ASASI isiyokuwa ya kiserikali ya
Tuwafikie Tanzania inayojihusisha na uhamasishaji wa elimu vijijini imeanza
kujenga maktaba katika kijiji cha Lugalo Kata ya Ilole Wilaya ya Kilolo
itakayoiwezesha jamii kupata nafasi ya kujifunza mambo mbalimbali ya kijamii.
Ujenzi huo umeanza baada ya
taratibu zote za kisheria kufuatwa ambapo ni mwanzo wa ujenzi wa maktaba katika
vijijini katika Mkoa wa Iringa.
Akizungumza na mtandao huu
katika eneo la ujenzi, mhamasishaji wa elimu vijijini kupitia asasi hiyo Bovan
Mwakyambiki alisema mpango huo utakamilika haraka endapo jamii itatoa mchango
wa ushiriki.
Amesema jamii inapaswa kujua
umuhimu wa elimu na kutumia muda wao kwa kukuza wigo wa elimu kwa watoto na
kizazi kijacho.
“Tunaanza ujenzi huu lakini huu
ni mwanzo wa uhamasishaji kwa kuwa tunampango wa kujenga maktaba nyingi vijijini
huko. Jamii yetu inauhitaji wa kujifunza mambo mengi hasa ya kijamii na hata
kilimo kinahitaji elimu.
“Shughuli hii itakwisha haraka
endapo jamii itatoa ushirikiano wa dhati ili kufanikisha mpango mzima ikiwa ni
pamoj na kutoa michango mbalimbali” amesema Mwakyambiki.
Ametoa wito kwa wale wenye kiu ya
kutaka maendeleo kuwa ili kukamilisha ujenzi huo, asasi inahitaji mifuko 300 ya
saruji na kwamba ni ruksa kwa mtu yeyote kuchangia.
“Tunaamini wapo wale wenye kiu ya
kutaka maendeleo kwa hiyo tunawakaribisha kushiriki nasi ila tunahitaji mifuko
ya saruji 300 kama wanaweza kuchangia tunawakaribisha sana” amesema.
Asasi ya Tuwafikie Tanzania ipo
kwenye mpango wa kujenga maktaba vijijini katika nchi nzima ili kupanua wigo wa
elimu nchini.

No comments:
Post a Comment