MTUHUMIWA wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha Channel Ten Daud Mwangosi aliyetakiwa kufikishwa mahakamani leo hakufikishwa kutokana na sababu zilizoelezwa kuwa anaumwa.
Mwendesha mashataka wa serikali Michael Luwena katika maelezo yake aliyoyasoma mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Dyness Lyimo alisema mtuhumiwa huyo hakuweza kufikishwa mahakamani hapo kwa taarifa kuwa anaumwa.
Pasificus Cleophace Simon (23) alitakiwa kufikishwa kwa mara ya tatu leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kutokana na tuhuma inayomkabili ya kumuua kwa makusudi mwandishi huo katika ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA katika kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa uliofanyika Septemba 2 mwaka huu.
Tofauti na wakati uliopita mahakamani hapo kuwepo na ulinzi mkali, leo hakukuwa na ulinzi mkali kuwadhibiti waandishi kupiga picha.
Mtuhumiwa huyo mwenye namba G 2573 wakati akifikishwa kwa mara ya kwanza alifikishwa katika ulinzi mkali kupitia gari lenye namba za usajili T 320 ARC linalosadikiwa kuwa ni la RCO huku kwa mara ya pili akifikishwa kwa miguu na kuondolewa mahakamani hapo kwa gari namba DFP 2175 pic up akiwa katika ulinzi mkali huku waandishi wa habari wakidhibitiwa na polisi na mmoja wao kunusurika kupigwa jambo lililozusha hisia tofauti miongoni mwa wananchi wengi mkoani hapa.
Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka, upelelezi haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Oktoba 24 mwaka huu itakapotajwa tena.
Mwangosi aliuawa kwa bomu Septemba 2 mwaka huu katika kijiji cha Nyololo alipokuwa akiwajibika kwa kazi za kihabari wakati wa ufunguziwa wa matawi hayo.
No comments:
Post a Comment