![]() |
Mkataba Mpya wa Kudhibiti silaha ni lazima uwepo |
Mkutano unaojadili rasimu ya mkataba mpya wa kudhibiti silaha unamalizika leo ( 27.07.2012) New York, huku mataifa makubwa yakishindwa kufikia maamuzi juu ya mambo muhimu kuhusiana na biashara hiyo ya mabilioni ya dola.
Wakiwa mjini New York, kwa mwezi mmoja sasa washiriki wa mkutano huo wanaonekana kusitasita juu ya orodha ya silaha hizo zitakazojumuishwa katika mkataba huo, unaolenga kuepusha umiliki ovyo wa silaha za kivita, ambazo aghalabu hupoteza maisha ya watu wengi katika nchi zenye mapigano.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon ameeleza masikitiko yake kutokana na maendeleo hafifu ya mkutano huo, unaotegemewa kusiha saa chache zijazo.
Watengenezaji wakubwa wa silaha hizo yaani nchi Ulaya, Marekani, Urusi na China na mataifa yanayoonekana kupinga uundwaji wa mkataba huo mpya kama vile Syria, Korea Kaskazini, Iran, Cuba, Misri na Algeria yanashiriki katika mkutano huo.
Wengi wanaupinga mkataba huu...Kwa nini lakini?
Mwezi Oktoba mwaka 2006, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura na kuamua kuwepo na mkataba utakaosimamia biashara hii ya shilaha inayokua kwa kasi, ambayo sasa ina thamani ya takriban dola bilioni 60, ambapo Marekani ilipiga kura ya" Hapana".
Serikali ya Obama ilibatilisha msimamo wa utawala wa Rais aliyemtangulia, George W. Bush, na kuliunga mkono azimio la baraza hilo la kufanya mikutano minne ya maandalizi pamoja na mkutano wa Umoja wa Mataifa kwa muda wa wiki nne mwaka huu, mahsusi kwa ajili ya kuandika rasimu ya mkataba wa biashara ya silaha.
Hatahivyo, Ban bado ana matumaini kuwa mkataba huo utapitishwa kisheria na kukidhi haja iliyopo.
Wapatanishi wamekuwa wakijaribu kuja na rasimu itakayokidhi wanasheria wa mkataba huo mzito ambao una kanuni ngumu.
Nakala za rasimu hiyo zilizosambazwa Jumanne inasema malengo ya mkataba huo ni kuweka viwango vya kusimamia biashara hiyo ya kimataifa katika silaha haramu na kuepusha na kupunguza biashara hiyo yenye athari mbaya kwa umma.
Aidha, wananaopigania mkataba huo nyeti wanasema orodha ya silaha hizo haramu ni finyu sana na inahitaji kuongezwa. Wanataka pia mkataba huo useme waziwazi kuwa silaha hizo haramu si tu za kupeleka nje ya nchi husika, bali aina zote za usafirishaji wa silaha.
Rasimu ya pili ya Argentina ni bora zaidi
Kwa mujibu wa Shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Amnesty International, rasimu ya pili iliyowasilishwa na Mwanadiplomasia kutoka Argentina, Roberto Moritan, ambaye ndiye aliyeongoza majadiliano hayo, ina maboresho mazuri.
Ikiwa washiriki hao watafikia muafaka, Moritan ataiwasilisha rasimu hiyo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na hatimaye zitahitajika nchi 65 kuutia saini ili kuupa uwezo wa kuanza kutumika.
Source: DW swahili

No comments:
Post a Comment