MKAKATI wa kumng’oa Mwenyekiti wa Mtaa wa Ngome Kata
ya Kihesa katika Manispaa ya Iringa Elizabeth Mkayula unazidi kushika kasi
baada ya ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa kumwandikia barua mwenyekiti huyo
kutaka akabidhi nyaraka za ofisi.
Taarifa zilizoufikia mtandao huu zimeeleza kuwa mkakati huo unalenga kulinga ubadhilifu wa fedha na vifaa
vya ujenzi katika soko jipya linaloendelea kujengwa katika mtaa huo.
Akizungumza kwa masikitiko
makali, mmoja wa kamati ya ujenzi wa soko hilo aliyeomba jina lake lisiandikwe
alisema mkakati huo ni wa makusudi ambapo ni watu wachache waliopanga kaufanya
hivyo kutokana na mwenyekiti huyo kuwa muwazi kwa wananchi.
Amesema kutokana na taarifa
zilizosomwa kwa wananchi juu ya ujenzi huo, zinatia shaka kwa kuwa mipango yote
inajulikana na kuwa taarifa ni za uongo.
“Ni kwamba umetokea wizi mkubwa
wakati wa ujenzi wa jengo la vyoo katika soko hilo. Mwenyekiti hakushirikishwa kwa kila
kitu ndiyo maana wanafanya kila linalowezekana kumuongoa mwenyekiti ili
wachukue mhuri kugonga nyaraka wanazotumia kwa kuiba ionekane mwenyekiti
alishiriki. Mimi nikiwa mmoja wa wanakamati ya ujenzi sikubaliani kabisa na
sitasaini gharama wanayosema imetumika kujenga kile choo kwa sababu ninajua
kila kitu” kimesema chanzo hicho.
Kwa nyakati tofauti wakazi wa
mtaa huo wameeleza kuwa utendaji wa kazi wa ofisa mtendaji wa mtaa huo Eliques
Ngakonda unatia shaka kwa sababu amekuwa akitumia imla kutaka wananchi wakubali
kila taarifa hata kama ni ya uongo.
Wameeleza kuwa ngakonda ameteua
baadhi ya watu ambao anashirikiana nao katika kufanya ubadhilifu na kuwatumia
hao kumpiga vita mwenyekiti wa mtaa ili asiendelee kuwaumbua kile
wanachokifanya.
“Jambo la kushangaza ni pale
mtendaji wa mtaa anapowateua watu wakushirikiana nao wakati mwenyekiti
tuliomchagua wananchi yupo halafu hawamshirikishi. Ina maana huyu mtendaji
ametuona sisi tuliyemchagua huyu mwenyekiti ni wajinga yeye tu mwenye akili?
Sasa tunamwambia kuwa sisi siyo wajinga, kama
tulivyompigia kura mwenyekiti huyo ndivyo tutakavyomkataa kuwa hatufai.
Wasituletee mambo ya ajabu hapa” amesema mwananchi mmoja.
Hata hivyo imeelezwa kuwa chanzo
cha mgogoro huo ni ofisa huyo kutompenda mwenyekiti kutokana na msimamo wake
kuwa ni wa haki kwa wananchi waliomchagua.
“Mwenyekiti tuliyemchagua sisi
hatolewi kama nyanya kwenye matenga ila
tukimchoka tutamtoa. Tunawashangaa wanamtoa wao kama
nani! Kwanza mtendaji mwenyewe si muadilifu
anataka atumie nafasi hiyo kutuburuza! Atatoka mwenyewe badala ya mwenyekiti. Kwanza sisi hatumjui aliyemchagua yeye na tunaweza
kumtimua mtaani hapa mara moja kuliko yeye anavyofikiri” kimesema chanzo hicho.
Mtandao huu umefanikiwa kunasa
barua iliyoandikwa katika ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa kumtaka mwenyekiti
huyo kuwasilisha nyaraka za ofisi.
Katika barua hiyo yeye kumbukumbu
namba IMC/A.50/06/37/33 iliyoandikwa Aprili 17, 2013 na kusainiwa na Erasto N.
Kiwale kwa niaba ya mkurugenzi anamtaka mwenyekiti huyo kuwasilisha nyaraka
zote za ofisi.
Hata hivyo barua hiyo haielezi makosa
yaliyosababisha mwenyekiti huyo kuondolewa katika nafasi hiyo.
Alipotafutwa kutolea ufafanuzi
juu ya kuondolewa katika nafasi hiyo, mwenyekiti wa mtaa huo Elizabeth Mkayula
amethibitisha kupokea barua hiyo na kueleza kuwa kosa lake halijui.
“Kweli nimeamini kuwa ukiwa mkweli
kwa wakati huu unageuka kuwa adui wa baadhi ya watu. Ni kweli nimekabidhiwa
barua kunitaka niende kukabidhi nyaraka za serikali za mtaa lakini kosa langu
silielewi. Lakini ninachoweza kusema ni kwamba, kuandamwa kwangu kulianza baada
ya kuuzwa kiwanja cha wazi. Diwani pamoja na mtendaji waliuza kiwanja cha wazi
nikaamua kufuatilia, walipoona nimelikalia kidete ndipo wakawatengeneza watu
wao waanze kunipiga vita” amesema Mkayula.
Hata hivyo, alipotakiwa kutolea
ufafanuzi juu ya ubadhilifu wa vifaa vya ujenzi alithibitisha na kusema ni moja
ya sababu inayomfanya sasa hivi kutengenezewa mikakati ya kuondolewa ili
lisijulikane kwa watu.
“Kuna makubwa zaidi ya hilo unaloniuliza kwani
sikushirikishwa kwa lolote katika ujenzi wasoko. Wanaogopa kunishirikisha
watashindwa kuiba kama ambavyo wamezoea kuiba.
Ila kuna baadhi ya nyaraka wanazotaka nirudishe mhuri ili wazigonge kwa sababu
wanaona kunijia kwa ajili ya kugonga mhuri nyaraka hizo nitawaumbua.
Walionichagua ni wananchi ambao wana mamlaka ya kunitoa wakati wowote tena
nikisia kuwa wananchi hawanitaki, nawajibika mwenyewe sisubiri kuwajibishwa”
amesema Mkayula.

No comments:
Post a Comment