![]() |
| Dkt. Christine Ishengoma |
VIVUTIO vya 67 vya utalii
vimetambuliwa katika Mkoa wa Iringa ambavyo vimeanza kutangazwa kupitia
vipeperushi na wasifu (profile) wa utalii.
Pamoja na vivutio hivyo kuanza
kutangazwa, uhamasishaji unaendelea kufanyika katika sehemu mbalimbali zikiwemo
shule na taasisi mbalimbali ambapo jumla ya shule 12 na Taasisi 4 zimeshakwisha
pata uhamasishaji wa utalii katika Mkoa huo.
Akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake leo Mkuu wa Mkoa wa Iringa Christine Ishengoma alisema
kamati ya utalii Mkoa kwa kushirikiana na TANAPA, Taasisi za Elimu ya Juu,
Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na wadau mbalimbali wanaendelea kutoa
elimu juu ya utalii.
Amesema utangazaji wa vivutio
hivyo unakwenda sambamba na utangazaji wa wasifu wa uwekezaji kupitia vikao
mbalimbali ambapo vikao vitano vimekwisha kufanyika katika Halmashauri ya
Kilolo na Manispaa ya Iringa.
Ishengoma amesema umefanyika
uhamasishaji wa usindikaji wa mazao kwa vikundi vitatu kwa msaada wa Shirika la
MUVI juu ya umuhimu wa kusindika mazao kabla ya kuyauza kwa kufuata viwango
vinavyokubalika na shirika la viwango Tanzania (TBS) ili kuongeza thamani ya
zao.
Hata hivyo amesema jumla ya
maeneo 159 yametengwa na kuendelezwa katika halmashauri kwa ajili ya kuendeleza
viwanda vidogo vidogo.
Kwa upande wa biashara Ishengoma
amesema jumla ya vikundi 8 vya wajasiriamali vimepatiwa mafunzo kuhusu mbinu za
kuyafikia masoko ya nje katika halmashauri ya Iringa vijijini na Manispaa.
“Uhamasishaji katika Halmashauri
zote umefanyika kupitia Idara za kililo, mifugo na biashara kwa kuwaelimisha
wananchi kutumia bidhaa za ndani ambapo vijiji 100 vimefikiwa. Halmashauri zimeendelea
kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa kutekeleza sheria za usajili wa
shughuli za biashara (BRELA) kwa kuhakikisha biashara mbalimbali zinasajiliwa
katika vijiji” amesema.
Katika ujenzi wa miundombinu
amesema jumla ya Km 720.04 za barabara zimefanyiwa matengenezo ya aina mbalimbali
ikiwa Km 236.0 zimefanyiwa matengenezo ya kawaida, Km 299.1 za maeneo korofi na
km 184.14 zimefanyiwa matengenezo maalum.
Hata hivyo ujenzi wa barabara ya Iringa
– Mafinga umekamilika kwa asilimia 95 wakati barabara ya Iringa – Dodoma ujenzi wake
umefikia asilimia 65.

No comments:
Post a Comment