WAZAZI na walezi wametakiwa kuwafundisha watoto wao kuwa wavumilivu pale wanapotendewa vibaya na wenzao ili kuwawezesha kuwa na roho ya msamaha na huruma.
Haya yamezungumzwa na Rais wa Baraza la maaskofu Tanzania Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa katika kongamano la watoto lilofanyika jana katika Kanisa la Mt. Joseph Mfanyakazi Parokia ya Ipogolo Jimbo la Iringa.
Alisema vitendo vichafu na vya kikatili vinavyotokea ni matokeo ya kutowafundisha watoto uvumilivu, msamaha na huruma na kusababisha kukuwa katika roho ya ukatili na visasi.
Mhashamu askofu Ngalalekumtwa ambaye pia ni askofu wa jimbo la Iringa alisema kama wazazi na walezi hawatakuwa na tamaduni za kuwafundisha watoto wao kuwa na msamaha na kumjua Mungu, taifa lijalo litakuwa ni taifa la hila na chuki kwa kuwa na migogoro isiyokwisha.
Alisema watu watu wanapofanya vitendo viovu mbele ya watoto wao, watoto hurithi na kuendeleza katika maisha yao wakijua ni mambo ya kawaida.
“Tunapofanya vitendo viovu, vya kijambazi, kikatili na vya kihuni, watoto wetu wanatuiga na kuendeleza katika maisha yao. Hapo ndipo tunajenga taifa la kikatili na la kihuni kwani matendo machafu hayatakwisha kwa kuwa yamekwisha kujengeka katika akili za watu. Tuepukane na vitendo hivyo ili tujenge taifa lenye kupenda uhai wa wengine” alisema.
Alisema jamii iwafundishe watoto ukweli ili katika makuzi yao wajue kusema ukweli na kuacha uongo ambao umekuwa ukisababisha mabishano yasiyo ya lazima kutokana na wachache kufanya ujanja ujanja kwa kuwahadaa wenzao kwa maslahi yao binafsi.
“Tuwe wakweli ili watoto wetu wawe wakweli. Tunapokuwa wadanhanyifu tunatoa fursa kwa watoto wetukuwa hivyo hivyo. Malumbano na migogoro iliyokithiri nchini inatokana na wachache kuwahadaa wengine kwa manufaa yao binafsi” alisema.
Alisema ili kufanikisha mambo yote na kuishi kwa kuheshimiana, umoja na ushirikiano na kuwasaidia wenye shida ni muhimu.
“Tuwe na umoja, ushirikiano na tuwasaidie wale wenye shida. Tukiyafanikisha hayo tutakuwa na heshima na tutaishi kwa kuheshimiana” alisema.
Alisema mahusiano chanya ni kuleta amani, utii, upendo na kuongeza furaha kwa jamii za watanzania.
“Tuwe na mahusiano yenye kuleta amani na furaha miongoni mwetu. Tuwe na malezi ya kupendana tukimcha Mungu ili huruma yake iwe miongoni mwetu. Tuwapende watoto na kuwa na mpango wa kuwalea ili wawe na furaha” alisema.
Alisema mwaka 2013 uwe na mazingira ya amani, upendo, utii, usafii unyenyekevu, upendo na huruma.
Zaidi ya watoto 1300 walihudhuria kongamano hilo lililohusisha watoto wa Parokia zote za Manispaa yani Parokia za Kihesa, Mshindo, Mkwawa, Ipogolo pamoja na Parokia ya Nyabula.
No comments:
Post a Comment