Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa amesema chokochoko za uvunjifu wa amani kuhusishwa na imani za kidini zilizojitokeza mwaka uliopita zisipodhibitiwa zinalipeleka taifa pabaya.
Hayo aliyasema wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu ya Mwaka Mpya iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Mama wa Mungu Parokia ya Lyasa katika jimbo Katoliki la Iringa.
Alisema mwaka 2012 haukuisha vizuri kutokana na matukio ya kihuni, kikatili na uvunjifu wa amani kutanda kila kona huku usalama wa raia ukiwekwa rehani na kusababisha wananchi kuishi kwa mashaka.
Alisema vurugu za kisiasa, kidini hata kimakabila ambazo hazijatiliwa mkazo hadi sasa, zinatia shaka kwa mwaka 2013 endapo utaratibu wa kudhibiti hautachukuliwa.
Mhashamu askofu Ngalalekumtwa alisema tamaduni za makabila mablimbali na utofauti wa kiitikadi visiwe chanzo cha uvunjifu wa amani na kuhatarisha usalama wa raia.
“Tamaduni zetu, makabila yetu, dini zetu na siasa zetu visiwe chanzo cha kukoseana heshima na kuvuruga amani ya kila mmoja na ya taifa” alisema.
Alisema amani inavunjika kutokana na watu kukosa upendo na kuwa na tama ya kujipenda wnyewe hali ambayo inatia wasiwasi kwa misingi ya amani na mshikamano kuvurugika.
“Amani inavunjinika kwa sababu ya watu kukosa upendo kwa wengine na watu kunyang’anya haki za wengine bila sababu” alisema.
Alisema jambo ambalo ni la muhimu katika amani kutenda haki kwa kila mtu pamoja na watu kuwa huru katika maamuzi na mipano yao ya kimaendeleo.
“Amani inatoweka pale tunapokoseana haki katika maamuzi na masuala mbalimbali ya kimaendeleo katika matumizi mbalimbali ya rasilimali za taifa” alisema.
Alisisitiza kuwa, katika maisha ya binadamu kila mtu ana kasoro zake lakini jambo la akili ni kusameheana na kuvumiliana.
“Kila mtu ana kasoro zake lakini cha maana na cha akili ni kusameheana na kuvumiliana. Tusiposameheana na kulichukulia kila jambo kuwa ni la kisasi hatuwezi kufika popote pale hali ambayo kila kunapokucha kutakuwa na mvutano na migogoro isiyokwisha” alisema.
Amewataka viongozi wa kidini za kikristo wasiwe chanzo cha upotevu wa amani bali wawe mfano mzuri wa kulinda amani pamoja na kutozichukulia kashfa zinazowahusu kuwa ndiyo chanzo cha cha kupoteza amani.
“Kashfa za kidini zikomeshwe, hizo zisiwe ni chanzo cha wakristo kuingia katika uvunjifu wa amani lakini wenye mamlaka wakemee hizo kwa sababu hizo ndizo chanzo cha kupoteza mwelekeo wa taifa katika kuingia kwenye migogoro ya kidini.
Amewataka viongozi hao wahakikishe kuwa hakuna malezi ya kufundisha kuua wala kutoa nafasi ya kufundisha mbinu chafu zinazoangamiza roho za watu kwani kufanya hivyo inakuwa ni kinyume na mafundisho ya kikristo.
“Ni Mungu gani aliyefundisha malezi ya kuua? Malezi ya kufundisha kuua hayana nafasi. Mungu amekataa kuua, tusiruhusu mbinu chafu za kuanamiza wengine bila sababu. Tutendeane haki. Kauli zetu na vitendo vyetu visiwaudhi wengine lakini uvumilivu ni jambo la busara” alisema.
Alisema mauaji ya raia si jambo la kuchukulia mzaha kwa kuwa damu ya mtu ikimwagika ni laana kwa vizazi vinavyobaki.
Hata hivyo alisema katika kudumisha uhuru, wengine wanatumia uhuru kwa kufanya mambo ya ukandamizaji na unyonyaji ikiwa ni pamoja na kutumia rasilimali za taifa vibaya kwa ubinafsi.
“Uhuru wetu usitumike vibaya kiasi cha wengine kuwakandamiza na kuwanyonya wenzao hata kutumia rasilimali za taifa vibaya. Kuiba wanyama wa taifa, madini, kodi za walipakodi, unyang’anyi wa ardhi za watu na mali zao ni matokeo ya watu kutumia uhuru vibaya kwa kujiona kama wako juu ya wengine” alisema.
Sambamba na hilo alisema baadhi ya vionozi wanatumia madaraka yao kwa kuwafanya wengine kufa kwa kukosa lishe huku wao wakifa kwa kula kupita kiasi.
“Kuna watu wanakufa kwa kukosa lishe bora kwa sababu ya kunyimwa fursa ya kupata chakula chenye virutubisho lakini wapo wanaokufa kwa kula mno kutokana na kuwanyang’anya wengine na kutaka kula peke yao kila kitu” alisema.
Alisema miongoni mwa matatizo makubwa ambayo yanalitafuna taifa ni kutokuheshimu sheria na taratibu za makubaliano ya pamoja kama mongozo wa maendeleo.
“Tuheshimu sheria tunazokubaliana kikatiba ikiwemo sheria ya uhuru, tukae kwa utulivu katika mwaka huu, tusiogopane kama wanyama wa mwituni, tutoe ushirikiano pale unapotokea uhalifu wala tusiogope kutoa taarifa za kuhalifu” alisema.
Aliongeza kusema kuwa ujambazi unaojitokeza katika kila kona ya nchi, unatokana na viongozi wezi na kusababisha vijana kukata tamaa na kutaka watanzania kutokubali kuwaendekeza viongozi wa mtindo huo pale wanapopata nafasi ya kufanya maamuzi.
“Ujambazi unaotokea katika nchi yetu ni matokeo ya viongozi wezi ambao wanasababisha vijana kukata tama kwa sababu njia nyingine ya kujikomboa. Mnapata nafasi ya kufanya maamuzi, msiwaendekeze viongozi wa mtindo huo” alisema.
No comments:
Post a Comment