RAIS wa Baraza la Maaskofu Tanzania Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa amewashauri watumishi wa Mungu kuachana na ajira za shetani hapa duniani badala yake watende kazi waliyotumwa na Mungu wa ajili ya wokovu wa wanadamu.
Mhashamu Ngalalekumtwa ambaye pia ni askofu wa jimbo la Iringa alisema hayo katika Ibada ya Misa ya daraja la Ushemasi ilifanyika katika Kanisa la Kiaskofu Parokia ya Kihesa.
Alisema Mungu hataki uchafu na uchoyo na kwamba ajira za shetani zinaangamiza roho za watu na kuvuruga mipango ya haki.
“Acha kuajiriwa na shetani. Aliye na ajira za haki ni Mungu pekee; uchafu na uchoyo ni mambo yaliyokinyume na mafundisho. Achani kuvutwa na shetani kwani mipango yake ni kuangamiza roho za watu na kuvuruga mipango ya haki” alisema.
Amewataka watumishi hao kuwa mfano mzuri wa kuigwa huku wakiendelea kulinda kiapo cha useja.
“Popote pale hakikisheni mnakuwa mfano wa kuigwa na siyo kukimbiwa na watu. Lindeni kiapo chenu cha useja. Watu watawaiga kwa matendo yenu mema. Msiwe na kiburi cha ukaidi wa maagizo ya haki” alisema.
Alisema watumishi hao wanatakiwa kuwatumikia watu kwa uchangamfu na kuwafariji na kutenda yale ambayo Mungu anataka.
“Watumikieni watu kwa uchangamfu, wafarijini waliokufani mkitenda yale ambayo Mungu anataka vinginevyo ni kufanya uasi” alisema.
Alisema fikra za utulivu huleta amani, unyenyekevu na kuumba moyo wa hofu ya Mungu iliyokamilika katika huduma ya upendo.
“Muwe na fikra za utulivu ili kulijenga taifa la Mungu katika amani, upendo na unyenyekevu. Kuweni na upendo kwa kila mtu bila kujali dini, dhebu au rangi. Ninyi ni kiungo kikubwa cha ukweli, unyenyekevu na amani” alisema.
Ibada ya Misa hiyo ilikwenda sambamba na utoaji daraja la ushemasi kwa mseminari Victorino Kalinga wa Parokia ya Kaning’ombe iliyopo ndani ya jimbo hilo.
No comments:
Post a Comment