![]() |
| Moja ya jengo la Shule ya Msingi Kitwiru lililobomoka. Majengo hayo yalijengwa tangu mwaka 1953 ilipokuwa ikianza shule hiyo. |
![]() |
| Sehemu ya jengo la Shule ya Msingi Kitwiru iliyobomoka. |
Shule ya Msingi Kitwiru iliyopo
Kata ya Kitwiru katika Manispaa ya Iringa iko hatarini kukwama kielimu kutokana
na kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa vymba vya madarasa
6.
Akiongea na mtandao huu leo, mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Chelestino Mage amesema upungufu
wa vyumba vya madarasa hayo unatokana na kuanguka kutokana na uchakavu kwa kuwa
majengo yaliyopo ni ya muda mrefu.
Pamoja na upungufu wa vyumba vya
madarasa Mage amesema shule hiyo pia ina kabiliwa na upungufu wa madawati 103
pamoja na nyumba 5 za kuishi walimu.
Shule hiyo ambayo ni kongwe
kuliko shule zote za Manispaa yenye jumla ya wanafunzi 683, wanafunzi
wanakabiliana na changamoto ya ukaaji wakati wa vipindi madarasani kutokana na
madawati yaliyopo kutokukidhi haja.
Kwa mujibu wa taarifa
zilizoufikia mtandao huu awali zilieleza kuwa shule hiyo ina nyumba za waalimu
6 na kuwa waalimu waliopo wana nyumba za kuishi.
Katika utafiti uliofanywa na mtandao huu, umebaini kuwa kati ya nyumba 6 zilizoelezwa awali, ni mwalimu
mmoja tu ambaye anaishi kwenye nyumba ya shule ambamo ameamua kutenga chumba
kimoja kwa ajili ya ofisi kutokana na majengo kutojitosheleza huku waalimu
wengine wakikosa mahali pa kuishi na kulazimika kupanga mitaani kwa gharama
zao.
Mage amesema tayari taarifa
hizo zipo katika ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ili kuzifanyia kazi ikiwa ni
pamoja na kumpeleka injinia wa Manispaa kwa ajili ya kufanya tathimini ili
waweze kuomba michango kwa wazazi na wadau mbalimbali wa maeneo hayo kwa ajili
ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Taarifa hizo zilithibitishwa na
ofisa mtendaji wa kijiji cha Kitwiru Edgar Mtono kuwa shule ilipo sasa ina hali
mbaya kutokana na majengo kuanguka yenyewe kutokana na uzee pamoja na upungufu
wa madawati.
“Kiujumla shule ina changamoto
nyingi ambazo siwezi kuziorodhesha zote lakini kikubwa ni majengo ya vyumba
vya madarasa, madawati na nyumba za walimu” amesema Mtono.
Shule ya Msingi Kitwiru
ilianzishwa mwaka 1953 kabla ya kuundwa kwa chama cha TANU.



No comments:
Post a Comment