| Rais wa baraza la maaskofu Tanzania akiwa na wazee wa shirika la Mt. Agustino nje ya Kanisa la moyo Mt. Yesu Parokia ya Kihesa jimbo la Iringa mara baada ya Misa ya uzinduzi hii leo. |
| Baadhi ya wazee wa shirika la Mt. Agustino wakiwa nje ya Kanisa. |
RAIS wa Baraza la
Maaskofu Tanzania Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa amesema wazee wasisahaulike
katika huduma muhimu ili waendelee kutoa mang’amuzi yao mbalimbali katika
jamii.
Mhashamu askofu
ameyasema hayo katika maadhimisho ya Misa Takatifu iliyokuwa maalum kwa
uzinduzi wa shirika la wazee na wastaafu mbalimbali la Mtakatifu Agustino iliyofanyika
katika Kanisa la Kiaskofu la Moyo Mtakatifu wa Yesu Parokia ya Kihesa jimbo la
Iringa hii leo.
Amesema wazee ni tunu
ya familia na hivyo kuwatenga wazee hao ni kumkosea Mungu kwa kuwa wao ndio
mashahidi wa misingi ya Baraka.
Askofu Ngalalekumtwa
ambaye pia ni askofu wa jimbo la Iringa amesema ndio wanaoendeleza mapokeo
mbalimbali yaliyo katika misingi ya maadili na kuongeza kuongeza mang’amuzi ya
changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya watanzania.
Amesema
wazee wahudumiwe kwa upendo bila kubaguliwa na wapewe haki stahiki bila
kusumbuliwa kwa kuwa ni haki yao kupata mahitaji muhimu kama walivyo wengine.
“Kanisa
linashuhudia uwepo wa Yesu Kristo na hawa wazee ndio mashahidi wa misingi ya
wokovu na Baraka za Mungu. Wahudumiwe bila kubaguliwa” amesema.
Vile
vile amesema katika familia wazee wanarithisha tunu za familia hasa katika
maadili na mafundisho yenye hekima na busara.
Hata
hivyo ameitaka jamii kuwa na upendo kwa rika mbalimbali ambazo zipo katika
jamii kwa kuwa upendo ndicho kiini cha imani na amani.
“Upendo
unalea, unaleta nguvu, unafariji na ndicho chanzo cha amani na furaha kwa
binadamu anayehitaji kufarijiwa na kuhudumiwa sawasawa na mwingine” amesema.
Amesema
tunu za nchi ambazo ni zawadi ya kutoka kwa Mungu ziwanufaishe wazee ambao kwa
namna moja au nyingine ndio washauri wa mambo mbalimbali na pale wanapohitaji
haki zao kusiwe na ubabaishaji.
Ubabaishaji
wa makusudi katika utoaji huduma ni kinyume na haki za binadamu ambao ni haki
yao kupata huduma.
Amewataka
viongozi mbalimbali walio na mafundisho ya kikristo kutumia mafundisho ya
upendo katika kuihudumia jamii bila kujali rika na hasa kuwapa kipaumbele wazee
ambao umri wao umekwenda.
Naye
Mwenyekiti wa shirika hilo William Myonga amesema lengo la kuanzisha shirika
hilo ni kuwaunganisha wazee kwa ajili ya kutathimini yale yaliyowakumba wakati
wa ujana.
Amesema
yapo mengi ambayo katika ujana yamekuwa kikwazo kwao kiasi cha kusababisha
kumtumikia Mungu ipasavyo na hivyo kupitia shirika lao watapata nafasi ya
kukumbushana na kumuomba Mungu.
Mhamasishaji
wa shirika hilo Licas Mwasimile amesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali
hasa katika kupokelewa katika majimbo mbalimbali.
Mwasime
amesema changamoto mojawapo ni pale wanapohamasisha na kuambiwa kuwa shirika
halitambuliwi kitaifa licha ya kuwa elimu na maelezo juu ya kulitangaza shirika
hilo yanajitosheleza.
Ametoa
kilio cha wazee hao kwa baraza la baaskofu kuwasaidia kupokelewa kwa urahisi katika
majimbo yao ili kuwawzesha utume wao kuwa mwepesi.
Shirika
la Mtakatifu Agustino limeshafika katika majimbo 22 ambapo kwa kanda ya nyanda
za juu kusini limeshaingia katika majimbi ya Mbeya, Mbinga, Songea na Iringa.
Mlezi
wa shirika hilo Padre Gregory Mashtaka amewataka wazee wa shirika hilo kuwa na
mshikamano pamoja na mawasiliano.
“Si
kwamba mmekwisha kufika, huu ni mwanzo tu. Hali yetu ni ya uzee. Hivyo,
tuipokee kwa furaha” amesema Pd. Mashtaka.
Amewataka
wazee hao kuwa washiriki walio hai na si hoi kwa kuishi kwa ushirikiano na kuwa
na maisha ya utakaso.
Katika
uzinduzi huo, jumla ya wazee 89 walipokelewa katika shirika hilo la Mtakatifu
Agustino.
No comments:
Post a Comment