| Mbunge wa viti maalum Chiku Abwao (CHADEMA) akihesabu pesa za kuwapa mkopo wanawake wa kikundi cha Tupendane. |
| Wanawake wa kikundi cha tupendane wakisubiri Mbunge wa viti maalum Chiku Abwao awape pesa za mkopo kwa ajili ya kufanyia shughuli za ujasiriamali. |
| Mbunge wa viti maalum Chiku Abwao (CHADEMA) akimpa mkopo mmoja wa wananakikundi cha wanawake cha Tupendane kilichopo kata ya Mivinjeni katika Manispaa ya Iringa. |
MABILIONI ya Kikwete yamelalamikiwa kuwadharirisha wanawake wa Mkoa wa Iringa kwa kile kilichoelezwa kuwa waliishia kupiga picha na kujaza fomu na baadhi ya viongozi kuishia kuangalia sura zao bila kupa chochote.
Haya yalizungumzwa jana na wanawake wa kikundi cha Tupendane kilichopo Kata ya Mivinjeni katika Manispaa ya Iringa walipokuwa wakipokea mkopo kutoka kwa Mbunge wa viti maalum Chiku Abwao (CHADEMA).
Akizungumza kwa niaba ya wanakikundi wenzake na waandishi wa habari hizi, Habiba Ngollo alisema mabilioni ya Kikwete yaliyotolewa kuwasaidia wajasiriamali mbalimbali yalilenga kuwadharirisha wanawake badala ya kuwasaidia.
“Walikuja hapa wakatuambia kuwa Kikwete amemwaga mapesa kwa ajili ya kutusaidia sisi wajasiriamali lakini ukweli pesa hizo zilitudharirisha kwa sababu walisema tupige picha na tujaze fomu tukafanya hivyo. Wakaja kwenye vikundi vyetu wakawa wanaangalia wenye sura nzuri, watoto wa shangazi zao, wajomba zao na watoto wao ndio wakawapa zile pesa sisi wakaishia kuangalia picha zetu tu” alisema Ngollo na kupigiwa makofi na wanakikundi wenzake.
Huku akionesha kuwa na imani kwa Mbunge huyo, Ngollo alisema viongozi waliowadharirisha waige mfano wa Mbunge huyo kwa kusaidia watu bila ubaguzi na kuwataka wanawake wenzake unapofika wakati wa uchaguzi wasiwape nafasi viongozi waongo na wadharirishaji kwani watawarudishia maendeleo yao nyuma.
Akitoa mkopo kwa wanawake wa kikundi hicho, Abwao alisema wanawake hao wasiwe na maneno ya kusengenyana badala yake washauriane ili waweze kuboresha kikundi chao kiweze kusonga mbele.
“Msiwe na maneno ya kusengenyana, tianeni moyo na kupeana ushauri wa kimaendeleo ili msirudi nyuma. Kikundi hiki kitaboereshwa na ninyi wenyewe mkiwa na dhamira ya kuukataa umasikini” alisema Abwao.
Hata hivyo alisema hakuna mtu aliyezaliwa tajiri na kuwashauri wanawake kuongeza juhudi wakimshirikisha Mungu ili waweze kujenga imani ya kukopesheka.
“Hakuna mtu aliyezaliwa tajiri duniani, ongezeni juhudi mkimshirikisha mwenyezi Mungu ili muweze kujijengea imani ya kukopesheka. Mkianza vizuri na kujijengea uaminifu, tunakoendelea mtakopesheka” alisema.
Alisema zamani wanawake walikuwa wakivaa vitenge na kanga kwa sababu ya kuwa na mapenzi ya dhati lakini imefika kipindi wanawake wanavaa kwa sababu ya umasikini.
“Zamani tulikuwa tunavaa vitenge na kanga kwa sababu ya kuwa na mapenzi ya kweli lakini imefika wakati tunavaa kwa sababu ya umasikini. Kwa nini tuendelee kuvaa mabango barabarani bila kulipwa” alisema.
Jumla ya shilingi 520,000/= zilitolewa kwa wanawake mbalimbali wa kikundi hicho kwa ajili ya kuwasaidia kufanyia kazi za ujasiriamali.
No comments:
Post a Comment