![]() |
| Meneja mawasiliano wa mradi wa TUNAJALI Agnes Kabigi akiongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa Green City juu ya kampeni za "tokomeza maambukizi" hii leo. |
WANAUME wametakiwa kutowapuuza
wenzi wao wanapokuwa katika kipindi cha ujauzito na kuambatana nao kriniki ili
kupata ushauri wa pamoja kwa ajili ya kulinda afya zao na afya ya mtoto
anayetarajiwa kuzaliwa.
Imeelezwa kuwa kumekuwa na idadi
kubwa ya waume wanaopuuza kuambatana na mwenzi wake aendapo kriniki kwa kigezo
cha kuona aibu.
Akizungumza waandishi wa habari leo katika ukumbi wa Green City Makambako mkoani Njombe, Meneja mawasiliano wa mradi wa
TUNAJALI uliochini ya shirika la kupambana na Ukimwi (USAID) Agnes Kabigi
amesema suala la wenzi kuambatana kriniki si jambo la ajabu wala la aibu kwa
kuwa linasaidia kuijenga familia na jamii katika suala zima la afya.
Amesema njia hiyo inasaidia kwa
kiasi kikubwa kutokomeza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) kutoka kwa mama
kwenda kwa mtoto na kusaidia jamii kubadili tabia.
Hata hivyo ameitaka jamii
kutambua umuhimu wa kupima afya zao na kuachana na tabia zinazosababisha
kuingia katika maambukizi ya VVU ikiwa ni pamoja na kuacha ngono na kutumia
nafasi zao kusambaza virusi kwa makusudi.
Amefafanua kuwa huduma
zinazotolewa na shirika la Tunajali ni za bure ikiwa ni pamoja na kupata vipimo
vyote na ushauri bila gharama na kwamba wahudumu wamepewa mafunzo kwa ajili ya
kutoa huduma zilizo bora au zisizowaudhi wa wagonjwa.
Amesema mama mjamzito apatikanapo
na maambukizi wakati wa ujauzito huanzishwa dawa za kufubaza nguvu ya virusi
hivyo pamoja na kupata huduma ya kumkinga mtoto asiambukizwe na virusi.
Naye Naibu Mkuu wa Mradi TCCP –
JHU.CCP chini ya udhamini (ufadhiri wa serikali ya watu wa Marekani Deo Ng'wanansabi amesema elimu inayoendelea kutolewa kwa wanawake na wenzi wao juu
ya maambukizi ya VVU yatasaidia katika kutokomeza maambukizi mapya matika
familia na jamii.
Amesema jamii ikitoa ushirikiano
katika mapambano haya, janga la Ukimwi litakwisha kutokana na jamii kuwa na
elimu na mwitikio mkubwa katika kuacha kile kinachoweza kuwa ni chanzo cha maambukizi.
Amesema janga la Ukimwi siyo
wimbo wa kuimba na kuusahau bali ni jambo linalopaswa kufanyiwa kazi kwa kila
mmoja katika kujikinga na kupambana nalo ili jamii iwe salama katika kizazi
kijacho.
“Kwa pamoja tubadilike na kujenge
nguvu ya pamoja kwani viongozi pekee yao
hawawezi au wahudumu pekee yao
hawawezi bali sisi sote tukishirikiana tutatokomeza janga hili” amesema.
Amesema mikakati iliyopo kwa sasa
ni kutumia nyenzo zote kwa ajili ya kuihamasisha jamii kujua umuhimu wa
kuhudhuria katika vituo vya afya na kupata mwitikio mkubwa wa wanawake na wenzi
wao kupata matibabu kwa ajili ya kukinga maambukizi hayo.
Hata hivyo amesema jukumu la
kupambana na mimba za utotoni ni la kila mmoja katika familia na jamii nzima
kwa ujumla.
“Kila mmoja ana jukumu hilo kwa kushirikiana na
serikali kwa kuwa watoto tunaishi nao majumbani mwetu. Vile vile wazazi
wanapaswa kuwaeleza watoto wao madhara ya kujihusisha na suala la mapenzi
katika umri mdogo” amesema.
Kwa upande wake Dkt. Michael
Msangi kutoka Wizara ya Afya Makao Makuu ambaye anafanya kazi katika kitengo
cha afya ya Mama na Mtoto alisema hadi sasa utoaji huduma wa kutokomeza
maambukizi ya VVU imefikia asilimia 67.
Amesema kutokana na ufadhiri wa
watu mbalimbali kutoka nje unasaidia kupanua huduma kwa kiasi kikbwa ambapo
hadi sasa kuna vituo 914 nchini vinavyotoa huduma kati ya vituo 5066 vilivyopo.
Amesema lengo ni kupunguza
maambukizi kutoka asilimia 50 hadi kufikia asilimia 4 na hatimaye kutokomeza
kabisa.
Ameeleza kuwa wanawake wengi
wanakufa kutokana na maambukizi VVU na magonjwa nyemelezi kutokana na
kutokujitokeza kwa ajili ya kupata ushauri na huduma.
Takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka
2010 vifo vya akina mama wajawazito vinavyotokana na maambukizi vilikuwa ni
asilimia 11 na mwaka 2010 – 2012 vilikuwa ni asilimia 18 wakati maambukizi ya
VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa mwaka 2010 ni asilimia 26 na mwaka
2012 ni asilimia 15.
Tunajali wanatarajia kuzindua
mpango wa “tokomeza maambukizi” Mkoa wa Njombe ambapo unatarajia kufanyika leo
katika kituo cha afya cha mji mdogo wa Makambako.

No comments:
Post a Comment