| Barua iliyonaswa baada ya ofisa mtendaji kuwaandikia wazazi na walezi wa wanafunzi kwa ajili ya kutoa michango. |
BAADHI ya wanafunzi wa darasa la saba wakiwemo watoto yatima
wa shule ya Msingi Kimala Kata ya Kimala Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa huenda
wasifanye mitihani ya mwisho kutokana na kukosa michango ya shilingi 47,000/=
ambayo wanadaiwa shuleni hapo.
Baadhi ya wanafunzi hao wameuambia mtandao huu kuwa
uwezekano wa kutokufanya mitihani upo kutokana na sababu nyingi ambazo
wanaziona ikiwemo ya kutokuruhusiwa kuingia madarasani wakati wa vipindi na
madala yake kufanyishwa kazi nje.
Wakiongea na mtandao huu shuleni hapo, wanafunzi hao (majina
tunayo) walisema wamekuwa wakifanyishwa kazi na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo
Ahamed Twalipo badala ya kusoma kwa sababu ya kuwa hawajalipa michango.
Walifafanua kuwa licha ya kutokuingia darasani kusoma
walizuiliwa kufanya mitihani ya kanda jambo ambalo wananchi walilipigia kelele
na kulazimishwa kufanyishwa mitihani 7 kwa siku 2 ambapo walikuwa wakifanya
hadi usiku.
Wakizungumza na mtandao huu kwa nyakati tofauti, wananchi wa
kijiji hicho walisema Mwalimu Mkuu wa shule hiyo amekuwa mbabe kutaka kila
anachokitaka yeye kifanyike pasipo makubaliano ya wazazi ama kamati ya shule.
Imeelezwa kuwa miongoni mwa michango hiyo ni pamoja na
mshahara wa mratibu elimu ambao mwalimu huyo kwa kushirikiana na ofisi ya
kijiji wamebuni licha ya kuwa mratibu huyo analipwa na serikali.
Boniface Kasuga ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya shule hiyo
ameonesha kushangazwa na mchango huo kuwa ni mipango ya watu binafsi na kuwa
haujawahi kujadiliwa katika mikutano au vikao vya kamati ili kuona umuhimu wa
wazazi au walezi kutoa michango hiyo.
“Hii michango ni ya uonezi. Mimi ni mzazi pia lakini mchango
huo siujui pamoja na kuwa ni mjumbe wa kamati. Ninachojiuliza ni kwamba;
mratibu anateuliwa na Mkurugenzi, kwa nini sisi wananchi tumlipe?
“Pia mchango wa darasa la saba unakujaje kwa kila mwanafunzi
kutozwa shilingi 47,000/=? Kuna watu wachache tu ambao wanapanga michango hiyo
kama ulaji kwao” alisema Kasuga.
Pia wananchi wamemlalamikia mwalimu huyo kutumia lugha za
matusi, kejeli na vitisho kwa wazazi wanaofika shuleni hapo kujiuliza uhalali
wa michango hiyo na mara nyingine kuwadharirisha wazazi mbele ya watoto wao
shuleni hapo.
Mwalimu Twalipo anadaiwa kuuza chakula walichochanga wananchi
kwa ajili ya wanafunzi wawapo shuleni hapo mchana kwa madai ya kukarabati
nyumba za walimu bila kushirikisha kamati ya shule.
Mwanafunzi ambaye aliomba jina lisiandikwe mtandaoni alieleza
kuwa mzazi wake alidharirishwa na mwalimu huyo shuleni hapo alipofika kutaka
ufafanuzi wa michango hiyo ambapo mwalimu Mkuu alimtolea maneno ya dharau,
matusi na kumrushia fedha aliyokuwa ameitoa kwa ajili ya mchango ambao amekuwa
akirudishwa mara kwa mara kwenda kuuchukua nyumbani.
Fened Ngusulu na Omari Kahemela ni miongoni mwa wananchi
walioueleza mtandao huu kwa nyakati tofauti kuwa walitukanwa na kutolea maneno
ya matusi na mwalimu huyo shuleni hapo walipofika kwa ajili ya kujua zaidi
kuhusu michango hiyo.
Katika mkutano wa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Gerald Guninita uliofanyika
kijijini hapo Agosti 28, 2013 alisema kuwa shule za msingi hazina michango na
kwamba kama michango hiyo ipo ni makosa.
Mweyekiti wa kamati ya shule hiyo Telaki Ndenga amethibitisha
kuwepo kwa michango hiyo na kwamba kamati ya shule haijawahi kushirikishwa juu
ya michango hiyo.
“Ni kweli michango hiyo ipo lakini sisi viongozi wa kamati
hatuijui wala hatuwezi kuizungumzia. Hiyo ni mipango ya mwalimu mkuu na
viongozi wa kijiji ambao wanataka kuila ila ingekuwa halali tungeshirikishwa.
Kwa kawaida michango yote halali ambayo inatakiwa kutolewa huwa inajadiliwa
kwenye vikao vya kamati kwanza kabla ya kuwatangazia wananchi.
“Cha kushangaza mwalimu Mkuuamegeuza shule kuwa mali yake
wakisaidiana na uongozi wa kijiji kuwakandamiza wananchi. Huo ni wizi tu ambao
wanaufanya kwa maslahi yao binafsi. Kibaya zaidi wanafanya bila kutushirikisha
viongozi wa kamati” alisema.
Hata hivyo barua iliyoandikwa na ofisa mtendaji wa kijiji
hicho Festo Mtenga kuwataka wazi na walezi wa wanafunzi wanaodaiwa michango
shuleni hapo kutoa haraka vinginevyo hatua kali zitachukuliwa imenaswa na
mtandao huu.
Mkuu wa shule hiyo alipotafutwa shuleni hapo kwa ajili ya
ufafanuzi zaidi, hakuweza kupatikana kwa kile kilichoelezwa kuwa amekwenda
kwenye kikao cha halmashauri wilayani na hata alipopigiwa simu ilipokelewa na
mwanamke aliyejitambulisha kuwa ni mke wake na kusema kuwa mumewe hayupo na
isingekuwa rahisi kumuona.
Mitihani ya darasa la saba inatarajiwa kuanza kufanyika
nchini Septemba 12, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment