![]() |
| Nelson Mbimbi mkazi wa kijiji cha Kising’a Mkoani Iringa akihojiwa na mwandishi juu ya mafanikio yake kutokana na kilimo cha alizeti. Pikipiki ni mali yake ambayo ni mafanikio ya kilimo. |
MBAO za
matangazo kwa wajasiriamali zimemkomboa kimaisha Nelson Mbimbi mkazi wa kijiji
cha Kising’a Kata ya Kisinga tarafa ya Isimani Wilaya ya Iringa katika Mkoa wa
Iringa.
Akiongea na mtandao huu Mbimbi
amesema mbao za matangazo zilizobandikwa na Muunganisho Ujasiriamali Vijijini
(MUVI) juu ya bei za mazo zimemfanya kujikomboa na umasikini aliokuwa nao.
“Niliona matangazo ya MUVI yamebandikwa
kwenye mbao za matangazo katika kijiji changu yaliyokuwa yakihusu wajasiriamali,
bei za mazao yote yanayozalishwa hapa kijijini, wanakijiji tulipewa elimu ya
matumizi ya ubao wa matangazo japo kuwa
sikuona umuhimu” alisema Mbimbi.
Amesema mara kwa mara alikuwa
akijiuliza, ni mara ngapi ubao uandikwe na kuundiwa kamati ya kuusimamia ubao
hali ambayo alisema aliona ni ya kipuuzi hadi hapo alipoeleweshwa kuutumia.
Amesema kwa muda mrefu wakulima
wa kijiji hicho wamekuwa wakilima bila mafanikio kutokana na elimu ndogo
waliyokuwa nayo na kubaki gizani kutokujua nini cha kufanya.
Hata hivyo amesema “licha ya
kulima bila mafanikio, hatukuwahi kufikiri kuhusu suala la mawasiliano,
kupashana habari juu ya kile tulichokuwa tukizalisha. Kila mtu aliuza kwa bei
yake hata walanguzi walitumia ukosekanaji wa taarifa kama njia ya kutunyonya
kwa kuwa hatukujua kama tunadhulumiwa”.
Amesema ubao huo uligawanyika
katika sehemu kuu mbili ambapo sehemu ya kwanza ilihusu taarifa za bei na
masoko na hehemu ya pili ilihusu taarifa kijamii.
Anaainisha kuwa “Sehemu ya
kwanza, taarifa za bei inayotembea kijijini hapa pamoja na mikoa ya jirani. Sehemu
ya pili taarifa zinazohusu jamii husika”.
Pamoja na kwamba mradi wa MUVI unajihusisha
na kuendeleza mnyororo wa thamani wa zao la alizeti na nyanya katika mbao za
matangazo hizo mazao mengine pia yamepewa nafasi katika ubao huo kuonesha bei.
“Wanakijiji wapatao 60-150
huweza kupata taarifa za bei kupitia ubao wa matangazo kila wiki. Mimi ni mmoja
kati yao, kila
siku bei zinavyoandikwa huwa naenda
kujisomea na kufahamu bei inayotembea
sokoni” anasema.
Anasema kuwa walanguzi wengi
hufika vijijini kununua mazao kwa mazoea kuwa watu wa vijijini hawajui bei za
matangazo lakini leo ni tofauti kwani wakulima wengi wameshapata elimu
“Anakuja mlanguzi anataka
kununua alizeti gunia moja lenye ujazo wa kilo 60 kwa shilingi elfu (30) thelathini…wakati
huo ubao wamatangazo umendikwa gunia la kilo 60 ni shilingi elfu 50 hamsini”
anasema.
Anasema wakati mwingine
walanguzi wanakuwa wanaifahamu bei ya mazao lakini kwa makusudi wanataka
kumgandamiza mkulima; wanajaribu kushawishi ili wanunue bei zao lakini kwa kuwa
bei zimeandikwa katika mbao za matangazo, inakuwa ni vigumu kushawishika
kirahisi.
“Mlanguzi akija na kuanza
kutushawishi kwa bei zake, swali la kwanza huwa tunamuuliza hivi: umesoma ubao
wa matangazo? Mlanguzi anajibu hapana halafu tunamwambia: Kasome halafu urudi… halafu anaondoka kwa aibu” anasema
Mbimbi.
Ubao wa matangazo kwa
wajasiriamali vijijini huandikwa taarifa
za bei kila baada ya siku tatu, yaani
jumatatu, jumatano na ijumaa.
Mbimbi anaeleza kuwa baada ya
kuweza kutumia vizuri mbao za matangazo kujihabarisha, amefanikiwa kununua
pikipiki aina ya SunLug na pia ameweza kulipia gharama za kuunganishiwa umeme
kwenye nyumba yake hapo kijijini.
Kijiji cha Kising’a kipo katika
umbali wa takribani kiometa 25 kutoka mjini
Iringa. Ni kijiji ambacho wakazi wake hujishughulisha na kilimo cha
alizeti pamoja na mazao mengine kama vile mahindi, kunde, mtama na mazao ya mboga mboga.


No comments:
Post a Comment