VIJANA wametakiwa kuungana kwa ajili ya kulinda rasilimali za nchi ili kuirudisha heshima ya nchi kama Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere alivyofanya.
Haya yalizungumzwa na Mkufunzi Msaidizi wa Chuo cha Mtakatifu John kilichopo Dodoma, Emmanuel Mrindoko, katika mdahalo uliofanyika juzi Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO) kwa ajili ya kufanya kumbukumbu ya Nyerere.
Alisema bila kujali kada za vyama na maslahi, vijana wakiungana kwa ajili ya kupigania matumizi sahihi ya rasilimali za taifa, heshima ya nchi inaweza kurudi kwa kuwa nguvu yao ni kubwa kuliko ya watu wengine wote.
Mrindoko alisema nchi inakwenda pabaya kwa sababu ya kukosa wazalendo wenye kulinda mali ya taifa kwa kuwa viongozi wengi wamejaa ubinafsi, rushwa na uchu wa madaraka na kutumia madaraka kwa kuuza rasilimali kwa wageni bila kujali faida ya nchi.
“Mwalimu Nyerere aliweza kuwaunganisha watu katika umoja, haki na usawa kwa sababu alikuwa mzalendo wa kweli, lakini nchi inakwenda pabaya kwa sababu ya kukosa wazalendo ambao wana uchungu na nchi; tatizo ubinafsi ndio uliotawala kila pembe ya nchi, viongozi wetu wengi ni waroho wa madaraka, wanaojipenda wenyewe, wamejaa rushwa na wanaifilisi nchi,” alisema.
Mrindoko alisema ili kufanikisha hayo, inahitajika bidii ya dhati kwa kila mtu kujituma katika nafasi zao ili kuleta changamoto kwa viongozi wanaojisahau kiuwajibikaji.
No comments:
Post a Comment