masuguru

Tangazo la cheti

Tangazo la cheti
tangazo

KLERUU

KLERUU
KLERUU

CAPRICORN

CAPRICORN

Ibada

Ibada

Saturday, July 7, 2012

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo atumia mabavu kudai mchango wa Mwenge > Achoma mafuta kufuata 70 elfu > Aamrisha askari kumkamata mwenyekiti kwa kushindwa kuchangia mwenge > Mwenyekiti akataliwa kujitetea

Mwenyekiti wa kijiji cha Udekwa Obadia Ubugo akitoa maelezo juu ya kilichompata


Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Gerad Guninita ameamurisha askari kumuweka chini ya ulinzi mwenyekiti wa kijiji cha Udekwa kutokana na kijiji kushindwa kutoa mchango wa Mwenge.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mwenyekiti wa kijiji cha Udekwa Obadia Ubugo amesema mkuu huyo wa Wilaya alitumia nguvu kijijini hapo wakati akiwa katika ziara.

“Ndugu mwandishi kwanza nikushukuru kwa kututembelea hata sisi tunaoishi vijijini, wananchi wa vijiji tumekuwa kama chambo kwa baadhi ya watu kujipatia mali hasa viongozi wanaotumia vyeo vyao wamakusudi kwa kudhani kuwa vijijini hatujui haki” alisema Ubugo.

Akifafanua zaidi alisema hawakuweza kutoa mchango huo kwa muda uliokuwa umeelekezwa katika barua baada ya kuona kuna upungufu wa vitendea kazi katika shule ya msingi kijijini hapo na kuamua pesa kidogo iliyokuwepo ielekezwe katika shule hiyo ili watoto waendelee kupata masomo.

“Kweli taarifa za uchangiaji mwenge zilifika lakini kijiji hakina hela na katika shule yetu ya msingi waalimu wakatuambia kuwa kuna upunufu wa vitendea kazi kama vile chaki na mengineyo tukakubaliana pesa kidogo zilizopo zielekezwe katika kununua vitendea kazi ili watoto wetu waedelee na masomo” alisema.

Katika ziara ya Mkuu wa Wilaya hiyo aliyoifanya Juni 29,2012 Mkuu wa Wilaya hiyo aliamuru askari aliyekuwa ameongozana naye kumuweka chini ya ulinzi na kesho yake kufikisha ofisini kwake na kumtaka achaue kutoa 70 elfu ili aachiwe au awekwe chini ya ulinzi.

“Alipofika hapa kijijini alianza moja kwa moja kwa kumwamurisha askari aliyekuwa ameongozana naye kuniweka chini ya ulinzi na kesho yake nifikishwe ofisini kwake au nichague kulipa 70 elfu ili niachiwe huru lakini kwa kuwa sikujua watanipeleka wapi baada ya kuwekwa chini ya ulinzi hadi kesho hiyo nikachukua pesa ya familia nikampa kwa kuwa kijiji hakina pesa ili niyaokoe maisha yangu” alisema.

Amesema alipotaka kutoa maelezo kwa ni kwa nini hawakuweza kutoa mchango huo mkuu huyo wa Wilaya hakutaka kusikiliza chochote huku akisisitiza kuwa anachotaka ni pesa siyo maelezo.

“Mbele ya wananchi alipoagiza askari aniweke chini ya ulinzi, nilitaka kutoa maelezo lakini kasema sitaki unyanyue mdomo wako na ukitaka kuongea toa pesa hizo; ninachotaka mimi ni pesa za mwenge siyo sauti yako” alisema Ubugo.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Udekwa Baraka Kasenegala alipotafutwa ili kuthibitisha kama alipokea pesa yoyote kutoka kwa mwenyekiti wa kijiji hicho alisema ni kweli.

Asante kwa kunitafuta. Nikweli nilipokea kiasi cha shilingi 274,000 kwa ajili ya kununulia chaki ambazo hizo hizo nilitumia nauli kwenda kununua chaki pamoja na mahitaji mengine ya shule vinginevyo zisingekuwa busara za mwenyekiti huyo na wajumbe wake masomo yangesimama” alisema Kasenegala.

Kasenegala alipoulizwa juu ya kilichomtokea mwenyekiti wa kijiji kwa Mkuu wa Wilaya alisema ni wazi ikiwa kila mtu ana uhuru wa kuongea hakutendewa haki.

“Nilikuwepo siku hiyo lakini yalitumika mabavu badala ya mjadala mezani hata niliposimama kutolea maelezo juu ya pesa nilizopokea kutoka kwa mwenyekiti Mkuu wa Wilaya hakunisikiliza na alikazia tu pesa zitolewe na hali ambayo tuliona ni uonezi mwenge wenyewe ulikuwa umeshapita. Picha inayokuja hapa kijijini ni kwamba Mkuu wa Wilaya hakuja kuongea na wananchi bali alifuata shilingi elfu 70 kwa mwenyekiti ambayo hata risiti haikuotolewa” alisema Kasenegala.

Mkuu wa Wilaya hiyo alipotafutwa kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo kwa mara ya kwanza alisema yupo kwenye kikao kwa hiyo hawezi kueleza chochote na kumtaka mwandishi asubri atapotoka kikaoni atampigia simu ili kutoa maelezo.

“Kwa sasa hatutaweza kuelewana kwa sababu nipo kwenye kikao, subiri nikitoka nitakupigia ili tuzungumze zaidi katika hali ya utulivu” alisema Guninita.

Baada ya ukimya kuendelea alipotafutwa kwa mara nyingine alisema hajui ufafanuzi gani kwa sababu mwenge ilishapita.

“Mbona unaturudisha nyuma ambako tulishasahau, sina ufafanuzi juu ya mwenge kwa kuwa ulishapita na tathmini tulishaifanya. Sina maelezo juu ya hilo. Samahani” alisema.

Tangu nchi ipate Uhuru mwaka 1961 Mwenge wa Uhuru haujawahi kufika katika kata ya Udekwa wala vitongoji vyake huku wananchi wakibaki kuuliza Mwenge ukoje licha ya kuwa wananchi hao kutoa michango ya Mwenge kila mwaka.

No comments:

Post a Comment