| Wanahabari wakitoka njea ya mahakama ya hakimu mafawidhi wa Wilaya baada ya kushinda siku nzima kusubiri mtuhumiwa wa mauaji ya mwanahabari mwenzao na kuambulia patupu |
| Wanahabari wa Mkoa wa Iringa wakitoka mahakamani baada ya kusubiri mtuhumiwa wa mauaji ya mwanahabari mwenzao mahakamani bila mafanikio. |
| Wanahabari wakisubiri Mtuhumiwa wa mauaji ya mwanahabari mwenzao katika mahakama ya Hakimu mfawidhi wa Wilaya leo |
| Wanahabari wakiwa kwenye viunga kusubiri mtuhumiwa |
Mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten Daud Mwangosi aliyetarajiwa kufikishwa katika mahaka ya hakimu mfawidhi ya Wilaya mkoani Iringa hakufikishwa kutokana na sababu ambazo hazikuwekwa wazi.
Kutofikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa huyo kulithibitishwa na waandishi wa habari mkoani hapo waliopiga kambi kuanzia majira ya saa 2 asubuhi hadi saa 9:37 alasiri pasipokushuhudia mtuhumiwa huyo kufikishwa mahakamani hapo kama ilivyotarajiwa.
Juhudi za wanahabari hao ambao walipiga kambi katika viunga vya mahakama hiyo ziligonga mwamba kufuatia taarifa kutoka kwa chanzo cha babari cha kuaminika ambacho hata hivyo hakikutaka kutajwa jina lake zilieleza kuwa mtuhumiwa huyo atapandishwa kizimbani mapema kesho.
“Mnasubiri nini hapa! Muda wa mahakama umeshaisha, muda mrefu nawaona mmekusanyika mahali hapa; kama ni suala la kufikishwa mahakamani kwa askari anayetuhumiwa kwa mauaji ya mwanahabari mwenzenu, jaribuni kuja kesho lakini mimi siyo msemaji wa mahakama” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo kulikuwa na tetesi kuwa hapo jana kulikuwa na kikao kizito kilichofanyika katika kituo kikuu cha Polisi (sokoni) mkoani humo kilichoongozwa na IGP Said Mwema kikihusisha polisi na viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini.
Taarifa kutoka ndani ya jeshi la polisi zilieleza kuwa Mwema aliitisha kikao hicho kwa lengo la kuomba radhi kwa viongozi wa dini kutokana na tukio la mauaji ya mwanahabari huyo na matukio mengine ambayo yanatuhumiwa kufanyika na jeshi hilo.
Katika hatua nyingine waandishi wa habari mkoani humo wamesusia wito wa Mkuu wa Mkoa huo Dk. Christine Ishengoma kutaka kuongea na waandishi kwa kile walichosema hawapo tayari kumsikiliza kiongozi huyo kwa kuwa hakuonesha ushirikiano katika msiba wa mwanahabari mwenzao.
Taarifa juu ya wito huo wa mkuu wa Mkoa zilitolewa na afisa habari wa Mkuu wa mkoa Denis Gondwe ambazo zilielezwa kuwa kiongozi huyo alihitaji kuongea na waandishi kuhusu shughuli za usalama barabarani pamoja na mambo ya utalii kauli ambazo wanahabari walizipinga vikali na kuahidi kubaki na msimamo wao kwa kuto toa ushirikiano kwa jeshi la polisi na Mkuu wa Mkoa.
No comments:
Post a Comment