masuguru

Tangazo la cheti

Tangazo la cheti
tangazo

KLERUU

KLERUU
KLERUU

CAPRICORN

CAPRICORN

Ibada

Ibada

Tuesday, January 15, 2013

Wanachuo wamzomea Dk. Ishengoma



MKUU wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, amechafua hali ya hewa katika kongamano la elimu lililokuwa likiwahusisha wanafunzi wa vyuo vikuu vya Iringa baada ya kuingia ukumbini akiwa ameongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama kana kwamba alikwenda kushughulikia masuala nyeti yanayohatarisha amani.

Kongamano hilo maalumu kwa ajili ya kuadhimisha sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar, miaka 50 ya uhuru wa Tanzania bara na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu, lilivihusisha vyuo vikuu vya Tumaini (IUCo), Ruaha (RUCo), Mkwawa (MUCE) pamoja na chuo cha elimu Kleruu ambacho kinatoa elimu ngazi ya stashahada.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ruaha ambacho ni chuo Kishiriki cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Olive Mwakilembe, alihoji kamati hiyo kuwepo kongamano hilo la elimu ilikuwa na maana gani jambo lililosababisha kuibuka kwa hoja za kuonesha kupingana na hali hiyo.

“Kwanza nasikitika sana kwa kitendo cha mkuu wa mkoa kuja hapa na Kamati ya Ulinzi na Usalama katika kongamano hili, najiuliza, kwani hiyo kamati yake ina mchango gani kwenye kongamano hili, mkuu wa mkoa umetudhalilisha na umeidhalilisha sekta ya elimu kwa ujumla” alisema.

Mwanafunzi huyo alisema katika jambo kubwa la kusikitisha, vinapojitokeza vikundi vya uvunjifu wa amani serikali inakaa kimya na kuchekelea, lakini katika masuala ambayo hayahitaji ulinzi na usalama wanatembea na ulinzi.

Naye mwanafunzi wa RUCo, Nicolaus Mpandula, akiunga mkono hoja hiyo alisema viongozi wengi wa nchini ni wanafiki kwa kuwa wanataka kujilinda wenyewe na kuwaacha raia wakiuawa bila sababu.

“Tatizo kubwa la viongozi wetu ni wanafiki kwa sababu wanataka wao kulindwa zaidi na kuwaacha wananchi wakifa, na wakati mwingine wanafurahia wananchi wanapokufa. Hii inaonesha ni mwendelezo wa ukandamizaji wa uhuru na matumizi mabaya ya dola,” alisema.

Rais wa Chuo cha Ruaha, William Rufil alisema serikali inapoacha vitendo vya kihalifu huku wakitaka kutumia dola kwa manufaa ya familia zao, ni sawa na samaki anayekwenda kinyume na mkondo wa maji.

Alipopewa nafasi ya kuzungumza katika kongamano hilo Dk. Ishengoma aliwalaumu wasomi kwa kudai kuwa wameishiwa maneno na badala yake wanatumia matusi jambo lililowafanya wasomi hao kumzomea.

“Mahali popote pale pana changamoto na kiongozi mzuri hakimbii matatizo, anakabili changamoto, msilalamike kila wakati, toeni mawazo yenu ili muisaidie serikali iweze kuyaboresha. Nilipokuja hapa niliyatarajia haya kwa sababu mimi ni mkufunzi najiona niko darasani,” alisema Dk. Ishengoma.

Naye Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa (CHADEMA) alisema katika kongamano hilo kuwa, mfumo wa elimu uliopo ni wa kizamani kwa kuwa uliundwa na wakoloni kwa kukidhi mahitaji ya wakati ule, lakini kutokana na fikra finyu za wasimamizi waliopo haisongi mbele.

No comments:

Post a Comment