RAIS wa Baraza la Maaskofu
Tanzania Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa amewata wakristo kumkumbuka Mungu
katika shughuli zao licha ya kuwa wanazongwa na mambo mengi katika pilika za
kutafuta mahitaji.
Ameyasema hayo juma hili wakati wa maadhimisho ya Misa ya
mazishi ya hayati askofu mstaafu wa Jimbo la Njombe mhashamu Raymond Mwanyika
na kwamba mwanadamu ana kiu ya Mungu.
Bila Mungu binadamu hawezi kupata
raha kwa kuwa Mungu ndiye anayemfanya binadamu kuwa na furaha wakati wote na kumuwezesha
kufanya kila analolitaka.
Anaendelea kusema ili kuwa
binadamu aliyekamilika, lazima kuwa na imani na amani katika kutoa huduma za
haki na uwajibikaji wa amani.
Pia anasema ukamilifu wa mtu ni kutumia
muda wake kwa ajili ya kupigania usawa na kutaka kila mmoja aweze kupata
chochote pasipo kikwazo na kwamba ukamilifu huo unasaidia kuwa na amani moyoni
mwake.
Amesema uzuri wa mwanadamu ni
pale anapoishi katika haki na amani kwa upendo na kuthamini wenzake kama viumbe wa Mungu bila kuonesha ubaguzi na upendeleo
katika utoaji huduma.
Mhashamu askofu Ngalalekumtwa
ambaye pia ni askofu wa Jimbo la Iringa na msimamizi wa Kitume wa Jimbo Kuu la
Songea anasema moyo wa mwanadamu umejaa mambo mengi ya hapa duniani yenye
udanganyifu mwingi ambayo ni kwazo kwa haki za wengine.
“Hupati raha ya kweli
pasipokuwepo Mungu. Pamoja na kufukuzia mambo mengi hapa duniani yenye udhaifu
mwingi, Mungu anamvuta mwanadamu kwa ajili ya uzima lakini msingi wa hayo yote
kinachotakiwa ni kuwa na imani na upendo kwa kila mmoja.
“Ni vema mwanadamu akayaelewa
hayo na kutenda kwa maongozo ya Mungu katika hekima na akili. Utamu na unono wa
mwanadamu ni pale unapotoa uhai kwa ajili ya wengine katika kutenda haki”
ameeleza.
Amesema mtu hawezi kuhubiri amani
wakati rohoni mwake hana imani na kwamba kwa kufanya hivyo ni kukosa ukweli
ndani ya nafsi yake na kwamba Dini ya ukristo siyo nadharia bali ni msingi wa
mafundisho wa yule aliyejitoa msalabani.
“Ukristo ni dini ya ukarimu wa
nafsi. Kristo ndiye kitovu na kiini cha kazi ya Mungu. Binadamu wote tumetolewa
na Mungu kama zawadi. Mungu anatulinda kwa
upendo na kutuhifadhi katika upole na faraja” anasema.
Vile vile anaeleza kuwa binadamu
akiwa ni mali
ya Kristo lazima ajiule mambo yote anayotenda kwani nia yake ni kutaka wanadamu
kujiweka chini ya uhai wa Baba yake.
Akimuelezea hayati askofu
Mwanyika, Mhasamu askofu Ngalalekumtwa anasema Alitamani kumsaidia kila mtu
lakini uwezo wake haukuruhusu kumfikia kila mmoja na kwamba alikuwa ni mtu
mwenye maneno machache na kuongea zaidi kwa matendo
Anasema kuwa hakuwa ni mtu wa
kugombana na yeyote, alihudumia kwa ukarimu na kuambatana na wakristo kwa
kusudi la wokovu.
“Kanisa Katoliki limejawa na
simanzi kuondokewa na askofu wa kwanza wa Jimbo la Njombe. Katika kipindi chote
cha uongozi wake, askofu Mwanyika amekuwa kielelezo na kuyatoa maisha yake kwa
Mungu na alikuwa mchapa kazi.
“Alifanya bidii kujenga jimbo ili
liweze kujitegemea. Alitamani kumsaidia kila mtu lakini uwezo wake haukuruhusu
kumfikia kila mmoja. Katika kipindi chake cha uuongozi alihamasisha sana miito. Alikuwa
kielelezi katika kuongoza malezi ya watawa jimboni” amesema.
Ameeleza kuwa Maaskofu watamkumbuka
jinsi alivyolihudumia Baraza la Maskofu Tanzania na kwamba alikuwa ni mtu
mwenye maneno machache na kuongea zaidi kwa matendo.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania
na Mbunge wa jimbo la Njombe Kusini Mama Anne Makinda alisema hayati askofu
Mwanyika alikuwa ni mtu muhimu kwa kuwa alikuwa na dhana ya ushirikiano katika
kuleta maendeleo licha ya kuwa alikuwa mtumishi wa Mungu.
“Kanisa limempoteza mtu muhimu sana. Alikuwa na moyo wa
maendeleo kwa kuhakikisha watu wake wanakuwa na amani, furaha, upendo na
alikuwa ni mtu wa huruma kwa kila mmoja bila kubagua” amesema.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilali alisema Taifa
linatambua mchango wa hayati askofu Mwanyika wakati wa uhai wake kwa kutoa
huduma kwa upendo na amani.
Anasema kuwa wakati wa uhai wake
alikuwa na uelewano kwa kila mtu bila kujali umri wa mtu, cheo na wasifu wake
na kutoa huduma kwa haki na kuhakikisha jamii inanufaika kiroho na kimwili.
Amesema kuwa askofu Mwanyika
wakati wa uhai wake alikuwa Alikuwa ni mtu mwenye uelewano na ni mtu aliyejenga
heshma katika Kanisa la Taifa kwa ujumla.
“Kuweni na ustahimilivu na subira
katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na Mungu awatie nguvu” anasema.
Amewataka watu wote kufuata
mafundisho yake ya amani, upendo, umoja na mshikamano kwa kushirikiana kwa kila
jambo.
Hayati askofu mstaafu Mwanyika
ambaye aliongoza Jimbo la Njombe kwa miaka 31 anaelezwa kuwa atakumbukwa kwa
mengi ikiwa ni pamoja na kufanya kazi zake kwa utulivu.
Kwa upande wake Makamu wa askofu
wa Njombe Padre Justin Sapula amesema Jimbo la Njombe limempoteza kiongozi
makini mwenye busara, mtu wa watu aliyempenda kila mmoja.
Mama Mkuu wa Shirika la Kitawa la Masista wa
Imilliwaha Sista Cotride Sanyika akizungumza na KIONGOZI amemwelezea askofu
Mwanyika kuwa wakati wa uhai wake alikuwa askofu ambaye hakupenda makuu na
kwamba alikuwa ni mtu wa watu.
Anasema alitumia hekima na burasa
kuwaongoza watu na kwamba alikuwa ni mtu mpole ambaye daima alikuwa akimtegemea
Mungu kwa kila jambo alilokuwa akilitenda.
“Aliwalea Mapadre na Watawa kwa
moyo mkunjufu. Hakupenda wakose kitu. Pia alikuwa mbunifu wa hali ya juu na
kutumia unyenyekevu katika utume wake. Aliwapenda hata viongozi wa kiserikali
kwa kutoa ushirikiano wa dhati kwa kuwa na mawasiliano ya karibu kwa kushiriki
shughuli za kimaendeleo” amesema.
Anna Silinu anasema kwa ujumla ni
pigo kubwa kwa wananjombe wote kwa kuwa askofu Mwanyika wakati wa uhai wake
alikuwa ni mtu wa mfano kwa kila kitu na kuhubiri amani, upendo na mshikano
bila ubaguzi.
Anasema wengi wanajifunza kutoka
kwake yale aliyokuwa akiyafanya na kuyatenda kwa kutoa ushirikiano katika mambo
yote ya kiroho nay a kijamii bila kurudi nyuma.
“Alikuwa ni mtu wa kujitoa bila
kujibakiza. Pamoja na kuwa alitoka katika familia masikini alikuwa ni mtu
muelewa kwa matatizo ya wanajamii. Alisistiza san asana watu tuishi kwa upendo
na amani” anasema.
Amesema katika hali isiyo kuwa ya
kawaida hayati askofu Mwanyika wakati wa kuugua kwake alionekana mwenye furaha
kushiriki mateso ya Kristo bila manung’uniko.
Silinu amewataka wakristo
kutowazuia watoto wao kufuata miito yao kwa kuwa Mungu humuita mtu kwa njia
tofauti na kwamba upadre na utawa na wito ambao una baraka na heri katika
maisha ya kiroho na kwamba malezi ya kiroho yanategemea uwepo wa watu
waliojitoa kiimani.
“Ushirikiano hauwezi kuzaa matunda
bila kuwa muwazi na mkweli. Tusiwanyime watoto wetu haki zao” amesema.
Wakati huo huo msemaji wa familia
Weliner Mwanyika amesema familia imepata pigo kwa hayati askofu Mwanyika
alikuwa nguzo ya familia
Amesema pengo lililopo haliwezi
kuzibika kutokana na nafasi yake aliyokuwa nayo na ukaribu wake kwa watu wote
katika familia na kutoa mahitaji bila upendeleo.
“Alikuwa akisikia tatizo tu, mara
moja alikuwa anawajibika. Alikuwa ni mtu wa karibu na familia. Katika familia
tumempoteza mtu muhimu sana”
amesema.
Hata hivyo amesema maisha yake yamekuwa
mwanga wa imani kwa familia na kuwataka wanafamilia kuyaishi yale aliyokuwa
aliyasisitiza kwa kuishi kwa upendo na kuruhusu miito ndani ya familia ili
kupata viongozi wa kiroho.
Amesema wajitoe katika yaliyo
mema kwa kumtumikia Mungu kwa kufanya ushirikiano na viongozi wa kiroho
kuiombea miito mitakatifu na kuwa mwanga wa njia ya haki na kweli katika maisha
kikristo.
Pia amesema kujituma ni jambo la
heri kwa ajili ya maendeleo ya Kanisa na ustawi wa kiroho kwa kushiriki katika
utume mbalimbali na kujitoa kwa uhakika kama hayati askofu Mwanyika alivyokuwa
akifundisha na kutenda katika katika maisha yake.
Katika familia hiyo tayari kuna
mapadre wawili, Pd. Prasdos Mwanyika na Pd. Osmund Mwanyika.
Askofu mstaafu Raymond Mwanyika wa Jimbo
Katoliki la Njombe, alifariki dunia 24 Oktoba 2013, akiwa na umri wa miaka 83.
Alizaliwa kunako mwaka 1930. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi,
akapadrishwa 11 Oktoba 1959.
Baba Mtakatifu Paulo wa sita, akamteua kuwa Askofu 16 Januari 1971 na hatimaye kuwekwa wakfu 25 Aprili 1971. Baada ya kuwatumikia watu wa Mungu, Jimbo Katoliki la Njombe kwa moyo na akili zake zote, akang'atuka kutoka madarakani 8 Juni 2002.
Baba Mtakatifu Paulo wa sita, akamteua kuwa Askofu 16 Januari 1971 na hatimaye kuwekwa wakfu 25 Aprili 1971. Baada ya kuwatumikia watu wa Mungu, Jimbo Katoliki la Njombe kwa moyo na akili zake zote, akang'atuka kutoka madarakani 8 Juni 2002.
Tangu mwanzo wa kazi yake kama askofu
alijizatiti kimamilifu katika kazi ya kulilea Jimbo changa, kulitunza na
kulielendeleza kwa hali na mali.
Kwa miaka yote katika kazi yake aliongoza kwa busara, upole uvumilivu na
unyenyekevu akishirikiana vema na wachungaji wote Wamisionari na wazalendo,
watawa na walei bila ubaguzi.
Marehemu Askofu Raymond Mwanyika atakumbukwa na wengi kutokana na mchango wake mkubwa wa maendeleo endelevu kwa wananchi wa Njombe. Amezikwa katika Kanisa la Kiaskofu jimboni Njombe.
Marehemu Askofu Raymond Mwanyika atakumbukwa na wengi kutokana na mchango wake mkubwa wa maendeleo endelevu kwa wananchi wa Njombe. Amezikwa katika Kanisa la Kiaskofu jimboni Njombe.
No comments:
Post a Comment