JULAI 18, mwaka huu Mahakama Kuu Kanda ya Iringa itatoa hukumu dhidi ya kesi ya kutoa rushwa katika mchakato wa kura za maoni CCM, inayomkabili kada wa chama hicho, Frederick Mwakalebela na mkewe Selina Julai 18.
Hukumu hiyo itatolewa baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (Takukuru) Mei mwaka jana kugonga mwamba baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa kutupilia mbali shauri hilo namba (2).
Mwakalebela alikuwa mshindi wa kwanza katika kura za maoni zilizoendeshwa na chama cha Mapinduzi katika Manispaa ya Iringa, mwezi Agosti mwaka 2010.
Katika kesi hiyo, Mwakalebela na mkewe Selina, kwa pamoja walikuwa wakituhumiwa kutoa hongo ya shilingi 100,000 kinyume cha sheria namba 15 (1) , (b) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ambayo inasomwa kwa pamoja na kifungu cha 21 (1) , ( a) na 24 (8) ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010.
AGOSTI 1, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Iringa itatoa hukumu ya kesi ya kutoa rushwa iliyokuwa ikimkabili Joseph Mungai aliyepata kuwa Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini kwa miaka 35.
Akiwa ameunganishwa na makada wengine wawili wa CCM, Fidel Cholela na Moses Masasi, Mungai alishitakiwa mahakamani hapo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) akihusihwa na mashtaka 15 ya kutoa rushwa kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007 na sheria ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010 kwa wapiga kura wa jimbo hilo.
Katika hati ya mashitaka hayo, ilidaiwa na Takukuru kwamba Julai 08, mwaka 2010, katika kata ya Ihalimba, Wilaya ya Mufindi, Mungai akiwa mmoja wa makada wa CCM waliokuwa wanawania kupitishwa katika kura za maoni kugombea ubunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, kwa pamoja na watuhumiwa wenzake, walitoa hongo ya kati ya Sh 5,000 na Sh.20,000 kwa wajumbe wa CCM tawi la Vikula kama kishawishi cha kumpigia kura wakati wa zoezi la upigaji wa kura za maoni.
Chanzo: bongo leaks

No comments:
Post a Comment