Mbunge wa jimbo la Iringa mjini Mch. Peter Msigwa (CHADEMA) anatafutwa na jeshi la polisi ili kutolea maelezo juu ya tuhuma mbalimbali zinazomkabili dhidi ya jeshi hilo.
Mtandao huu umebaini hayo leo mkoani hapa likielezwa kuwa Msigwa anatuhumiwa kwa uchochezi na kutumia muda zaidi katika mkutano uliofanyika katika viwanja vya Mwembetogwa.
Imeelezwa kuwa katika mkutano uliofanyika 19 Septemba mwaka huu maeneo ya Soko Kuu la Manispaa ya Iringa Msigwa alitoa maneno ya uchochezi na kuhamasisha wananchi wasijihusishe na wiki ya nenda kwa usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuwataka wananchi wawazomee viongozi wa ngazi ya juu watakao fika katika maadhimisho ya wiki hiyo hadi kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda atakapoondoka Iringa..
Tuhuma nyingine imeelezwa kuwa katika mkutano uliofanyika katika viwanja vya Mwembetogwa na kumhusisha Ally Bananga pamoja na Joshua Nasari maarufu kwa jina la dogo janja, Msigwa alipitiliza muda unaotakiwa kutumika katika mikutano.
Kwa mujibu wa chanzo chetu RCO Wankyo Mwita amekwisha kufanya mawasiliano na Msigwa ili afike kutoa maelezo lakini hajafika jambo ambalo linawalazimu kumtafuta popote alipo.
“Mbunge wenu Msigwa anatafutwa na jeshi la Polisi kwa ajili ya kujibu tuhuma zinazomkabili. RCO amekwisha kufanya mawasiliano naye lakini hadi sasa hajafika jambo ambalo tumeambiwa tumkamate popote alipo” kilisema chanzo hicho.
Mch. Msigwa alipotafutwa ili kuthibitisha juu ya jambo hili alikiri kuwa alipigiwa simu na RCO kuwa anatakiwa kuripoti kituoni kwa ajili ya kutolea maelezo hayo lakini kwa wakati huo alikuwa kwenye matibu ya mguu unaomsumbua.
“Ni kweli mwandishi nimepigiwa simu na RCO kuwa ninatakiwa kufaika kituoni kutoa maelezo kutokana na kauli zangu za uchochezi na kufanya mkutano hadi kupitiliza kuda lakini mimi nipo kwenye matibabu ya mguu
wangu unaonisumbua” alisema Msigwa.
19 Septemba mwaka huu Msigwa alitoa tamko kuwa Kamuhanda lazima aondoke Iringa kwa kuwa ameshindwa kuwalinda wananchi na mali zao na badala yake anasababisha mauaji ya watu wasio na hatia.
“Kamuhanda lazima aondoke, Iringa hatukuzoea mauaji ya namna hii, hatuwezi kuishi na nyoka ngani ya nyumba. Kamuhanda ni nyoka lazima aondoke hatumhitaji” alisema.
No comments:
Post a Comment