masuguru

Tangazo la cheti

Tangazo la cheti
tangazo

KLERUU

KLERUU
KLERUU

CAPRICORN

CAPRICORN

Ibada

Ibada

Wednesday, March 13, 2013

DIWANI ADAIWA KUTUMIKA KUPANGA MIKAKATI YA KUMWACHISHA KAZI OFISA KILIMO

Simon Mangula Diwani wa Kata ya Itandula Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa


Ngwalanje Emmanuel ofisa kilimo wa Kata ya Itandula Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa akijibu tuhuma wakati wa mkutano wa mkuu wa wilaya Evarista Kalalu uliofanyika 18 Februali Mwaka huu katika kijiji cha Kimilinzowo.

DIWANI wa kata ya Itandula Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa Simon Mangula (CCM), anadaiwa kutumika kupanga mikakati ya kumfukuza kazi ofisa kilimo wa kata hiyo kwa madai kuwa ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Chanzo cha kuaminika kutoka katika ofisi ya Wilaya kimeeleza kuwa mikakati hiyo ni mwendelezo wa adhima ya kufukuza ofisa huyo baada ya kushindikana katika mkutano wa hadhara uliofanyika 18 Februali Mwaka huu katika kijiji cha Kimilinzowo ulioongozwa na Mkuu wa Wilaya Evarista Kalalu kwa lengo hilo na wananchi kubaini mbinu hizo jambo walilolipigia kelele.

Chanzo chetu cha habari kimeeleza kuwa, Mkuu wa Wilaya hiyo baada ya kushindwa kumfukuza katika mkutano wa hadadhara, mbinu zingine za kichinichini zimeanza kufanyika ili kufanikisha hilo kwa madai kuwa kama lengo hilo halitatimia, na kasi ya CHADEMA kuendelea kama inavyoendelea sasa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kipo hatarini.

“Nchi hii kama kweli ina uhuru, kwa nini mtu asichague kufanya kile anachoona kizuri kwake? Baada ya kuona wananchi wamegundua mbinu inayotaka kutumika kumfukuza ofisa kilimo wao na kuipigia kelele waliamua kuahirisha vinginevyo wangelazimisha siku ile kwenye mkutano wa hadhara wananchi wangechukua uamuzi ambao siyo mzuri. Lakini wameamua kutumia mbinu nyingine kukaimisha watu uongozi ili lengo lao liweze kutimia. Kwa upande wangu sioni haja ya kufanya hivyo ila jambo la msingi ni kuangalia kazi zinafanyika? Tukifanya kazi kisiasa hatuwezi kufika popote. Huu ni uonezi” kilisema chanzo hicho na kuhoji.

Chanzo hicho kimeeleza kuwa aliyepewa kazi ya kuhakikisha ofisa huyo anang’olewa ni diwani wa Kata hiyo Simon Mangula pamoja na ofisa mtendaji wa kata hiyo Ngano Francis aliyekaimishwa kwa ajili ya kufanikisha mikakati hiyo.

“Diwani huyo ni wa CCM na ofisa mtendaji aliyekamishwa ameahidiwa kupewa cheo kamaili cha kuwaofisa mtendaji mara atakapo kamilisha shughuli hiyo” kilisema chanzo hicho.

Katika hatua nyingine 11 Machi mwaka huu, kilifanyika kikao cha kamati ya maendeleo ya kata hiyo kujadili maendeleo lakini baada ya kuanza kikao hicho wakaanza kumkajadili ofisa kilimo huyo jambo lililosababisha wajumbe wa kamati hiyo kutofautiana.

Kwa mjibu wa habari kutoka katika mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo zinaeleza kuwa mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni diwani aliwataka wajumbe kupiga kura za kutokuwa na imani na ofisa huyo jambo lililowagawa wajumbe katika makundi mawili yasiyoelewana kufanya hivyo na kikao kuvunjika.

“Kawaida kikao cha kamati ya maendeleo huwa kinajadili maendeleo siyo watu lakini cha kushangaza siku hiyo mwenyekiti wa kikao ambaye ni diwani akaanza kumjadili ofisa kilimo wetu na kibaya zaidi tulichoona siyo haki ni pale walipotutaka wajumbe kupiga kura za kutokuwa na imani naye wakati yeye hayupo na hajapewa nafasi ya kuzungumza.  Lakini hata angepewa kazi nafasi ya kujieleza kwa upande wetu hatuoni kosa kwake kwa sababu anafanya kazi kwa kujituma wala hakuna anayemlalamikia kuwa anamuonea. Huu ni uonezi tena wa machomacho” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kimeeleza kuwa agenda zilizoanza kujadiliwa tofauti na matarajio ni pale ziliposomwa agenda 3 zinazomhusu ofisa kilimo ikiwemo agenda ya ofisa huyo kuwa mwanachama wa CHADEMA, ofisa huyo kuwahamasishwa wananchi wasifanye shughuli za maendeleo na kuhamasisha kutokuwepo na amani.

“Agenda hizo zote zilikuwa batili kwetu kwa sababu ofisa huyo tunamfahamu hajawahi kufanya upuuzi huo wanaomtwisha lakini kuwa mwanachama wa chama chochote cha kisiasa ni haki yake kikatiba ila tunachoangalia kazi zinafanyika ipasavyo? Ingekuwa kazi hafanyi hilo ni jingine lakini kazi zinafanyika na anatumia hata muda wa ziada kuwahudumia wananchi bila kutaka malipo. Uonezi huu hatutauvumilia na kama watalazimisha kufanya hivyo, wajue wazi kuwa wao ni chanzo kikubwa cha uvunjifu wa amani katika maeneo yetu” kilisema chanzo hicho.

Imeelezwa kuwa kikao kilichoshindikana kufanyika baada ya wajumbe kutofautiana kwa kutakiwa kupiga kura za kutokuwa na imani na ofisa huyo, sasa kitafanyika 18 Machi Mwaka huu katani hapo kuendeleza kujadili agenda zilizowatofautisha wajumbe.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika uliofanyika 18 Februali Mwaka huu katika kijiji cha Kimilinzowo, Mkuu wa Wilaya alijitoa katika mkakati wa kumfukuza kazi ofisa huyo baada ya kugundua kuwa tatizo siyo ofisa huyo bali ni serikali nzima ya kijiji na kata kwa ujumla kwa kukandamiza haki za raia ikiwa ni pamoja na kuuza ardhi bila kuwashirikisha wananchi, kuwatoza faini pasipo haki na kuwafanyia ubabe pale wanapohoji mapato na matumizi ya vijiji vyao.

Mwenyekiti wa CHADEMA katika Kata ya Itandula, Titus Kaduma alisema kwa sasa mikakati hiyo inafanywa na diwani pamoja na ofisa mtendaji wa kata kwa nia ya kupata vyeo hapo baadaye wakikamilisha zoezi hilo.

“Llakini sisi wananchi hatulali na hatutakubali kuendelea kuona uonezi huo ambao kimsingi ni matakwa ya watu wachache na siyo wananchi. Ubabe kama huu hatuuhitaji katika maisha yetu. Sasa imetosha” alisema.

Naye ofisa kilimo huyo, Ngwalanje Emmanuel alipoongea na gazeti hili alisema hana mengi isipokuwa anasubiri kikao ikatakachofanyika Machi 18 Mwaka huu.

Akiongea kwa njia ya simu, Diwani wa Kata ya Itandula Simon Mangula amekiri kuwepo na kikao hicho ambacho japo alishindwa kueleza kuvunjika kwa kikao hicho.

“Sikatai kuwa tulikua na kikao ila kuvunjika kwa kikao hicho sihui japo kuwa ni kweli ofisa kilimo huyo kazi zake zina mashaka kwa sababu anafanya kazi za siasa kunadi CHADEMA wakati yeye mtumishi” alisema diwani Mangula.

Hata hivyo alisema hakuna taratibu za kumfukuzisha kazi kwa kuwa yeye hana mamlaka ya kumfukuza kazi mtumishi licha ya kuwa ana maamuzi ya kumchukulia hatua mtumishi anapokwenda tofauti na taratibu za kazi.

Awali, Februari 4 mwaka huu ofisa kilimo huyo aliitwa na Mkuu wa Wilaya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama kumhoji kwanini anajihusisha na masuala ya siasa na kumtaka aandike barua ya kuacha kazi jambo alilolikataa na kusema ni unyanyasaji kwa kuwa utaratibu wa kazi anauelewa, na anaufuata.

No comments:

Post a Comment