masuguru

Tangazo la cheti

Tangazo la cheti
tangazo

KLERUU

KLERUU
KLERUU

CAPRICORN

CAPRICORN

Ibada

Ibada

Saturday, May 12, 2012

Rais wa wanafunzi RUCO atoa tamko kwa RC Iringa

Rais wa serikali ya wanafunzi  Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO) akitoa tamko juu ya vitisho vya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa tume ya uchaguzi.




Ikiwa ni siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Christine Ishengoma kutoa tamko vitisho kwa tume ya uchaguzi wa serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ruaha RUCO kujiuzulu, Rais wa serikali ya wanafunzi atoa tamko kali kumtaka mkuu huyo arekebishe kauli yake.


Akizungumza na Tanzania Daima chuoni hapo leo Rais wa serikali ya wanafunzi Elia Shibanda amesema wanakusudia kuandamana hadi kwa mkuu wa mkoa ili alitolee ufafanuzi suala hilo kwa kile alichodai hakikuzingatia sheria inayompa yeye kuingilia uchaguzi wa viranja wa vyuo au shule.


“Haiingi akilini ndugu mwandishi kitendo cha mkuu wa mkoa kuacha kazi zake na kuingilia uchaguzi wa viranja wa chuo. Kiujumla hakuna sheria inayowataka tume ya uchaguzi wa serikali ya wanafunzi hapa chuoni kujiuzulu kwa sasa kwa mujibu wa katiba yetu. Vitisho vya mkuu wa mkoa vinatupa shaka juu ya utendaji wake kazi” alisema Shibanda.

Imeelezwa kuwa wanafunzi walishaamua kuandamana kwenda kwa ofisi ya mkuu wa mkoa lakini uongozi ukawataka wanafunzi wavute subira ili mkuu huyo apate nafasi ya kurekebisha vitisho vyake kwa hiari.


“Wanafunzi walidhamilia kundamana kwenda kwa mkuu wa mkoa lakini tukawataka wavute subira ili mkuu wa mkoa apate nafasi ya kufuta vitisho vyake lakini kama ataendelea kukaa kimya, nitaitisha maandamano ambayo tunawaomba wananchi watuunge mkono hadi ofisini kwake ili aweze kutolea ufafanuzi mbele ya wanafunzi wote na jamii nzima” alisema Shibanda.


Shibanda amewataka wanafunzi kupuuzia vitisho hivyo ambavyo ni woga wa kushindwa kuwajibika na badala yake wasimamie misingi na katiba yao kama wanachuo bila kuyumbishwa na mtu yeyote.


“Sisi wanachuo msimamo wetu ni mmoja. Hatutishiki na vitisho vilivyo nje ya katiba yetu. Ninaamini kama tutakubali kutishika hakika vyeti vyetu vitakuwa vyakugushi. Tunachokusudia tunataka kiongozi ajenge hoja makini lakini siyo kututishia” alisema.


Akimnukuu mwandhishi wa vitabu wa uingereza William Shake Spea ambaye anasema “watu waoga hufa mara moja kabla ya kifo cha mwisho lakini mtu shujaa hufa mara moja” Shibanda amewataka wanafunzi kutokuogopa vitisho vya watu waoga wasio jiamini katika nafasi zake bali wawe shujaa kusimamia haki za jamii.


Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1970 alipohudhuria hafla ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema “Chuo Kikuu ni mahala pa kujifunzia elimu ya juu, namna ya kufikiri vizuri, fikra za kutokutegemea mtu mwingine, ni mahala pakutatulia mambo yasiyojulikana vizuri vile vile ni mahala pa kupatia majawabu magumu yaliyoshindikana kwa watu wasio na taaluma”.


Shibanda amesema mkuu wa mkoa alipaswa kufanya upembuzi wa kina kabla ya kutoa vitosho visivyo na msingi wowote.

“Nimkumbushe mkuu wa mkoa kuwa alipaswa kufanya upembuzi yakinifu na kuyapeleka kwa wanazuoni kabla ya maamuzi. Wanazuoni wanaendelea kutilia shaka juu ya uteuzi wake na nafasi yake kama mkuu wa mkoa kutokana na tishio alilotoa kutaka tume ijiuzulu. Tunatoa wito kwa wanairinga kutoa ushauri kwa viongozi kwa kutowaingilia katika nafasi zao” alisema.

Hata hivyo Shibanda amesema viongozi wanapaswa kuwasaidia wananchi katika hali zo za maisha magumu lakini siyo kuwanyanyasa.

“Viongozi kama mkuu wa mkoa wanatakiwa kuwasaidia wananchi wanaoishi chini ya dola moja na watoto wa wakulima wanaopata fedha za mikopo kwa njia ya maandamano na migomo baada ya kuchelewa badala ya kuwaingilia viranja wa vyuo vikuu” alisema.

Baada ya vitisho hivyo Misunza Gabriel (mwanasheria mwaka 4) miongoni mwa wanatume hiyo amejiondoa katika tume kwa kile alichodai kuwa yeye ni mtumishi serikalini kwahiyo anaogopa kufukuzwa kazi.

Alipohojiwa na Tanzania Daima juu ya mahusiano ya kazi serikalini na tume ya uchaguzi wa serikali ya wanafunzi alisema hana majibu juu ya suala hilo.

Tanzania Daima ilipotaka kujua mahusiano yake ya karibu na mkuu wa mkoa vitisho vilivyomsababisha kujitoa kwenye tume alishindwa kujijitetea na kusema hana majibu.

Tanzania Daima ilipomtaka mkuu wa mkoa kutoa ufafanuzi juu ya vitisho vyake kwa tume ya uchaguzi wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo juhudi zilishindikana baada ya simu yake ya mkononi kupokelewa saa 07:44 mchana na mwanamume na kusema yupo Kigoma.

“Mimi nipo Kigoma huyo unayemtafuta simjui”  alisema mwamume huyo ambaye hakutaka kujitambulisha na kukata simu.

 

No comments:

Post a Comment