| Mistari inayoonekana katika picha ni nyufa za jengi hilo ambapo kiti kinatengana na ukuta hali inayoweza kusababisha jengo hilo kuporomoka wakati wowote. |
JENGO la sekondari ya Kata ya Kimala Wilaya ya Kilolo mkoani
Iringa lipo hatarini kuanguka kabla ya kumalizika kujengwa kutokana na kile
kinachodaiwa kujengwa chini ya kiwango huku viongozi wa Kata akiwemo Diwani wa
kata hiyo wakibebeshwa lawama za matumizi mabovu ya michango ya wananchi.
Wakizungumza na mtandao huu kijijini hapo kwa nyakati
tofauti, wananchi hao wameonesha kusikitishwa na michango yao kutumika vibaya
huku wakikosa ufafanuzi wa njia zilizotumika kumpata mkandalazi wa jengo hilo.
Telaki Ndenga mwananchi wa kijiji cha Kimala ameliambia
gazeti hili kijijini hapo kuwa wananchi wamekuwa wakipuuzwa na viongozi pale
wanapohitaji ufafanuzi juu ya jengo hilo kuonesha dalili za kuanguka huku
wakisukumiwa matusi.
Alisema kila wakati wamekuwa wakitoa malalamiko yao kwa ofisa
Mtendaji wa Kata hiyo na kwa diwani wao lakini wamekuwa na kigugumizi cha kutoa
ufafanuzi juu ya suala hilo na badala yake kuitwa wajinga.
“Suala hili ni la muda mrefu tu kwani tuliliona mapema kabisa
kuwa jengo linalojengwa kwa ajili ya shule ni bomu kwa watoto wetu watakaosoma
hapo; tumetoa malalamiko yetu kwa mtendaji wa Kata na diwani lakini majibu
hatupewi.
“Tatizo linaloonekana hapa diwani na mtendaji wao ndiyo kila
kitu. Hawashirikishi kamati ya ujenzi ila wao wanachokiamua ndicho wanachotaka
kifanyike. Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya tulichukua hatua ya kutoa
malalamiko yetu kwa Mkuu wa Wilaya ila mengine alitujibu na mengine akatuambia
kuwa anayafanyia kazi” alisema.
Rudio Mtenga mmoja wa wanakamati ya ujenzi wa shule hiyo
alisema kuwa wanankamati wamedharauliwa na viongozi hao ambapo wanafanya kazi
kwa kujinufaisha badala ya maendeleo ya wananchi wote wanaotoa michango yao kwa
ajili ya ujenzia wa shule hiyo.
Alisema wakati mwingine vikao vya kamati ya ujenzi
vinavyofanyika ni vya kihuni kwa kile alichoeleza kuwa vimekuwa vikiitishwa na
ofisa mtendaji wa Kata na diwani ambao wanajihusha moja kwa moja na matumizi
machafu ya pesa za wananchi.
Alieleza kuwa wakati vikao hivyo vikiitishwa, wanakamati
wamekuwa hawana hoja kwa kile walichokuwa wakielezwa kuwa hawajapewa semina na
kutakiwa kukaa kimya.
“Tulipohoji diwani alitujibu kuwa hatujapewa semina kwa hiyo
tutapata nafasi ya kuhoji tutakapopata semina. Tangu hapo wamekuwa wakichukua
michango kwa wananchi bila kutushirikisha sisi wanakamati.
“Desemba 25, 2012 tulikubaliana kuwa kamati ipewe majukumu
yake tukianza na utafutaji mbao lakini tulipotafuta mbao na kurudisha majibu
ili tupewe fedha ya kulipa tukaambiwa mbao zimeshanunuliwa. Tulipouliza ni nani
kanunua wakati kazi hiyo ni ya kwetu, diwani alisema juu ya mbao tusiulize ila
tuendelee na mambo mengine japo kuwa kamati walisema bila kujulikana mnunuzi wa
mbao hizo kamati haiwezi kuendelea kufanya lolote” alisema.
Alisema kutoka hapo diwani na ofisa mtendaji wakatumia nguvu
kujengea mbao hizo japo kuwa zilikuwa chini ya kiwango kwa mujibu wa ujenzi wa
jengo hilo na kwamba tangu hapo hawajawahi kushirikisha kamati shughuli yoyote
inayoendelea.
Boniface Kasuga mwanakamati wa ujenzi wa shule hiyo alisema
michango ya wanachi inatumiwa na watu wachache kwa manufaa ya familia zao bila
kujali kuwa ni kuwaumiza wananchi wanaojitoa kwa ajili ya maendeleo ya elimu.
Alisema kuwa fedha zinazotolewa na wananchi kwa ajili ya
ujenzi hazifikishwi kwenye kamati kwa ajili ya kupangia bajeti na badala yake
diwani na ofisa mtendaji wa kata wamekuwa wao ndio wanakamati na ndio
watendaji.
“Pia fedha inayotoka halmashauri sisi wanakamati tunatakiwa
tuandikie bajeti lakini wao hawafanyi hivyo na tunaambiwa tu kuwa hela hizo
wanazichukua na kwamba zikichukuliwa zitafanya kazi gani hatuambiwi wala
hatujui na pia hatujui wanatumia muhtasari gani kuchukua fedha hizo. Hapo ndipo
tunapoona mtendaji wa kata na diwani
hawatutendei haki” alisema Kasuga.
Naye mjumbe wa Kamati hiyo Sadick Kasuga alisema kuwa mafundi
wanaojenga jengo hilo linabomoka ni ndugu zake na diwani.
Alisema waliligundua hilo mapema tu kwenye kikao cha kwanza
kwa ajili ya kuanza kujenga jengo hilo na kwamba walitilia shaka juu ya uhalali
wa jengo hilo kutokana na mafundi hao kuwa ndugu wa diwani.
“Sisi wanakamati tunaulizwa na wananchi juu ya maendeleo ya
jengo hilo na kwamba ni kwa nini linabomoka lakini tunashindwa kuwajibu kwa
sababu kila kitu wamejihodhisha viongozi bila kutushirikisha sisi wanakamati.
“Tunachopenda kama wataalamu wa majengo wangefika hapa ili
waone hali halisi na wathaminishe kwa jengo lenyewe na gharama zilizotumika
wangejua kabisa kuwa tunachokizungumza sisi siyo uzushi bali nikitu cha kweli”
alisema.
Hata hivyo alisema kuwa waliandika barua kwa ofisa mtendaji
wa kata kuomba maandamano ya amani kuelekea sehemu ya jengo ili wananchi watoe
kero na hisia zao lakini mtendaji huyo hakuwa tayari kuruhusu maandamano.
“Wananchi waliandika barua ya kuishtaki kamati ya ujenzi ambayo
nayo haikujibiwa hadi leo. Tukihoji matumizi wanatuambia kuwa Mkurugenzi
amesema hana fungu la kuendesha semina. Chakushangaza vifaa vya ujenzi vinaanza
kukarabati jengo ambalo halijaisha badala ya kuendelea kujenga majengo mengine.
Hii ni aibu kubwa hata kwa wenzetu wanaoliona jengo hili” alisema.
Mtandao huu umefanikiwa kufika katika eneo la jengo hilo na
kushuhudia jengo hilo likiwa na nyufa nyingi kala sehemu pamoja na kuwa
linaendelea kujengwa huku nyufa zingine zikiwa zimezibwa na kupasuka tena na
kulazimika kujengwa nguzo nyuma ya jengo ili kuzuia lisiporomoke.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Gerald Guninita
alipoelezwa na wananchi katika mkutano uliofanyika Agosti 28, mwaka huu alisema
atalifanyika kazi na kwamba majibu yatatolewa ambapo alitoa mifuko 50 ya saruji
kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.
Ofisa mtendaji wa Kata hiyo Richard Ngungulu alipotafutwa
ofisini hapo hakuweza kupatikana licha ya ofisi kuwa wazi na kutokuwepo mtu
yeyote na lakini alipotafutwa kwa simufua.
“Huo ni uongo tena ni uzushi. Usiamini maneno ya watu, hao
waliokuambia hivyo ni waongo tu” alisema
Naye diwani wa kata hiyo Mejusi Mgeveke alipotafutwa hakuweza
kupatikana kwa kile kilichoelezwa kuwa yupo kijijini kwake Idunda ambako hakuna
mawasiliano ya simu.
No comments:
Post a Comment