Wananchi wa Mtaa wa Lukosi kata ya Mkwawa katika Manispaa ya Iringa wameulalamikia uongozi wa mtaa huo kushindwa kuwasilisha ripoti ya mtaa iliyo kamili katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana mtaani hapo.
Akiwasilia ripoti katika mkutano huyo afisa mtendaji wa mtaa Neema Kizwi alishindwa kuweka baya mapato na matumizi pamoja na kuchanganua michango mbalimbali inayochangishwa mtaani humo huku akishikwa na kigugumizi alipokuwa akiulizwa maswali.
Imeelezwa kuwa wananchi hao hawajui lolote kuhusu mapato na matumizi sanjari na taarifa za michango wanayochangishwa na viongozi wao licha ya kuwa hujitoa katika maendeleo na kuwajibika wanapotakiwa.
“Litakuwa ni jambo la kushangaza kama sisi wananchi tutadanganywa kweupe namna hii. Mtendaji, hakuna atakayedanganyika hapa. Tunachoomba, tusomee taarifa sahihi kwa kuwa sisi kama wawajibikaji, watekelezaji na wadau wa maendeleo katika nchii hii, tunajua kila kitu. Hakuna mtoto hapa sisi sote ni watu wazima. Taarifa zako ni za uongo” alisema Msafiri Mgilangwa.
Akiorodhesha baadhi ya taarifa zinazodaiwa kupotoshwa mbele ya mkutano huo Mgilangwa alisema kuwa wanataka kujua juu ya taarifa ya mapato ya michango ya serikali, mapato yatokanayo na asilimia 5 ya mauziano, luzuku za mitaa zitokazo serikalini, michango itolewayo kwa ajili ya watoto waishio kwenye mazingira magumu pamoja na mapato ya michango ya wadau ambao huwa wanatoa fedha kwa ajili ya maendeleo ya mitaa wakiwamo wananchi wenyewe.
“Mtendaji, nadiriki kusema huo ni uongo kwa sababu taarifa ulizozisoma hazijulikani kuwa zimetoka wapi! Nikupe mfano wa taarifa tunazotaka kuzisikia hapa: tunataka kujua juu ya taarifa ya mapato ya michango ya serikali, mapato yatokanayo na asilimia 5 ya mauziano, luzuku za mitaa zitokazo serikalini, michango itolewayo kwa ajili ya watoto waishio kwenye mazingira magumu, taarifa za mapato na matumizi ya mtaa wetu, taarifa za makusanyo ya michango ya ujenzi wa shule ya sekondari, shilingi 10,000 zinazokatwa kwa kila msiba zinafanya kazi gani pamoja na taarifa ya michango ya wadau ambao huwa wanatoa fedha kwa ajili ya maendeleo ya mitaa wakiwamo wananchi wenyewe” alisema Mgilangwa.
Akiendelea na ufafanuzi juu ya madai hayo alisema kuwa wamekuwa wakichangishwa michango mbalimbali kama vile kuchangia mchango wa shule ya sekondari MKWAWA lakini ujenzi wa shule hiyo haulidhishi na kila unapotokea msiba mwenyekiti wao hukata shilini 10,000 bila kueleza kazi yake.
“Tunachotaka hapa kila mtu aridhike katika nafasi yake lakini kama tutakuwa tunafichwa haki zetu wenyewe hatuwezi kukubailiana na hatutakubaliana. Haburuzwi mtu hapa. Uongo umezidi sasa” alisema Mgilangwa.
Afisa mtendaji huyo alishindwa kutoa majibu ya maswali hayo na kulazimika kukaa huku ububu ukimtawala.
Mwenyekiti wa mtaa huo Kened Mahona alipotakiwa kutoa majibu ya maswali hayo alishindwa kutoa ufafanuzi kwa kile alichosema hana kumbukumbu na kusema fedha huchuliwa na mkurugenzi wa Manispaa Teresia Mahongo ambapo hadi kiasi cha fedha kilichochukuliwa ni shilingi 560,000.
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo Tobiasi Kikula maarufu kama “Kikulacho” aliwaomba wananchi wawe na subira hadi jumapili ijayo ili mwenyekiti huyo aweze kuandaa taarifa sahihi.
Wananchi walionekana kutuliza hasira wakisubiri taarifa sahihi katika mkutano utakaofanyika jumapili ijayo huku wakiahidi kumnyoa mtu atakayeleta uongo mwingine.
No comments:
Post a Comment