KWA mara ya tatu mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi
wa habari wa kituo cha runinga cha Channel Ten Daud Mwangosi hakufikishwa
mahakamani kutokana na sababu iliyoelezwa kuwa ni mgonjwa.
Mwendesha mashtaka wa serikali Adolf Maganda ameiambia
mahakama leo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Dyness Lyimo kuwa mtuhumiwa
asingeweza kufikishwa mahakamani kutokana na taarifa ugonjwa japo kuwa
haikuelezwa yupo katika hospitali gani.
“Shauri hili inaletwa kwa ajili ya kutajwa lakini kwa taarifa
zilizotufikia ni kwamba mtuhumiwa anaumwa kwa hiyo hatoweza kufika lakini hata
hivyo upelelezi bado unaendelea” amesema Maganda.
Hata hivyo kesi imeahilishwa hadi 31 Januari mwaka huu
itakapotajwa tena.
Siku ya kwanza mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa
gari la kifahari lenye namba za kiraia T 320 ARC linalosadikiwa kuwa ni la RCO
huku kwa mara ya pili akifikishwa kwa miguu na kuondolewa mahakamani hapo kwa
gari namba DFP 2175 pick up akiwa katika ulinzi mkali huku waandishi wa habari
wakidhibitiwa na polisi na mmoja wao kunusurika kupigwa jambo lililoamsha hisia
tofauti miongoni mwa wananchi wengi mkoani hapa.
06 Desemba mwaka jana mtuhumiwa huyo hakufikishwa mahakamani
kutokana na sababu iliyotolewa kuwa gari la kusafirishia mahabusu limekosa
mafuta.
Katika hali isiyo ya kawaida, mtuhumiwa huyo mwenye namba G
2573 akiwa mahakamani hapo alipandisha hasira na kutaka kumpiga mwandishi wa
gazeti hili aliyekuwa akipiga picha mahakamani hapo.
Pasificus akiwa na jazba alisikika akisema “watu tuna uchungu
na kesi halafu wewe unapigapiga picha hapa kwa sababu gani, nitakumaliza mimi,
alaa”.
Katika hatua ya mtuhumiwa akisaidia na askari kutaka kumpiga
mwandishi, mwendesha mashtaka aliingilia kati na kuwataka askari waache fujo
kwa kuwa mwandishi huyo hakuvunja sheria jambo lililowasababisha baadhi ya
asjkari waliokuwepo hapo kutoka katika chumba cha mahakama wakiwa katika hali
ya aibu.
“Waandishi wanaujua utaratibu wao, hebu mwacheni na yeye
anafanya kazi katika nafasi yake. Muda wao wakupiga picha wanaufahamu hebu
waacheni waandishi wawe huru, ni haki yao” alisema Maganda.
Mwangosi aliuawa kwa bomu Septemba 2 mwaka jana katika kijiji
cha Nyololo Wilaya ya Mufindi alipokuwa akiwajibika kwa kazi za kihabari wakati
wa ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
No comments:
Post a Comment