masuguru

Tangazo la cheti

Tangazo la cheti
tangazo

KLERUU

KLERUU
KLERUU

CAPRICORN

CAPRICORN

Ibada

Ibada

Monday, October 22, 2012

Watanzania tuishi kwa upendo na amani

                                                                                          Mtazamo mpya

KUNA msemao usemao: “Muuliza njia si mjinga.” Kama tatizo ni lugha si fedheha wala dhambi kuuliza mwingine anayejua maana yake.

Wahenga pia walisema: “Kidole kimoja hakivunji chawa.” Pia “Mikono miwili hunawishana.” Hayo yote kwa pamoja tunaweza kusema: “Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.”

Lakini kutokana na migogoro ya hapa na pale inayotokea hapa nchini, tatizo kubwa ni ubinafsi ambao huleta mvurugano na uhasama ndani ya jamii.

Tatizo kubwa linalosababisha matukio kama haya duniani kote, ni baadhi ya watu kutaka ubinafsi na kutumia mamlaka waliyonayo wakiamini kuwa wao ndio kila kitu, bila kuangalia mitazamo na mawazo ya wengine.

Kwa mtazamo wangu, sina maana ya maneno ‘Uhuru na Amani’ kama yanavyotumika katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wimbo wa taifa na kwenye hotuba mbalimbali za viongozi, kwa sababu huo uhuru na hiyo amani havipo nchini.

Kwa sasa wananchi wamekuwa wakiishi kwa woga, kwa sababu wanaogopa kuchukuliwa hatua kabla ya kubainika kama wamefanya kosa au la.

Hakika tukiendelea hivi, nchi itajikuta inaishia pabaya, ikiwamo vita ya wenyewe kwa wenyewe, kisha tutabaki kujutia.

Mifano halisi tunaiona kutoka nchi jirani, hivyo ni vema tukafanya kazi kwa kuelewa mambo kuliko kuhisi na kuanza kuwachukulia watu hatua bila sababu. Hali hiyo inawafanya wananchi waishi kama digidigi.

Digidigi ni mnyama ambaye maisha yake ni ya wasiwasi wakati wote, kwani huhofia kuliwa na wanyama wakubwa muda wowote pindi atapojisahau.

Kwa hiyo, huishi kwa kujificha kila wakati ili asionekane na wabaya wake. Bahati mbaya hali kama hiyo ya digidigi huweza kutokea kwa mtu yeyote yule na wakati wowote na sekunde yoyote bila kutegemea, kutokana na mazingira tunayoishi hapa nchini.

Lakini kwa matukio ya Morogoro na Nyololo mkoani Iringa, hayana cha bahati mbaya.
Na hii yote inatokana na baadhi ya viongozi wa serikali kutokujua na kuelewa maana ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwamba ina lengo gani.

M4C ina lengo la kuleta mabadiliko katika jamii, katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo na si migogoro.

Lakini kuna baadhi ya viongozi wameshindwa kujua maana yake na kupotosha umma. Hapa tatizo lililopo ni uelewa kwa viongozi hao.

Nasema hivyo kwasababu mkoani Iringa mwandishi wa habari Daudi Mwangosi aliuawa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu.

Kwa mtazamo wangu, sioni kama kuna haja ya askari kubeba bunduki na mabomu katika mikutano ambayo wananchi hawana silaha yoyote wala vumbi mikononi mwao.

Labda wangetueleza hapa nchini vita iko wapi inayowashawishi watembee na silaha kwa kujihami.

Watueleze dhumuni lao la kutembea na silaha katika nchi hii ambayo inaitwa kisiwa cha amani. Labda niulize swali, waandishi wa habari si raia wa kawaida?

Waswahili walisema: “Usipoziba ufa, utajenga ukuta.” Nisingependa kufikia wakati wa kupeleka mawazo yangu kuwafikiria wakimbizi kwani nilijua mtu kuitwa mkimbizi ni kitu kigumu.

Kutokana na hilo, hapa ndipo nafikiria maisha ya digidigi na wakimbizi. Nimezoea kusikia wakimbizi ni raia wa nchi nyingine wanaoingia nchi nyingine kutafuta hifadhi lakini kumbe sikuwa sahihi.

Nimejua kuwa mkimbizi anaweza kuwa mtu yeyote hata ndani ya nchi yake, kwa sababu ataishi kwa kuogopa muda wote kutokana na kutokuwa na imani na nchi yake.
 

No comments:

Post a Comment