| Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa akihubiri wakati wa maadhimisho ya Misa ya Upadrisho na Yubilei ya miaka 75 ya Parokia ya Kaning'ombe. |
| Padre Victorino Kalinga akiwa amelala kifudifudi akiombewa Roho Mtakatifu kabla ya kuwa Padre. |
| Mhashamu Baba Askofu akimuweka wakfu Padre Victorino Kalinga |
RAIS wa Baraza la Maaskofu Tanzani Mhashamu Tarcisius
Ngalalekumtwa amewataka watu wasiwe wasanii kwa kutumia jina la Mwalimu Nyerere
kuwa wanamuenzi huku wakifanya mambo ya ajabu ya unyanyasaji na ukandamizaji wa
haki za watu.
Aliyasema hayo jana katika maadhimisho ya Misa utoaji wa daraja la
Upadre kwa Shemasi Victorino Kalinga iliyokwenda sambamba na maadhimisho ya
Yubilei ya Miaka 75 ya Parokia ya Kaning’ombe jimbo Katoliki la Iringa.
Askofu Ngalalekumtwa ambaye pia ni askofu wa Jimbo la Iringa alisema,
kutokana na usanii wa watu wanaojifanya wanamuenzi hayati Baba wa Taifa Julius
Nyerere huku wakifanya mambo ya kihuni ipo siku uongo wao utawatokea puani.
“Ipo siku mtasema mnamuenzi halafu mmkute ameketi juu ya
kaburi sijui mtasema nini? Nyio watu wadanganyifu mnaotumia jina la Mwalimu
Nyerere, acheni usanii, uhuni na uongo kuwadanganya watu wenye akili” alisema.
Alisema kuwa si kila mtu amefirisika kifikra na kwamba watu
wanajua kila kitu kinachoendele kuwa ni uongo au ukweli.
Alisema binadamu wa leo ametoka nje ya matakwa ya Mungu na
kufanya mambo yasiyo stahili kwa kutenda dhambi kwa kujifanya wema huku
wakiwaumiza wenzao.
Aliwaasa Wakristo kuwa wajumbe wa habari njema kwa ajili ya
kulinda amani ambapo wanatakiwa kumtafuta Mungu kwa ajili ya wokovu.
“Maaskofu na Mapadre wameteuliwa na Mungu kwa ajili ya
kufungua mioyo ya watu ili waweze kumtafuta Mungu na kuufifikia wokovu wa wa
milele.
“Mungu mwenye upendo, huruma na msamaha ni Yule tunayehitaji
kuajikabidhi maisha yetu kwa ajili ya furaha ya milele” alisema askofu
Ngalalekumtwa.
Hata hivyo alisema Padre anapasika kuwa na msimamo usio na
lawama ili asije akachakachua maagizo ya Mungu na kujitunza nafsi yake kwa
ajili ya kuwa muangalizi mwema wa kondoo alioachiwa na Mungu.
“Padre awe na msimamo safi na awe na akili kichwani ili apate
kubaini kufichua na kukemea yale ambayo hayastahili yanyowafanya wana wa Mungu
kuishi kwa hofu. Padre ni mjumbe wa amani ambaye anatakiwa kuwa mstari wa mbele
kwa ajili ya kuishi kwa upendo, mshikamano na kuwahurumia wengine” alisema.
Alisema kuwa pamoja na purukushani zote zilizopo, bianadamu
ana kiu ya Mungu ambayo padre anatakiwa kuizima kiu hiyo.
Alisema kuwa wakristo wanatakiwa kukusanyika pamoja na kutoa
dua kwa Mungu ili kuliombea Taifa linaloingiliwa na watu wasio na mapenzi mema
wanaopenda kuwasambaratisha watu wasio kuwa na hatia.
Miaka 75 ni heshima tuliyopewa na Mungu kwa ajili ya
kutangaza uweza wake kwa mataifa ambayo bado hayajamfahamu.
“Miaka 75 iwe ishara ya kuendeleza na utamaduni wetu wa
upendo aliotuachia Kristo Mwokozi kwa ajili ya maisha yetu. Lindeni hayo ili
Mungu Mwenyezi azidi kutulinda katika ukamilifu wa upendo, mshikamano, huruma,
hekima, busara na amani” alisema.
Kanisa lazima litoe lishe kwa watu wake ili miili yao isishambuliwe na
magonjwa ya dhambi. Kwa njia ya padre, binadamu watapata faraja ya Mungu kwetu
tunaoishi katika bonde la machozi.
No comments:
Post a Comment