| Godfrey Mtete (kushoto) mwenyekiti wa kijiji cha Ibofwe akiwa na mgonjwa mwenzake katika kituo cha afya cha Ipogolo |
| Baadhi ya wagonjwa walioolazwa katika kituo cha afya cha Ipogolo |
| Mganga mfawidhi wa kituo cha afya cha Ipogolo Mary Makundi |
Mtu mmoja amefariki na wengine zaidi ya 40 wamelazwa katika hospitali katika vituo vya afya na hospitali mbalimbali katika Mkoa wa Iringa baada ya kula chakula na kunywa togwa zinazosadikiwa kuwa na sumu katika sherehe ya kutoa mahali.
Tukio hilo lilitokea juzi jumamosi katika sherehe hiyo ilifanyika katika kijiji cha Ibofwe Kata ya Ilole Wilaya ya Kilolo katika Mkoa wa Iringa baada ya mkazi wa kijiji hicho Jamesi Ngaile kuandaa chakula na kinywaji aina ya togwa kwa ajili ya sherehe ya kumwoza binti yake.
Mmoja wa majeruhi hao Yamile Mhehe ambaye amelazwa katika kituo cha afya cha Ipogolo kilichopo katika Manispaa ya Iringa amesema utaratibu wa kupata chakula ulikuwa ni sahani moja kwa watu watatu na kwamba huenda ikawa ni sababu mojawapo katika kupatwa na matatizo hayo.
Mhehe ametaja chakula hicho kuwa ni wali huku mboga ikiwa ni maharage na kabeji na kinywaji kilichotumika kwa wageni ni togwa za ulezi pamoja na unga wa mahindi.
“Chakula tulichokula ni wali na mboga ilikuwa ni maharage na kabeji huku wageni waalikwa katika sherehe hiyo wakitumia kinywaji aina ya togwa kilichotengenezwa kwa ulezi kwa kuchanganywa na unga wa mahindi” alisema Mhehe
Alisema masaa mawili baada ya kuwasili nyumbani baada ya kumaliza shughuli za sherehe yeye na mke wake walijisikia kuumwa tumbo na kuanza kuharisha damu ndipo walipoamua kwenda kuomba msaada kwa majirani ambapo baada ya kufika kwa majirani wakakuta nao wakiwa na tatizo kama la kwao na kuamua kwenda kwa mwenyekiti wa kijiji kuomba msaada na kushindikana kwa kuwa naye alikutwa akiwa hoi hajiwezi kutokana na tatizo hilo hilo.
Baada ya kuonekana kijiji kina watu zaidi ya 20 wanatatizo linalofanana, uongozi wa kijiji uliamua kukodi daladala na kuwakimbiza katika kituo cha afya cha Ihimbo kilichopo wailiani humo na wale waliokuwa na hali mbay azaidi walikimbizwa katika kituo cha afya cha Ipogilo mjini Iringa kwa matibabu zaidi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi akiwa katika kituo cha afya cha Ipogolo, Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Gofrey Mtete alisema tukio hilo ni la kwanza katika kijiji hicho nab ado tatizo halijabainika kuwa lilitokana na chakula, mboga au togwa japo uchunguzi unaendelea kufanyika na wataalamu mbalimbali wa afya za binadamu.
“Watu waliopatwa na mkasa huo ni zaidi ya 40 lakini ambao walionekana kuwa mahututi na kukimbizwa matibabuni ni 38 japo wananchi wengine zaidi wameendelea kufikishwa katika vituo vya afya na hospitali mbalimbali kwa ajili ya matibabu” alisema Mtete.
Hata hivyo Mtete amemtaja Wagila Nyaipumbwe ambaye ni mjomba wake kuwa alifariki dunia kijijini hapo kabla ya kukimbizwa katika kituo cha afya.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mganga mfawidhi wa kituo cha afya cha Ipogolo Mary Makundi amekiri kupokea wagonjwa 9 katiika kituo hicho na kuwataja kwa majina kuwa ni Rafiki Kabogo, Beth Ngaile, Neema Ngaile, Emelia Mwilafi, Edina Mkemangwa, Costansia Maliga, Ayubu Kaywanga, Godfrey Mtete na Yamile Mhehe na kusema kuwa hali zao zinaendelea vizuri na kusema kuwa wagonjwa wengine walipelekwa katika hospitali ya Mkoa wa Iringa kwa matibabu zaidi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa Michael Kamhanda alisema hajapokea taarifa kuhusiana na tukio hilo na kuomba alifanyie uchunguzi na kuwa atakapozipata taarifa hizo atazitoa.
No comments:
Post a Comment