KAMA maktaba za jamii zingekuwa nyingi kama zilivyo nyumba za kulala wageni, elimu nchini
ingekuwa kwa kiwango kikubwa tofauti na alivyo sasa.
Haya yamevungumzwa na Mkurugenzi wa asasi isiyokuwa ya kiserika ya Tuwafikie Tanzania Bovan Mwakyambiki alipokuwa akiongea na mtandao huu leo.
Mwakyambiki amesema angetamani maktaba za jamii zingekua nyingi kuliko nyumba za kulala wageni ili kukuza wigo wa elimu na kutoa fulsa kwa kila mmoja kujisomea kile anachopenda.
“Kama tunavyoyahangaikia matumbo yetu kuyalisha vyakula vizuri na kupata nguvu, vivyo hivyo jamii inavyopaswa kulisha na kuboresha fikra kwa kujiongezea uwezo wa kufikiri na utaalamu wa mambo mbalimbali. Jamii yetu imekua ikiisikia njaa ya tumbo kwa hisia kubwa sana na kuipuuza sauti au hisia ya ukosaji wa chakula cha akili na fikra” amesema Mwakyambiki.
Amesema ni jambo la kushangaza kuona ya kwamba sekta ya elimu inakosa kupewa kipau mbele na kuzidi kuzalisha jamii ya watu wasiojitambua, jamii isiyoelimika na jamii isiyojua kusoma na kuandika kwa ufasaha.
Amesema jamii imeiweka elimu katika kundi dogo sana na kufifisha uwezo wa kufikiri na kutumia muda wa kuongeza uelewa kwa kujisomea mambo mbalimbali ya kijamii na kisayansi.
“Jamii inafikiri kwamba suala la kujisomea ni la wanafunzi waliopo mashuleni kitu ambacho si sahihi. Kila mtu kwa nafasi yake anawajibu wa kujisomea mambo mbalimbali ili kuweza kuboresha fikra zake na kuongeza uwezo wa kufikiri. Ujinga wa mwanadamu umeelezwa ikiwa ni hali ya kukosa au kutokua na elimu, kukosa taarifa na kutojitambua. Unaweza kuwa umepata elimu fulani na ukawa na taarifa kuhusiana na jambo fulani lakini kama utakosa kujitambua bado utabakia kuwa mjinga” amesema Mwakyambiki
Amesema kuwa asilimia kubwa ya jamii bado inaishi vijijini, na huko ndiko kwenye changamoto nyingi zinazohusiana na suala la utoaji na upokeaji wa elimu.
“Ili kuwa na jamii iliyoelimika tutahitaji kuwa na jamii ambayo itakuwa na tabia za kujisomea na kutafuta taarifa mbalimbali ili kuweza kufanikisha uletaji wa maendeleo katika jamii yetu. Maktaba za jamii ni moja ya jambo muhimu kutiliwa mkazo na kushiriki kuweza kufanikisha kuwa na maktaba za jamii za kutosha hasa vijijini ili kuiwezesha jamii yetu kujifunza na kupata taarifa mbalimbali” amesema.
Amesema njia hiyo itasaidia hata wanafunzi ambao wanatokea katika mazingira magumu kuweza kuazima vitabu kwa urahisi na kuvitumia kwa kuwa ni njia mojawapo inayosaidia kuondoa adha kwa waalimu kwa kuwa na eneo ambalo litawasaidia pia kuandaa mambo mbalimbali yatakayoweza kuboresha aina ya mada wanazofundisha na kuongeza ufaulu wa watoto waliopo vijijini.
“Maktaba za jamii vijijini zitasaidia pia kupunguza mimba za wanafunzi mashuleni, na pia zitasaidia kuleta mitizamo mipya na yenye ubora itakayopelekea jamii kuwa na fikra bora, taarifa sahihi na kujitambua. Maktaba za jamii zitawasaidia wakulima na wafugaji kuweza kujipatia taarifa mbalimbali ndani ya maktaba hizo” amesema.
Ameongeza kuwa watu wa vijijini wanashindwa kujua umuhimu wa maktaba kwa kuwa hawana elimu ya kutosha na uelewa juu ya umuhimu wa elimu katika jamii.
“Inashangaza sana unapoongea na watu waishio vijijini na kuwauliza maana ya maktaba na kujibu kuwa maktaba ni duka la vitabu na yote haya yanatokea kwa sababu jamii yetu imejisahau sana na kuanza kuichukulia elimu kama jambo la anasa. Ujenzi wa maktaba za jamii vijijini sio anasa bali ni jambo la muhimu kufanyika ili kuongeza na kuboresha utoaji na upokeaji wa elimu au taarifa mbalimbali katika jamii yetu” amesema.
Asasi ya Tuwafikie Tanzania imeanzisha mradi wa kujenga maktaba vijijini na inashirikisha jamii yote ya watanzania kushiriki kwa njia ya hali na mali ili kuweza kufanikisha ujenzi wa maktaba za jamii vijijini na sasa ujenzi wa maktaba ya jamii kijiji cha Lugalo, mkoani Iringa unaanza ambapo lengo ni kujenga maktaba kwenye mikoa yote nchini.

No comments:
Post a Comment