| Hili ni Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa |
Mgogoro unaoendelea ndani ya kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) dayosisi ya Iringa dhidi ya kikundi cha waamini wanaoupinga utawala wa askofu wa kanisa hilo Dkt Owdenberg Mdegella limechukua sura mpya baada ya watu kufunga milango ya kanisa hilo kwa minyororo na makufuli mapya ili kuzuia ibada ya jumapili ya jana.
Akizungumza na Tanzania Daima mlinzi wa kanisa hilo Anderson Mgoba alisema kundi la watu lilifika katika lango kuu la kuingilia katika kanisa hilo jana majira ya saa 11.00 alfajiri na kufunga milango ya kanisa hilo ili kuzuia ibada na huduma zingine zisiendelee hadi hapo atakapojiondoa madaraka kiongozi huyo.
Alisema baada ya kufika katika lango hilo, yeye pamoja na walinzi wenzake hawakuwa na shaka nao kwasababu ndani ya uzio wa kanisa hilo wanaendesha biashara ya kupaki magari hivyo walijua ni madereva wa magari hayo .
“Walipofika tulidhani ni madereva wa magari yaliyokuwemo ndani ya uzio wa kanisa hili, hata hivyo katika mazingira ya kushangaza walitoa minyororo na kuanza kufunga lango hilo kuu la kuingilia kwa ndani” alisema.
Mlinzi huyo alisema kuwa watu hao walitumia mnyororo na kufuli mbili kufunga lango hilo na kutoweka katika eneo.
Mchungaji wa Usharika huo, Huruma Bimbiga alisema hawajui sababu za watu hao hao kufunga milango ya kanisa hilo.
Akitakiwa kutoa ufafanuzi juu ya madai hayo, Dk Mdegella alisema hawezi kuzungumzia suala lililotokea katika usharika mmoja huku yeye akiwa ni kiongozi wa makanisa yote ya Dayosisi hiyo.
“Kwanza mimi niko safarini naelekea Dodoma, na kwa kuwa mimi ni kiongozi wa makanisa ya dayosisi nzima, siwezi kuzungumzia suala hilo, wafuateni viongozi wa kanisa watawaeleza,”
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa Peter Kakamba amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtu mmoja anahojiwa na jeshi hilo na ambapo amesema ataendelea kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari juu ya tukio hilo.
No comments:
Post a Comment