UCHAGUZI wa wajumbe wa mabalaza ya Katiba katika
Mtaa wa Ngome Kata ya Kihesa katika Manispaa ya Iringa umewashangaza wakazi wa
mtaa huo baada ya ofisa Mtendaji kudaiwa kuwaingiza watu wake bila kufanyika
uchaguzi.
Imeelezwa kuwa ofisa mtendaji huyo amekuwa na
kawaida ya kufanya maamuzi yake bila kuwashirikisha wananchi licha ya kuwa
wananchi ndiyo watendaji wa maendeleo.
Wananchi wa mtaa huo wameeleza kuwa katika taratibu
za ufanyaji mikutano zimekuwa zikikiukwa mara kwa mara hata ofisa huyo
kushirikiana na baadhi ya watu kumpiga vita mwenyekiti wa mtaa huo kutokana na
kuwa mkweli na muwazi katika shughuli zake.
Hata hivyo wakazi wa mtaa huo wamesema
hawakutangaziwa sehemu ambayo uchaguzi huo utafanyika sambamba na kutoyaona
majina ya wagombea wa nafasi hizo ambayo kwa mujibu wa mwongozo wa uundwaji wa
mabaraza ya Katiba yalikuwa yabandikwe ili wanamtaa husika waweze kuyaona na
kudhiria.
Walisema kuwa zengwe hilo lilianza wakati wa
kuwasilisha majina ya kugombea nafasi hizo kwa kile walichokuwa wakiambiwa kuwa
anayeandika barua lazima awe anamiliki nyumba.
“Watu tumeandika barua za kugombea nafasi hizo
lakini tulipowasilisha kwa mtendaji akasema kama hatumiliki nyumba
haturuhusiwi. Ina maana hivyo Katiba ni ya watu wenye nyumba tu? Mtendaji alishindwa
kutuambia ukweli kuwa ana watu wake anaowataka awaingize huko kama alivyozoea”
alisema mkazi mmoja ambaye alikuwa na hasira.
Na kwamba “mwenyekiti wetu anapofanya vizuri
wanampiga vita tena akishirikiana na watu wachache tu ambao anataka kufanya nao
wizi. Na sababu ya kumpiga vita ni kwa sababu ni muwazi, hafichi kitu kama
wanavyofanya wao”.
Ofisa mtendaji wa mtaa huo Eliques Ngakonda
alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi juu ya hilo alisema uchaguzi ulifanywa na watu
105 katika viwanja vya soko jipya linaloendelea kujengwa katika mtaa huo.
“Tumefanya uchaguzi katika viwanja vya soko ambapo
kulikuwa na watu 105 walioshiriki katika uchguzi huo saa 5 asubuhi na majina yalibandikwa” alisema
Ngakonda.
Alipotakiwa kutaja majina ya watu waliochaguliwa
alisema majina hayakumbuki kwa kuwa hayupo ofisini.
Hata hivyo alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa tuhuma
anazotuhumiwa kutumia mabavu katika uongozi wake alishindwa kujieleza kwa kile
alichosema hajui lolote.

No comments:
Post a Comment