Watawa wameonywa kutokubali kutawaliwa na matendo maovu na badala yake wafanye kazi kwa kufuata mafundisho ya kumtumikia Mungu na taifa lake.
Haya yamesemwa leo na Mhashamu askofu Castory Mswemwa wa jimbo Katoliki la Tunduru Masasi wakati wa Misa ya nadhiri za watawa wa shirika la masista Wateresina (C.S.T) na shirika na mabruda la Mt. Maria Imakulata (SCIM) iliyofanyika katika Kanisa la Moyo Mt. Yesu Parokia ya Tosamaganga katika Jimbo la Iringa.
Amesema watawa hao wasionekane wapole kwa sasa na baadaye kulegea na kukubali dunia kuwaendesha katika mambo na matendo yasiyompendeza Mungu huku wakifanya mambo kwa kujipendelea.
“Leo hii mnaonekana wapole mnapofunga nadhiri zenu lakini mkishafika huko matakakopelekwa kwa ajili ya kumtumikia Mungu na taifa lake mnaanza kukunjua makucha yenu na kuanza kwenda kinyume na mafundisho” amesema askofu Msemwa.
Askofu Msemwa amesema nyakati hizi ni za kumtumikia Mungu katika haki na kweli ili kuweza kufikia kilele cha utakatifu.
“Toeni maisha yenu kwa kumpenda Mungu na taifa lake kwa kuyatoa maisha yenu kwa ajili ya utumishi mtakatifu usio wa kuigiza. Epukeni kujiingiza katika dunia iliyo na giza mkamsahau Mungu wenu” amesema.
Askofu Msemwa amesema tatizo lililopo sasa ni watu kuwa wabinafsi, wasiowajali wengine wanaohitaji msaada na kujifanyia kila jambo kiubinafsi na kusababisha migogoro katika jamii.
“Tatizo linalokuja sasa ni kwamba watu wamekuwa na ubinafsi kwa kila kitu hata kama kitu ni cha jumuiya wanaamua kujibinafsisha kwa maslahi yao bila kujali wengine. Hapa ndipo migogoro katika jamii zetu inazaliwa kila siku” amesema.
Amesema haki imetoweka kwa kuwa kila mtu anataka kufanya anachotaka bila kuwakumbuka hata watoto yatima huku wengine wakidiriki kunyang’anya kile kinachotolewa kwa ajili ya kuwasaidia wengine na kukitumia wao.
“Haki imetoweka kabisa. Watu wanapenda kujiridhisha wao na kudiriki kunyang’anya kile kinachotolewa kwa ajili ya kuwasaidia wengine na kujimilikisha. Jitoeni katika haki na kutumia wajibu wenu katika utumishi wa haki na amani mkiwajali wengine kwa kuwa na mahusiano mazuri yanayompendeza Mungu” amesema.
Amesema kuna mambo mengi ambayo yanapaswa kutumika na kutumiwa vizuri lakini yamekuwa yakitumika kinyume na kuzua malumbano yasiyoisha kutokana na watu kukosa maadili ya haki na upendo.
Jumla ya masista 22 wamefunga nadhiri za daima huku 7 wakiadhimisha jubilei ya miaka 25 ya utawa, 2 wakiadhimisha jubilei ya miaka 50 na 3 wakiadhimisha jubilei ya miaka 60 wakati mabruda 7 wakifunga nadhiri za daima, 2 wakifunga nadhiri za kwanza, 1 akiadhimisha jubilei ya ya miaka 50 na 1 akiadhimisha jubilei ya miaka 60 ya utawa.
No comments:
Post a Comment