| Wanafunzia wa shule ya sekondari Mwembetogwa wakisikiliza namna ya kuepukana na vitendo vinavyoweza kukatisha masomo kwa wanafunzi. |
Haya yalizungumzwa jana na Mkurugenzi mtendaji wa Tanganyika Centre for Development and Advocacy (TCDA) Jackson Kiyeyeu alipokuwa akiongea na wanafunzi wa Mwembetogwa juu ya kuepukana na vitendo vinavyoweza kuwasababishia kukatisha masomo.
Kiyeyeu alisema baadhi ya watu wanatumia vyeo, nyadhifa na nafasi zao kwa kuwaharibu watoto wa shule ama kwa kutumia pesa huku wakijua kuwa hawatendi haki.
“Huwezi ukazungumzia jambo hili bila kutoa machozi kama huna moyo wa chuma. Msiwe watu rahisi hasa sana akina dada. Wapuuzeni hao wanaowarubuni. Msikubali ujinga wao” alisema Kiyeyeu.
Alisema watu wanaowapa wanafunzi ujauzito kwa hali ya kawaida huwezi kuwadhania kwa kuwa walitakiwa kuwa wawe mfano mzuri wa kuigwa kimalezi lakini wao ndio wanaongoza kuwa na tabia chafu.
“Utandawazi huu wengi wetu tunautumia vibaya. Upuuzi ni mwingi kuliko busara. Tatizo watu wanafanya mambo kwa mazoea bila kuwa na mtazamo wa mbali. Tubadilike na tubadili tabia zetu. Kibaya zaidi unapata mimba
na Ukimwi juu” alisema.
Hata hivyo alisema wapo baadhi ya watu ambao wanadhani kutoa mimba ni kukwepa tatizo kumbe ni kuongeza tatizo juu ya tatizo.
“Wazee ambao ni rutuba ya taifa wamekuwa kikwazo kwa vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa kwa pale wanapoamua kwa makusudi kuwakatisha mabinti masomo. Huo ni uhaini”
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo, Jinsia na Mahusiano katika asasi hiyo Upendo Nsemwa alisema wapo wazazi ambao wanajiheshimu wanaotakiwa kuigwa na hivyo watumiwe kimaadili na kimalezi.
“Msipende hela badala ya kusoma, msipende starehe badala ya masomo na lililo la msingi zaidi ni kujiheshimu” alisema.
Hata hivyo wanafunzi walieleza kuwa, wanaoongoza kwa kuwapa wanafunzi ujauzito ni wanafunzi wa vyuo vikuu kwani wamekuwa wakitumia pesa za mikopo kwa kufanya starehe na kuwarubuni wanafunzi wa shule za msingi
na sekondari.
Huu ni mwendelezo wa kupambana na mimba mashuleni unaofanywa na TCDA katika Mkoa wa Iringa baada ya uzinduzi uliofanyika katika shule ya sekondari ya Mkwawa hivi karibuni.
Kuanzia mwaka 2006 hadi 2011, zaidi ya wanafunzi 40 walikatishwa masomo katia shule za msingi na sekondari zilizopo Manispaa ya Iringa huku kwa mwaka 2012 pekee wanafunzi 30 wakikatishwa masomo kwa sababu ya ujauzito na shule ya sekondari ya Mkwawa ikiongoza kwa wanafunzi
10.
No comments:
Post a Comment