Na
Happiness Elias, Iringa
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kimemtaka
Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dokta Jakaya Mrisho Kikwete kueleza
amepata wapi mamlaka ya kuisemea tume ya katiba kufuatia tamko lake alilotoa
usiku wa kuamkia mwaka mpya 2013, juu ya maendeleo ya mchakato wa katiba mpya.
Akiongea katika mkutano wa hadhara uliofanyika
katika viwanja vya Mwembetogwa Manispaa Iringa Januari 3 mwaka huu katika
viwanja vya Mwembetogwa, Mbunge wa Singida Mashariki Mh.Tindu lissu alisema
kuwa, Rais anatakiwa kueleza amepata wapi mamlaka ya kupanga ratiba juu ya
katiba mpya itapatikana na kwa taratibu zipi.
Lissu alisema kuwa kwavile sheria inasema,
Rais atajua maendeleo ya mchakato wa katiba endapo atapelekewa ripoti kutoka
tume ya katiba, hivyo CHADEMA imemtaka Rais kueleza amejua lini, na nani
amemuambia kwamba tume itamaliza kazi yake itakapofika mwezi Julai.
“Kama hana majibu ya maswali hayo, tunataka
mwenyekiti wa tume ya katiba Jaji Joseph Warioba atuambie kwa nini Rais
anazungumza mambo hayo, atuambie nani miongoni mwa wajumbe wa tume ambaye
anapeleka maneno hayo Ikulu na atuambie tupate hizi taarifa kabla ya Januari 14
mwaka huu, kwani Januari 14 tutaanza kamati za bunge” alisema Lissu.
Kwa muujibu wa sheria yamabadiliko ya katiba
tume inatakiwa kufanya kazi kwa miezi 18 ambapo mpaka sasa tume hiyo inamiezi
saba tangu ianze kazi na ingetarajiwa kumaliza kazi yake Desemba 1 mwaka huu.
Rais alisema kwamba kazi ya tume ya katiba ya
kuandaa rasimu ya katiba mpya itakamilika Mei 5 mwaka huu ambapo tume hiyo
itamaliza kazi yake, pia alisema kuwa baada ya mwezi Mei tume ya katiba itaanzisha
mabaraza ya katiba yakayojadili rasimu ya katiba mpya kazi itakayofanyika kati
ya mwezi Juni hadi Agusti mwaka huu na baada ya hapo bunge maalumu la katiba
litakutana mwezi Novemba mwaka huu kuipitisha katiba mpya.
Kutokana na maelezo ya Rais Kikwete kuhusiana
na mchakato wa katiba alisema kuwa, kama kila kitu kitaenda kama
wanavyotarajia katiba mpya itapatikana 2014 nchi itakapofikisha miaka 50 ya
muungano.
“Sasa ndugu zangu hayo ni maneno ya Rais
kuhusiana na mchakato wa katiba, hoja yangu ni kwamba, Rais Kikwete na Serikali
yake na Chama chake wanahujumu utaratibu wa kupata katiba mpya, hali
itakayosababisha Watanzania kupata katiba mpya kwa jina huku ikiwa na mambo
yale yale ya kumkandamiza Mtanzania”
Alisema kuwa Tume ilianza kazi rasmi Juni 1
2012 ambapo kuanzia kipindi mambo yote juu ya tume katiba yamekuwa
yakizungumzwa hadharani na mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Warioba.
Jaji Warioba ndiye
msemaji wa Tume ya mabadiliko ya katiba na ndiye anayepaswa aeleze ratiba ya tume ikoje, na
kwa muujibu wa sheria hiyo, mtu pekee anayeweza kutuambia kazi ya mchakato wa
katiba itaisha lini ni Jaji Warioba pekee.
“Sijaona mahali popote ambapo sheria hii
inatamka kwamba Jakaya Mrisho Kikwete amekuwa msemaji wa tume ya katiba.
Sijaona mahali pameandwikwa Waziri mkuu Mizengo Pinda au Mawaziri wengine wa
Kikwete au mwanashiria mkuu
wake ni wasemaji wa Tume. Wanaotakiwa kutuambia kinaendelea gani ni tume ya
mabadiliko ya katiba chini ya Mwenyekiti wake Jaji Warioba na sio Rais Kikwete”
Alisema kuwa kwa muujibu wa sharia kifungu cha
8(3) kinachosema kuwa Tume itakamilisha kazi yake ndani ya kipindi kisichozidi
miezi 18 kuanzia kuanzia tarehe ya kuanza kazi.
Kutokana na sheria hiyo, tume ya mchakato wa
katiba ilianza Juni 1 2012 hivyo inapaswa kumaliza kazi Desemba 1 2013 na sio
mwezi Mei 2013 kama alivyosema Rais Kikwete,
na kudai kuwa huo ni mwanzo wa utaratibu wa kuchakachua mchakato huo.
Pamoja na urais wake, hana mamlaka ya
kuzungumzia chochote juu ya kazi ya tume kabla tume haijamaliza kazi yake na
kumkabidhi ripoti. sheria hii ya mabadiliko ya katiba kifungu cha 20(1) inasema
kwamba, baada ya kukamilisha kazi yake tume itawakalisha ripoti kwa Rais
Kikwete na Rais wa Zanzibar ,
ataijua ripoti pale tume itakapomaliza kazi yake na kumpelekea.
“Hii ya kusema atamaliza mwezi Mei ameitoa
wapi? Nani amempelekea taarifa hizo? Kwenye sheria hii hakuna maali popote
ambapo tume au mtu mwingine yeyote anaruhusiwa kumpelekea Rais taarifa yeyote
kabla ya kazi ya tume kukamilika”
Aliongeza kuwa,Rais kuingilia kazi ya tume
anavunjwa sheria ya mabadiliko ya katiba kutokana na kifungu cha 10 kinachosema
kuwa tume itakuwa na mamlaka na uhuru kwa kadri itakavyokuwa muhimu kwaajili ya
utekelezaji wa majukumu na mamlaka yake chini ya sheria hii na haitaingiliwa na
mtu au mamlaka yeyote.
Alihoji yakuwa Kikwete atakuwa na makusudi
gani ya kuhakikisha tume inamaliza kazi yake kabla ya muda ambao sheria
imeuweka.
Aidha alisema kuwa kutokana na kifungu cha
sheria cha 20(2), baada ya ripoti kupelekwa Rais, Rais anatakiwa ndani ya siku
31 atoe tangazo katika gazeti la Serikali litakaloitisha bunge la katiba juu
tarehe na mahali ambapo bunge la katiba litakaa.

No comments:
Post a Comment