| Diwani wa kata ya Mivinjeni Manispaa ya Iringa Frank Nyalusi akiongea na wakazi wa Mkwawa na vitongoji vyake. |
| Mbunge wa Singida mashariki Tundu Lissu akiwahutubia wakazi wa Mkwawa na vitongoji vyake leo. |
“SERIKALI dhalimu
huondolewa na wenye hasira na waliochoka, kunyanyaswa na kudhulumiwa haki zao”.
Hayo yamesemwa na
Mbunge wa Singida Mashariki na mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani bungeni Tundu
Lissu katika mkutano wa hadhara uliomalizika hivi punde katika viwanja vya
Mkwawa nje kidogo na geti la Chuo Kikuu.
Lissu amesema serikali yoyote haiondolewi
madarakani kwa maombi bali kwa kutumia maamuzi ya kisiasa na kwa kupiga kura za
kuikataa hasa unapofika wakati wa kufanya uchaguzi.
Amesema mambo ya
kikaisari yanatatuliwa kikaisari na hali lilipofikia taifa la Tanzania, ni
pabaya ambapo wananchi wana kila sababu ya kukichukia chama tawa ambacho
kinawatia umasikini wananchi bila sababu.
“Usije ukadanganyika
kuwa ukimuomba Mungu utakuta CCM imetoka madarakani, haya ni mambo ya kikaisari
ambayo yanatakiwa kutatuliwa kikaisali hivyohivyo. Usidhani ukimuomba Mungu
pale utakapokuwa unamaliza sala utakuta CCM haipo, kamwe! Huu ni wakati wa
kuichukia na kuiondoa, haifai tena. Ila siwaambii kama musiende kumuomba Mungu,
saline lakini hakikiseheni mnachukua maamuzi ya kuiondoa CCM” amesema Lissu.
Amesema upinzani
wamekuwa na hoja za kuisaidia serikali lakini kwa sababu ya ufinyu wa fikra za
viongozi wa chama hicho, hoja zao zimekuwa zikipuuzwa kwa sababu ya uwingi wa watu
kwa kutumia “ndiyooo!” badala ya kuangalia mwenendo mzima wa maisha ya
watanzania.
“Ndugu zangu, kwenye
bunge letu tuna wabunge wachache tu na wengine wengi ni kundi tu la walaji ambalo
halina kazi yoyote” amesema.
Amesema CCM imegombana
na kila mtanzania kwa kila nyanja kwa kuwa kila kitu kinachofanyika na serikali
kinambana mwananchi.
Ameeleza kuwa serikali
imeingia katika mifuko ya hifadhi ya jamii na kutumia hela za watanzania bila
sababu huku ikiwanyima haki zao pale wanapostaafu.
“Kila kinachofanyika na
serikali kinatumia pesa za wananchi wanaoweka pesa zao katika mifuko yao bila
kuwaarufu wananchi wenyewe. Niwambieni kuwa leo hii kwa wewe unayeweka pesa
zaoko katika mfuko wowote wa jamii pindi utakapostaafu imekula kwako hutaipata
tena pesa yako kwa sababu watu wamegawana” amesema.
Amesema hakuna ambaye
halalamiki juu ya kile anachotendewa na serikali awe polisi, mwalimu, machinga,
mama lishe hata mwanafunzi.
Hata hivyo amesema
jeshi la polisi linalotumika na baadhi ya wanasiasa wa Chama cha Mapinduzi
limedhurumiwa na serikali kuliko hata
machinga.
Akifafanua zaidi
amesema kila wakati zimekuwa zikitolewa pesa kwa ajili ya mafunzo ya jeshi la
polisi, nyongeza za mishahara, likizo na kupandishwa vyeo lakini zimekuwa
zikipigwa juu kwa juu na viongozi wa chama tawala.
“Leo hii ugomvi wa
wanafunzi wa vyuo vikuu na serikali ni mkopo, nchi inadaiwa na benki za nje,
taasisi za fedha za nje na mashirika ya fedha, walimu na polisi pia; ni nani
hajaumizwa na serikali hii dhalimu?” amesema.
Amewataka watanzania
kupongezana kwa kazi ambayo imekwisha kufanyika na kuwakumbusha kuwa bado kuna
kazi kubwa ipo mbele yao kuhakikisha serikali dhalimu inaondoka.
Lissu amekwenda kinyume
na kauli ya Waziri William Lukuvi bungeni kuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Iringa
Michael Kamuhanda anafanya kazi nzuri na hivyo kumtaka aendelee na kazi hiyo
kuwa inaonesha dhahiri jinsi Chama cha Mapinduzi kinavyotumia jeshi la polisi
kuwakandamiza wananchi.
“Katika tume
zilizoundwa kuchunguza mauaji ya mwandishi wa habari Daudi Mwangosi ikiwemo
tume ya serikali ya tume ya haki za binadamu, ripoti inasema Kamuhanda Mwangosi
aliuawa kwa usimamizi wa Kamuhanda na ni muuaji lakini leo hii anasimama Waziri
halafu anasema Kamuhanda huyo huyo anafanya kazi nzuri! Inatisha sana” anasema.
Hata hivyo amesema
Kikwete pamoja chama chake wanatambua kuwa inchi ilipofika sasa mbele ni giza
tu kwa kuwa hakuna njia zinazowezakutumika kuwakomboa wananchi kwa udhalimu
wao.
Lissu amesema wananchi
wa hali ya chini ndiyo wanaokamuliwa kodi huku watoto wa viongozi na
wafanyabiashara wakubwa wakiachwa kwa sababu ndio walioinunua serikali.
Hata hivyo mwanafunzi
wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO) Olime Mwakilembe amesema imefika mahali CCM
inakata ushauri na kufanya mambo magumu kwa njia rahisi wakidhani wanatatua
matatizo na badala yake kuwapa mzigo wananchi.
Amesema hali ya maisha
ya watu ilipofika inatisha kwa sababu ya serikali legelege isiyo na masikio
inayotumia mabavu kuwalazimisha wananchi kuingia motoni badala ya kutumia
rasilimali watu kuokoa maisha ya watanzania.
“Matatizo magumu
wanafanya kwa njia rahisi. Ushauri wa maana wanaukata kwa sababu ya uhuni wao
wa kutumia mabavu na kuwanyanyasa wananchi ambao ndio walipa kodi
wanazoendeshea maisha yao na familia zao. Uhuni huu unafanyika kwa wazi kabisa
huku watanzania wakiuona” amesmea.
Amewataka watanzani
kutokufumbia mamcho matatizo yanapotokea ambayo chanzo kikuu ni viongozi
wanafiki waliojaa dhuruma na kujilimbikizia mali.
Hata hivyo amesema
wakati wa kuiaga CCM umefika na kiama chake kimekamilika ambacho ni Chadema.
Mkutano huo uliandaliwa
na shirikisho la vyuo vikuu Mkoa wa Iringa ambavyo ni Chuo Kikuu kishiriki cha
Tumaini Iringa, Chuo Kikuu kishiriki cha Mkwawa na Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO).
No comments:
Post a Comment