| Baraka Frank mwenyekiti wa waendesha bodaboda Mafinga akihojiwa na mtandao huu |
| Sehemu ya maegesho ya bodaboda Mafinga mbele ya stendi ya mabasi |
MAGARI ya serikali yamedaiwa kuwa
ni chanzo cha ajali barabarani kwa kukiuka sheria na taratibu za matumizi ya
barabara.
Haya yamesemwa mwenyekiti wa
waendesha pikipiki (bodaboda) Mafinga Baraka Frank katika mahojiano maalumu na mtandao
huu yaliyofanyika katika maegesho ya pikipiki zao maeneo ya stendi.
Frank amesema madereva wa magari
hayo wamekuwa wavunjaji makusudi wa sheria za barabarani kutokana na mwendo wao
kuwa mkali na kutozingatia alama zilizopo pamoja na kutumia vibaya barabara
wakidhani ni wao tu ndio wenye barabara.
“Ajali nyingi zinazotokea
zinasababishwa na madereva wa magari ya serikali. Wanatembea hovyo kwenye
barabara pamoja na kuwa na mwendo mkali kiasi cha kutowajali waendao kwa miguu,
waendesha baiskeli pamoja na sisi waendesha pikipiki” amesema.
Amesema kila inapotokea ajali
ikihusisha pikipiki, shutuma nyingi wamekuwa wakibebeshwa waendesha pikipiki
kwa kuwa ndio wenye chombo kidogo.
Hata hivyo amesema hata wenye
magari makubwa wamekuwa hawawathamini wenye vyombo vidogo kwa kuwa hata
ingetokea wanagongana wao hawawezi kupata tatizo jambo ambalo kwa upande
mwingine limekuwa ni la unyanyasaji.
“Tunawaomba viongozi wa serikali
kila wakati wajaribu kukaa na madereva wao na kuwaelekeza matumizi ya barabara
na hata wenye magari makubwa wapewe semina mara kwa mara ili watumie barabara
vizuri kwa usalama” amesema.
Hata hivyo amelishauri jeshi la
polisi kitengo cha usalama barabarani kutoa semina za mara kwa mara kwa
madereva wa magari ya serikali na maroli ili waweze kuzingatia matumizi ya
barabara wawapo barabarani.
No comments:
Post a Comment