| Mkurugenzi mtendaji wa TCDA Jackson Kiyeyeu akiwa ofisini kwake wakati wa mahojiano na mtandao huu. |
Kufuatia tatizo sugu la mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari Mkoani Iringa,
Tanganyika Centre Development and Advocacy (TCDA) wameanzisha mkakati wa
kumaliza tatizo hilo
Mkoani humo.
Akizungumza na mtandao huu ofisini kwake leo Mkurugenzi mtendaji wa TCDA Jackson Kiyeyeu alisema kuwa, wameamua
kushughulikia suala la mimba mashuleni kutokana na tatizo hilo
kuendelea kukua kwa kasi licha ya kuwepo kwa sheria ya kuwabana wale ambao
watapatika na hatia kama hiyo.
Amedai kuwa, sababu kubwa inayochangia kuendelea kwa
tatizo la mimba mashuleni ni
kunatokana na vijana wengi kukosa elimu ya afya na uzazi.
“Vijana wengi wanashindwa kufikia malengo kwa sababu
hawana elimu ya afya na uzazi ndiyo maana tatizo la mimba mashuleni linaendelea
kuwa sugu na kuonekana kama ni kitu cha
kawaida. Kwa hiyo tumeona tuanze kupambana na hili kwa kutumia njia mbalimbali
ili tuweze kulimaliza kabisa” amesema Kiyeyeu.
Amesema zipo sababu nyingi zinazochangia suala la mimba
kwa wanafunzi mashuleni ambapo wakianza kuzifanyaia kazi zinaweza kupunguza
tatizo hilo kama
siyo kumaliza kabisa.
Amefafanua njia zitakazotumika,kuwa ni pamoja na
kuishauri familia moja kuthamini motto wa familia nyingine na kuchukulia kama motto wake pamoja na kutoa elimu kwa vijana juu ya
changamoto za ujanani.
“Tutatumia njia
mbalimbali katika pambano hili. Tutatoa elimu ya afya na uzazi kwa vijana, tutaunda
vikundi vya vijana na kuvitumia katika kwa ajili ya kuzungumzia changamoto za
ujana, tutatumia michezo kama njia moja wapo ikiwa ni pamoja na kugawa mipira
katika vikundi hivyo pamoja na kuishirikisha jamii katika suala zima la malezi
ili kila mtu amuone mtoto wa mwenzake kama mtoto wake” amesema.
Alisema jamii ina mwamko mdogo katika kushiriki suala
la malezi huku baadhi ya watu kuendelea kuwarubuni watoto wa wenzao na
kuwakatisha masomo.
“Watu wengine hawaheshimu watoto wa wenzao. Wanafunzi
wengi wanaokatishwa masomo, wahusika ni watu wazima ambao tungetegemea wawe
walezi wazuri na mfano mzuri wa mwenendo wa tabia lakini wamegeuka kuwa ndiyo
watu wa kuogopwa” amesema.
Hata hivyo amesema kumekuwepo na ushirikiano duni kati
ya wazazi na waalimu hali inayosababisha pengo kubwa la utekelezaji kwa vitendo
katika suala zima la maezi na elimu.
“Kumekuwepo na tatizo la kutegeana malezi kati ya
wazazi na waalimu. Mwalimu anabaki akilaumu kuwa wazazi wanawafundisha watoto
tabia mbaya huku mzazi naye akimlaumu mwalimu kuwa hawajibiki ipasavyo”
amesema.
Hata hivyo alisema pamoja na lawama kwa upande wa
walimu na wazazi, baadhi ya waalimu wamekuwa siyo waadilifu na kutumia nafasi
walizo nazo kwa kuwakwamisha wanafunzi wao.
“Baadhi ya waalimu siyo waadilifu has asana walimu wa
kizazi kipya wanatumia nafasi zao kwa kurudisha maendeleo ya wanafunzi. Badala
ya kufundisha kile anachotakiwa kumfundisha mwanafunzi, yeye anaanza mahusiano
mengine kabisa. Tunataka ifike mahali hiyo tabia ikaisha kabisa” amesema.
Sambamba na waalimu hao, amesema wapo baadhi ya
maafisa watendaji wa vijiji, mitaa na wa kata kutumia tatizo la mimba mashuleni
kama njia ya kujipatia fedha.
“Kuna baadhi ya maafisa watendaji wamekuwa ni chanzo
kikubwa cha tatizo hilo
kwa sababu wanafurahia wanafunzi wanapopata ujauzito na kutumia mwanaya huo kwa
kujipatia fedha. Wanaamua kuwaita wahusika na kutaka wawape fedha ili suala
lisiweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ndiyo maana watu wanaendelea
kufanya hivyo wakijua kuwa watakapo patikana wanamalizana kiaina” amesema.
Utafiti uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana katika
Manispaa ya Iringa pekee unaonesha kwa mwaka jana wanafunzi 34 walikatishwa
masomo kwa sababu ya ujauzito.
Shule 9 za sekodari zilizofanyiwa uchunguzi, ziliweza
kubainika kuwa na mimba 30 huku shule ya sekondari ya Mkwawa pekee yake
ikipatikana na mimba 4 na shule za msingi 4 zilizofanyiwa uchunguzi
zilipatikana na mimba 4.
No comments:
Post a Comment