HATIMAYE ripoti ya Tume ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora, kuhusu vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu na
mauaji yaliyotokea Arusha Januari 5, 2011 kwenye maandamano ya CHADEMA imevuja.
Licha ya ripoti hiyo kufichwa
kwa kutosomwa hadharani kwenye vyombo vya habari kutokana na kulishutumu moja
kwa moja Jeshi la Polisi, Mtandao huu umefanikiwa kuinasa.
Maandamano hayo ya CHADEMA ya
kupinga ukiukwaji wa kanuni na sheria katika uchaguzi wa Meya ya Manispaa ya
Arusha, Gaudence Lyimo, licha ya kuruhusiwa na polisi awali baadaye yalipigwa
marufuku na Mkuu wa Jeshi hilo nchini, IGP Saidi Mwema.
Hata hivyo, CHADEMA walikataa
kutii agizo hilo kutokana na taarifa ya IGP kutowafikia kwa maandishi kama
inavyoelekezwa kwa mujibu wa taratibu za utendaji wa jeshi hilo.
Kufuatia vurugu hizo za polisi
na wafuasi wa CHADEMA, watu watatu waliuawa kwa kupigwa risasi, wengine zaidi
yya 30 kujeruhiwa na wafuasi zaidi ya 70 wakiwemo viongozi waandamizi wa chama
ambao walifunguliwa mashtaka mahakamani.
Kutokana na tukio hilo Tume ya
Haki za Binadamu, iliunda tume iliyochunguza suala hilo Januari 10 hadi 13
mwaka 2011, kwa kuwahoji viongozi wa CHADEMA mkoa wa Arusha, Jeshi la Polisi,
hospitalini walipolazwa majeruhi na njiani walipoandamana wafuasi wa chama
hicho.
Tume hiyo iliongozwa na
Kamishna Joaquine De-Mello akiandamana na ofisa uchunguzi, Philipo Sungu,
kutoka idara ya elimu kwa umma na mafunzo kufuatilia tukio hilo kwa muda wa
siku tatu ili kupata picha halisi.
Lengo kuu lilikuwa kubaini
chanzo cha vurugu hiyo, uvunjwaji wa haki za binadamu ambapo Januari 11,
asubuhi tume hiyo ilianza kuonana na madaktari na wagonjwa majeruhi waliolazwa
katika hospitali mbili za Mount Meru na Seliani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo
ambayo gazeti hili linayo nakala yake, taarifa zilizopatikana katika hospitali
zilionyesha kupokelewa kwa majeruhi 26 katika hospitali ya Mount Meru na wawili
Seliani.
Majeruhi watatu walipoteza
maisha wakati wakipatiwa matibabu ya awali hapo hospitali ya Mount Meru, 22
walilazwa katika hospitali ya Mount Meru na watatu walipatiwa matibabu na
kuruhusiwa kuondoka hospitalini.
Ripoti ya madaktari
ilithibitisha kuwa vifo hivyo vilitokana na majeraha ya risasi za moto huku
majeruhi wengine wakithibitisha kupigwa risasi za moto huku wakionyesha
majeraha hayo kwenye miili yao.
Licha ya ripoti kuonyesha
vitendo hivyo vya uvunjifu wa haki za binadamu uliofanywa na polisi, inasema
kuwa maandamano ya CHADEMA na mkutano yalikuwa halali na jeshi ndilo
lilisababisha fujo hizo kwa kutofuata sheria.
“Tanzania inajivunia Katiba
inayoainisha vipengele mbalimbali vinavyotambua na kulinda haki za msingi za
binadamu, hivyo kama nchi nyingine inawajibika kwa Azimio la Ulimwengu la Haki
za Binadamu la mwaka 1948 (UDHR) ambalo ni mama wa matamko, makubaliano na
mikataba ya vizazi vyote vya haki,” inasema ripoti hiyo.
Kwamba Tanzania kama miongoni
mwa nchi wanachama zilizoweka sahihi na kuridhia mikataba hiyo zinawajibika
moja kwa moja “kuheshimu, kulinda, kutetea na kutekeleza” haki zilizoainishwa
kwenye mikataba husika.
Ripoti hiyo inaongeza kuwa
“kanuni za jumla za jeshi la polisi namba 403 kifungu cha kwanza inasema; Mtu
yeyote ambaye anataka kuitisha, kukusanya, kuandaa na mkutano wowote au
maandamano katika eneo lolote hadharani atapaswa kuwasilisha taarifa ya
maandishi si chini ya saa 48 kabla ya wakati mkutano au maandamano kufanyika
kwa ofisa wa polisi wa wilaya husika.
Na pindi anapopelekea taarifa
kwa maandishi kwa mkuu wa polisi wa wilaya anaruhusiwa kuendelea kuandaa, kuitisha,
kukusanya, kuunda, au kuandaa mkutano au maandamano kama ilivyopangwa.
Ila mpaka atakapopata taarifa
ya maandishi kutoka kwa Afisa Polisi wa Wilaya husika kueleza sababu za
kusitisha maandamano hayo.”
Ripoti hiyo inasema kuwa kwa
mujibu wa sheria hiyo, polisi “Officer in charge” wa eneo katika eneo hilo la
Arusha mjini ni OCD wa Arusha Mjini – ndiye aliyepaswa kutoa maelekezo ya
kuzuia maandamano na si Kamanda wa Polisi wa Mkoa au Inspekta Jenerali wa
Polisi.
“Kwa mantiki hii, taarifa ya
CHADEMA kwa polisi ilitosha kwa wao kuendelea na mipango yao ya maandamano na
mkutano kama inavyoelezwa kisheria,” anasomeka taarifa hiyo.
Pia inaonyesha kuwa Sheria Na.
tano (5) ya mwaka 1992 ya vyama vya siasa kifungu cha 11 vifungu vidogo vya (4)
na (6) na sheria Na. 1 ya 1939 ya polisi na huduma za mgambo kifungu 43.-(1),
(2), zilikidhi pia hitaji la CHADEMA kuendelea na mipango yao ya maandamano na
mkutano wa hadhara kama ilivyopangwa.
Kwamba Sheria Na.5, 1992 ya
vyama vya siasa kifungu 11. — (8) inasema: kama jeshi la polisi linasitisha
maandamano au mkutano taarifa hizo hutolewa kwa maandishi kueleza sababu, wala
si kutumia televisheni, kama ilivyojitokeza kwa tukio la Arusha.
“Hivyo CHADEMA walikuwa sahihi
kwa kuwa hawakupata taarifa ya kimaandishi licha ya polisi kudai kutoa barua
hiyo lakini walishindwa kuthibitisha madai yao mbele ya tume.
Ripoti hiyo pia inaongeza kuwa
askari walifanya vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya viongozi na
waandamanaji hasa wanawake bila kujali hali zao.
Kwa mfano wanatajwa mbunge wa
viti maalum Lucy Owenya na mke wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Josephine Mushumbusi,
kuwa walipigwa na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za miili yao.
Kwamba viongozi wa CHADEMA na
wananchi wengi walikamatwa na kuwekwa rumande katika kituo kikuu cha polisi
kati mjini Arusha.
“Askari waliwapiga waandishi wa
habari, waliwanyang’anya vifaa vyao vya kazi na kufuta picha na kazi walizokuwa
wanazifanya kwenye maandamano. Askari na waandamanaji walisababisha uharibifu
wa magari na mali za umma na wananchi.
“Aidha walisababisha upotevu wa
mali za wananchi zikiwemo simu mbili za mkononi za Owenya na fedha tasilimu sh
2,700,000 za majeruhi Ally Ogaga walizodai kunyang’anywa na askari, wakati
Ofisi ya CCM Mkoa wa Arusha ilivunjwa vioo kwa mawe na waandamanaji na nyumba
ya mwananchi Salum Ally iliungua kwa moto uliosababishwa na mlipuko wa bomu
lililoruka kutoka kwenye gari la polisi,” ilisomeka.
Chanzo: Tanzania Daima


No comments:
Post a Comment