mei mwaka huu, baada ya Rais Kikwete kuishauri Rwanda kukaa na
kuzungumza na FDLR wenye makao yao DRC, hatua ambayo haikuifurahisha Serikali
ya Rwanda.
Wakati Rwanda ikieleza hayo jana Katibu Mkuu
Kiongozi, Ombeni Sefue alizungumza na gazeti hili, na kutaka majibu ya kauli
hiyo ya Rwanda yatolewe na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiao wa kimataifa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mkumbwa Ally
alisema kauli iliyotolewa na Rais Kikwete ilikuwa ni ushauri, kwamba Rwanda
wanaweza kuukubali ama la.
“Kilichomkasirisha Rais Kikwete ni lugha za matusi
zilizokuwa zikitolewa na viongozi wa Rwanda, ila kwa hicho walichokisema
sidhani kama kitakuwa na tatizo kwetu,” alisema Mkumb
wa.
Alifafanua
kwamba, alipokuwa mkoani Kagera Rais Kikwete hakutoa agizo la Wanyarwanda
kufukuzwa, bali alitoa agizo la kuanza kwa operesheni ya kuwakamata wahamiaji
haramu, wale wanaomiliki silaha kinyume na taratibu.
“Rais
alizungumzia masuala ya jinai ‘Criminal Element’, siyo kuwafukuza Wanyarwanda,”
alisisitiza.
Hatutazungumza
na FDLR
Waziri
wa Mambo ya Nje, Louise Mushikiwabo, aliendelea kusema sera ya Rwanda kuhusiana
na makundi ya aina hiyo, iko wazi na haitabadilika, kauli ambayo amekuwa
akiirudia kila mara na kuwataka wote wanaofikiria kuhusu Rwanda kuzungumza na
FDLR kwa namna yoyote kusahau wazo hilo.
“Kama
umehusika kwa namna yoyote na maangamizi, wewe utakuwa adui wa kila mtu. Ni
wazi kwamba Wanyarwanda wote watakuwa kwenye majonzi iwapo kwa namna yoyote
kutakuwa na mawasiliano ya FDLR,” alifafanua.
Kundi
la FDLR ambalo ni kifupisho cha Democratic Forces for the Liberation of Rwanda,
linaundwa na watu walioshiriki kwenye mauaji ya kimbari yaliyowalenga watu wa
kabila la Watutsi mwaka 1994, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 800,000 kwa
miezi mitatu.
Kundi
hilo ambalo limeweka makazi yake mashariki mwa DRC, linadaiwa kufanya
mashambulizi kadhaa yakiwamo ya milipuko ya mabomu nchini Rwanda, ambapo mwezi
uliopita shambulio la aina hiyo mjini Kigali lilisababisha vifo vya watu watatu
na kujeruhi watu kadhaa.
Uhusiano
wa kihistoria
Familia
za Rwanda zikiwamo zilizoishi Tanzania tangu miaka ya 1950, zimeelezwa kuwa
zimekuwa zikiwasili nchini humo kupitia mpaka wa Rusumo baada ya agizo la Rais
Kikwete kuwataka wawe wameondoka ndani ya wiki mbili, kabla ya kuanza kwa
operesheni rasmi ya kuwaondoa.
Kwa
mujibu wa mamlaka nchini Rwanda, mamia ya Wanyarwanda waliokuwa wakiishi mkoani
Kagera ambako ndiko Tanzania inapopakana na Rwanda wamekuwa wakirejea kwa
wingi, ambapo hadi juzi, zaidi ya watu 300 walikuwa wameshaorodheshwa kwenye
ofisi za Uhamiaji.
Chanzo: Tanzania Mpya
Chanzo: Tanzania Mpya

No comments:
Post a Comment