| Picha inayoonekana ni marehemu Padre Salutaris Lello Masawe aliyekuwa Mkuu wa Shirila la Wamisionari wa Consolata Tanzania ambaye amezikwa leo katika makaburi ya Jimbo la Iringa yaliyopo Tosamaganga. |
Wakristo Wakatoliki wameshauriwa
kujiuliza kuwa wanahusiana na wengine vipi kama
ishara ya kujiandaa kuufikia uzima wa milele mbinguni.
Hayo yamezungumzwa leo na Askofu
wa Jimbo Katoliki la Iringa Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa alipokuwa
akihubiri wakati wa Misa ya Mazishi ya Padre Salutaris Lello Massawe
ilifofanyika katika Kanisa la Moyo Mt. wa Yesu Parokia ya Tosamaganga jimboni
humu.
Amesema binadamu hataulizwa
endapo alitenda matendo ya upendo bali ataulizwa kama
alikuwa na roho ya ubinadamu na haki katika kuwajali wengine.
“Swali la kujiuliza kila wakati
katika maisha ni kwamba, umehusiana na watu wangapi wakakubariki? Na tena
hatutaulizwa endapo tulitenda upendo bali tutaulizwa kama
tulikuwa na roho ya ubinadamu na haki katika kuwajali wengine” amesema
Amesema Mungu ana mzaha katika
kuvichukua viumbe wake kwani huchukua muda anaoutaka ambao binadamu haujui
lakini jambo la msingi ni kujiandaa kiroho ili kuwa tayari wakati wowote.
“Munu ana mzaha pia. Mzaha
wenyewe ni kiama huu ambao kila mtu anajiuliza kwa nini Massawe ameondoka
wakati ambao hakutarajiwa? Kila mtu anajiuliza, kwa nini mapema? Kwa nini
ghafla? Huo ndiyo mzaha wenyewe ila yeye anajua kila mtu atamchukuaje na kwa
wakati gani” amesema.
Akimzungumzia Massawe Mhashamu
askofu Ngalalekumtwa amesema alikuwa ni mtu mwenye bidii, uaminifu katika
kuwajibika na alikuwa na maneno ya kutia moyo.
“Kazi za kitume alizitenda kwa
bidii na kwa uaminifu. Pia alikuwa na maneno ya kutia moyo. Aliadhimisha
matendo ya wokovu kwa nidhamu. Tunaimani kabisa kuwa huko alikokwenda ni
kuzuri” amesema.
Amewataka Wakristo kuwa ni watu
wa kutenda haki na kujituma katika kuwasaidia wanaohitaji msaada kwa kutenda
matendo ya upendo wakijua kuwa maisha ya mwanadamu ni safari ya kumtafuta
Mungu.
“Tendeni matendo ya haki, matendo
ya upendo kwa kuwasaidia wahitaji kwa kujua kuwa safari ya mwanadamu ni
kumtafuta Mungu; binadamu kajaliwa moyo mkubwa wa kuweza kumwelekea Mungu”
amesema.
Padre Salutaris Lukas Massawe
Lello alizaliwa Moshi Julai 8, 1962. Baba yake ni Lukas Victor na Mama, Maria
Illuminata Manka.
Alisoma katika shule ya msingi ya
Singachini kati mwka 1971 – 1978, akajiunga katika seminari ya Maua ambapo alisoma mpaka 1985, alipohitimu
masomo ya sekondari.
Mwaka 1985 alianza masomo ya
falsafa na teolojia katika seminari ya Consolata ya Nairobi na kuhitimu mwaka 1988 alipoanza
unovisi. Alimaliza unovisi mwaka 1989 na akafunga nadhiri za kwanza 21 Julai
1989 Sagana (Kenya).
23 Oktoba 1992 alifunga nadhiri
za milele Nairobi
na 28 Novemba 1992 akapewa daraja la ushemasi.
Julai 27, 1993 alipewa daraja la
upadre Moshi kwa kuwekewa mikono na Mhashamu Baba Askofu A. Msarika.
Pd. Massawe alifanya kazi ya
umisionari katika nchi ya Ethiopia
kutoaka 1995 hadi mwaka 2000 baada ya hapo akatumwa Italia akifanya kazi ya uhamasishaji
wa roho ya umisionari hadi mwaka 2007 aliporudi Tanzania.
Baada ya kusoma katika Chuo Kikuu
cha Mt. Augustino Mwanza, akatumwa Bunju, Dar
es Salaam kwa ajili ya shughuli za gazeti la
wamisionari wa Consolata “Enendeni. Kutoka Septemba 7, 2011 alikuwa Baba Mkuu
wa Shirika la Wamisionari wa Consolata nchini Tanzania.
Pd. Massawe alifariki Oktoba 25,
2012 Bagamoyo kwa ajali ya Maji na kuzikwa Oktoba 30, 2012 katika makaburi ya
Jimbo yaliyopo Tosamaganga.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na
viongozi mbalimbali wa serikali na madhehebu ya kidini kutoka ndani na nje ya
nchi ambapo jumla maaskofu wanne walihudhuria mazishi hayo.
Maaskofu hao ni pamoja na
Mhashamu Desderius Rwoma wa Jimbo Katoliki la Singida, Mhashamu Alfred Maluma
wa Njombe, Mhashamu Evaristo Chengula wa Mbeya pamoja na Mhashamu Tarcisius
Ngalalekumtwa wa Iringa ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania.
No comments:
Post a Comment