| Kamanda wa operesheni na mafunzo Benson Kigaila kushoto akizungumza na waandishi wa habari na kulia mwenye kofia ni Mwenyekiti wa Baraza la vijana (BAVICHA). |
| Naibu katibu Mkuu wa CHADEMA Hamad Yusuph |
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, kimeahirisha kwa muda operesheni yake ya mikoa mitano kwa ajili ya kujadili na kuchukua hatua dhidi ya serikali kutokana na mauaji yanayoendelea katika mikutano yake.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa leo kamanda wa opersheni hiyo iliyokuwa ihusishe mikoa mitano Benson Kigaila amesema baada ya kamati kuu ya Chama hicho itakutana jijini Dar es Salaam, jumapili hii na kitatoa tamko juu ya nini kifanyike.
Kigaila ameema katika mkutano huo wa dharura ya kamati kuu watawasilisha taarifa nzima juu ya matukio mbali mbali yaliyotokea kuanzia siku ya kwanza ya operesheni na kisha yatatolewa uamuzi.
“Tunahitaji kukaa na kutafakari juu ya matukio haya kwa kuwa si jambo la kawaida kuruhusu watu kufa kila wakati nasi tukaendelea na mikutano yetu bila kuchukua hatua stahiki”alisema Kigaila.
Amesema wakati wote kuanzia kutokea kwa Msiba wa Daudi Mwangosi kuna propaganda nyingi zilizojitokeza juu ya hali hiyo huku watu wakiaminishwa kuwa hali hiyo inasababaishwa na Chadema.
“Kuna wanaofanya propaganda juu ya hili na baada ya sisi kumaliza mambo yote ikiwa ni pamoja na kuhakikisha waliokamatwa wameachiwa tumeona tuwambie ukweli juu ya kile kilichotokea” alisema.
Kigaila ameongeza kuwa Watanzania wanapaswa kutambua kwamba kuna kitu cha ziada ambacho serikali ya chama cha Mapinduzi na jeshi la polisi wanakifanya dhidi ya Chadema na siyo zoezi la sensa ambalo ni sababu waliyoitumia kusitisha mikutano ya Chadema.
“Siku ambayo Chadema tunafungua matawi na kufanya kikao cha ndani na polisi wakituzuia tusifanye CCM nchi nzima walikuwa wanafanya mikutano yao ya uchaguzi ndani ya Wilaya huku wakibebana kwa malori na kukusanyana kwenye Wilaya lakini hawakuzuiwa kwamba wanaingilia zoezi la sensa lakini mikutano ya Chadema tena ya ndani ikaonekana inaingilia zoezi la sensa” alisema Kigaila.
Amesema tukio la kifo cha Mwangosi lilitokea wakati Chadema wakifungua matawi na si katika mkutano wa hadhara kama propaganda za jeshi la polisi na Chama cha Mapinduzi CCM zinavyodai.
Hata hivyo Kigaila alitilia shaka askari polisi waliotumika katika tukio hilo kuwa hawakuwa na mafunzo bali walikuwa ni mamluki ambao waliaandaliwa maalum kwa ajili ya kutekeleza zoezi lililopangwa na kusabaisha kifo cha mwandishi huyo.
“Kitu ambacho mimi nilikiona kwamba inawezekana RPC alivalisha magwanda ya jeshi mabaunsa wa CCM na kuwatumia kama askari polisi na ndiyo maana kwa namna yoyote ile hawawezi kutii amri ya mkubwa wao; askari wamefundishwa utii, mkubwa akisema ni amri lazima wanatekeleza wala hawahoji. Askari aliokuwa nao RCO kwenye tawi la kwanza walikuwa wakihoji na kulaumu kitendo cha RCO kuwazuia wasipige” alisema.
Imekuwa ni kawaida kwa serikali ya chama cha Mapinduzi kuvalisha raia nguo za jeshi wakafanya kazi za jeshi wakapewa vitambulisho vya usalama wa taifa na pia kuvua askari magwanda na kuwavalisha nguo za chama wakafanya kazi za chama katika uchaguzi mbalimbali.
“Tuliona kule Kiteto baunsa wa CCM tunamjua alitoka Manzese akapewa SMG ya polisi na kuteka viongozi wetu ambapo mpaka sasa kesi ipo polisi haijawahi kutolewa maamuzi. Tunajua ni kwa sababu askari aliokuwa nao RPC wengi alikuwa amewavalisha mavazi ya magwanda wakiwa ni wafuasi wa CCM na ndiyo maana wakamuua Mwangosi” alisema.
Amesema kabla ya kifo cha Mwangosi, marehemu alieleza kutilia shaka askari waliokuwapo katika kikosi hicho kuwa si wale wanaofanya kazi za jeshi bali ni mamluki wasio na mafunzo.
“Marehemu aliniambia kuwa hapa nina shaka na hawa Polisi kwa kuwa wengi ninawafahamu lakini ninaowaona hapa si wale ninaowafahamu” alisema Kigaila.
Naye mwenyekiti wa baraza la vijana Chadema taifa (BAVICHA) Deo Munishi amesema CCM kwa kutumia jeshi la polisi imedhamiria kuiangamiza Chadema isiendelee kushika kasi ya kuiangusha CCM madarakani.
“Serikali imedhamiria kuiangamiza na kutokomeza Chadema nchini na miongoni mwa vyombo vinavyotumika kukiangamiza Chadema ni jeshi la Polisi na sasa ameingia msajili wa vyama vya siasa John Tendwa kutaka kukifuta ambapo kauli yake ni mwendelezo wa kauli zinazotolewa na serikali pamoja na CCM kuwa Chadema ni chama cha vurugu. Ninachoweza kumwambia kuwa kama anataka kufanya hivyo aanze kukifuta Chama cha Mapinduzi CCM kwa kuwa tumeshabaini kuwa si chama cha siasa tena bali ni chama cha magaidi” alisema Munishi.
Akitolea mfano wa matukio mbalimbali yanayofanywa na chama cha mapinduzi bila kuchukuliwa hatua alisema ni pamoja na mauaji ya Igunga, vurugu za Kiteto, Singida na Biharamulo ambapo hadi sasa jeshi la polisi pamoja na John Tendwa wamekaa kimya.
Aidha Chadema wameahidi kujitokeza kutoa ushahidi wa tukio zima la mauaji mbele ya tume huru na wala si tume iliyoundwa na jeshi la polisi wala tume iliyoundwa na waziri wa mambo ya ndani Emanuel Nchimbi.
Sambamba na Chadema kuwa tayari kutoa ushahi, wamelitaka jeshi la polisi kueleza vifaa vya marehemu Mwangosi vipo wapi ikiwemo camera na kompyuta aina ya Laptop.
No comments:
Post a Comment