| Wanafunzi wa shule ya Msingi Kidabaga wakiwa nje ya ofisi za kijiji kusubiri maelekezo nini hatima ya madai yao. |
| Mwenye sweta la kijani ni miongoni mwa wanafunzi 9 wanaofundishwa |
Wanafunzi wa darasa la saba katika shule ya Msingi Kidabaga Wilaya ya Kilolo katika Mkoa wa Iringa wameandamana katika ofisi ya kijiji kupinga kitendo cha kubaguliwa na waalimu katika kufundishwa huku wanafunzi 9 wakiendelea kufundiswa.
Mtandao huu umeshuhudia wanafunzi hao wakiwa katika ofisi ya kijiji wakisubiri kupewa maelekezo ya kutoka ofisi ya kijiji nini kifanyike ili waweze kupata haki yao ya kufundishwa.
Akizungumza na mwandishi wa habarihizi kwa niaba ya wanafunzi wenzake Luth Myinga amesema hawajui sababu ya waalimu kuwabagua wakati wa vipindi.
“Kweli kaka sisi hatujui ni kwa nini tumebauliwa na waalimu kuendelea kufundisha wanafunzi 9 wakati darasani tupo wanafunzi 84. Hatujui sababu ni nini ndiyo maana tumekuja hapa ofisini ili wazazi wetu waweze kutusaidia na sisi tupate haki yetu ya kufundishwa” alisema mwanafunzi huyo.
Akitoa ufafanuzi zaidi mwanafunzi huyo amesema tabia hiyo inafanywa zaidi na mwalimu mmoja ambaye pia ni mwalimu wa taaluma katika shule hiyo na kwamba wanapojaribu kuhoji mwalimu huyo hufunga mlango na kuendelea kuwafundisha wanafunzi hao wachache.
“Tabia hii inafanyika zaidi na mwalimu mmoja ambaye ni mwalimu wa taaluma na tunapotaka kuhoji ni kwa nini anatubagua, hufunga mlango na kuendelea kuwafundisha wenzetu” alisema mwanafunzi huyo.
Mwandishi wa habari baada ya kufika ofisini na kumkosa mwalimu Filomena Myenzi ambaye ni mwalimu wa taaluma katika shule hiyo, alikwenda hadi nyumbani kwake ambapo alitakiwa kutoa ufafanuzi alisema hawezi kueleza chochote kwa kuwa siyo muda wa kazi na yupo nje ya ofisi lakini hata kama kuna tuhuma dhidi yake mwalimu Mkuu atajibia.
“Kwanza huu siyo muda wa kazi, pili nipo nje ya ofisi na tatu mimi siyo msemaji na hata kama kuna tuhuma juu yangu mtafute mwalimu Mkuu ili ajibie kwa sababu mimi daima natekeleza sheria” alisema.
Alipotakiwa kufafanua ni sheria zipi anazitekeleza, alisema “nimeshakwambia umtafute mwalimu Mkuu ndiye atakayekujibu maswali yako yote mimi siyo msemaji” alisema.
Miongoni mwa wanafunzi 9 wanaodaiwa kufundishwa alipokutana na mwandishi na kuulizwa juu ya utaratibu wao kufundishwa wachache alisema hawezi kusema chochote kwa kuwa walikataliwa na mwalimu wa taaluma kuongea kwa watu juu ya hilo .
Daniel Kumbulu ni Mwenyekiti wa Kamati ya shule katika shule hiyo ambapo alisema kuwa mwalimu Mkuu ndiye mwenye majibu kuhusu hilo kwa kuwa utaratibu anaujua.
“Mwalimu Mkuu ndiye mwenye majibu, sijui niseme nini kwa sababu juu ya kuandamana kwa wanafunzi bado sijajua ila kama ni kuhusu michango au sababu gani kwa sasa sitaweza kujibu kwa kwa kuwa sijajua waliandamana kwa sababu zipi. Nashukuru kwa kunijulisha mimi nilikuwa safarini ndiyo naingia kwa hiyo bado sijapata taarifa yoyote ila nitalifuatilia kwa ukaribu zaidi” alisema Kumbulu.
Mmoja wa wazazi wa wanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo licha ya kuomba jina lake lisiandikwe azetini kwa kuwa yeye si msemaji wa wazazi amesema kuwa utaratibu wa walimu shuleni hapo haujulikani kwa kuwa waliomba wazazi wachangie shilingi 40 elfu ili watoto wao waweze kufundishwa vipindi vya ziada lakini cha kushangaza wanafunzi wanatengwa katika vipindi licha ya kuwa pesa walizoambiwa wachange wamechanga.
“Ndugu mwandishi hiki kijiji kina matatizo na matatizo haya yanazidi kutumaliza. Mwalituambia tuchangie shilingi 40 ili watoto wetu wa darasa la saba waweze kufundishwa hata vipindi vya ziada lakini sha kushangaza pesa tumetoa lakini watoto wetu wanabauliwa, hatujui mpango wao ni nini!” alisema mzazi huyo.
“Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Peter Tengelakwi alipotafutwa na mwandishi kwa njia ya simu alisema yupo katika kikao kwa hiyo hana muda wa kuonea na simu.
“Sina muda wa kuongea na simu kwa sababu nipo kwenye kikao” amesema Tengelakwi.
Naye mratibu wa elimu kata ya Dabaga Monica Mgenzi alipoulizwa juu ya suala hili alisema hajui lolote na kusema kuwa atalifanyia kazi na wakati huo huo akaamua kuwafuata wanafunzi waliokuwa katika ofisi za kijiji ili aweze kuongea nao.
“Mwanangu kwa kweli sijui lolote ndiyo wewe unanitonya sasa lakini kwa kuwa wanafunzi wenyewe wapo katika ofisi za kijiji nakwenda sasa hivi ili nikutane nao nijue tatizo. Hivi ninavyoonea mwanangu naomba niwajibike kukutana na watoto hao kabla hawajaondoka” alisema na kunyanyuka kitini.
No comments:
Post a Comment