masuguru

Tangazo la cheti

Tangazo la cheti
tangazo

KLERUU

KLERUU
KLERUU

CAPRICORN

CAPRICORN

Ibada

Ibada

Sunday, September 16, 2012

Walitaka Mwangosi naye awe msanii wa filamu?









                                                            MTAZAMO WANGU

KIFO cha David Mwangosi, aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten na Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Iringa, hakikupewa uzito na viongozi wa serika kwa vile hakua mwigizaji ama mwanamuzikii.

Wakati umma ukimlilia Mwangosi, viongozi wako kimya, hawakuona thamani yake kwao.
Kitendo hiki cha serikali, ndicho kimenifanya nifikirie kuwa yawezekana kwa vile Mwangosi hakuwa mwimbaji wa nyimbo za bongo fleva wala mcheza filamu.

Leo hii Mwangosi anaonekana alikuwa mtu muhimu kwa waandishi wenzake na wananchi wa kawaida na pia katika mataifa mengine si kwa viongozi wetu wa serikali.

Inasikitisha kuona kuwa tulioamini kuwa ni viongozi wake, watawala waliokubali kuwatumikia watanzania baadhi yao wakiwa mstari wa mbele kufurahia kile kilichomkuta Mwangosi.

Nani asiyekumbuka kifo cha muigizaji wa filamu nchini Steven Kanumba kilichomfanya Rais Jakaya Kikwete kuahirisha safari yake nje ya nchi kumuenzi?

Ni nani asiyekumbuka serikali ikitoa ubani wenye thamani ya shilingi 10 milioni katika msiba wa Kanumba?
Ni nani asiyekumbuka kauli na matamko ya serikali juu ya kusikitishwa na kifo cha mwigizaji huyo? Hii ndio hulka ya serikali yetu inayoimba usiku na mchana kujali makundi yote katika jamii.

Ni kwanini Mwangosi ametendwa hivi na viongozi wetu wa serikali akiwemo Rais wetu ambaye amekuwa mwepesi kutoa pole misiba mbalimbali na ikiwezekana kufika au kuwakilishwa rasmi?

Ama kwa sababu alikuwa akiwasumbua watawala kwa kalamu yake na sauti yake ya kuibua uozo wao? Hiki kilichofanywa na serikali kwa Mwangosi, kinatoa tafsiri nyingi sana.

Mojawapo iliyo wazi kabisa, ni kuwa kwa Tanzania usipokuwa muigizaji wa filamu au mwimbaji wa nyimbo za kizazi kipya hata ukipata tatizo ambalo linahitaji msaada, huwezi kupata.

Siku chache tu zimepita nilishuhudia na kusikia maneno ya Waziri Stephen Wassira akiwa katika runinga ya TBC akisema Mwangosi ni nani hata watu kushinikiza tume kuundwa ili kuchunguza kifo chake?”

Hii ni kauli iliyotolewa na mwakilishi wa wananchi kupitia Jimbo la Bunda ambao nao ni sehemu ya watanzania walioguswa na tukio hilo la mtu asiye na hatia kuuawa kinyama tena na askari Polisi.

Wassira ni aina mojawapo ya viongozi wa nchi hii aliyeguswa na tukio la Mwangosi. Inasikitisha sana kuona viongozi wetu wamefikia ujuha wa kiwango hiki kwani penye kifo mengine yote huwekwa kando.

Lakini, ungetaraji nini kutoka kwa Wassira kwani ni kutoka ndani ya serikali hiyo hiyo ambayo jeshi la polisi lililokatisha uhai wa Mwangosi limo.

Kauli yake sio tu inalenga kuashiria alichofanyiwa Mwangosi ni cha kawaida, pia ni kutoa jawabu kwa umma kwamba serikali ndivyo ilivyo.

Kwa upande mwingine, siwezi kumlaumu Wassira kwa sababu anafikisha ujumbe kwa umma kuwa serikali yenye jeshi la polisi lililogawana nyama ya Mwangosi ndivyo ilivyo.

Wacha niseme, popo ni ndege pia ni mnyama wa ajabu sana! Ukifika mudawa kulala yeye hutanguliza miguu yake juu na sehemu ya kichwa chake huning’inia chini.

Akitaka kupumua yeye hafikirii kama atajichafua na matokeo yake hujichafua.

Mauaji yaliyotokea Morogoro na baadaye Iringa ambayo jeshi la polisi linahusika moja kwa moja, sijasikia kauli ya Mkuu wa Mkoa kulaani au kukemea hali hiyo.

Najiuliza hivi kazi za Mkuu wa Mkoa ni zipi? Labda kwao kuuawa wananchi ndani ya Mkoa wao ni kitu cha kawaida na pia ni hazina yao.

Tuachilie mbali kauli ya Rais ambaye hadi sasa haijulikani kama yupo au hayupo kutokana na ukimya wake. Ina maana yule mwananchi aliyeuawa kule Morogoro pamoja na Mwangosi hawakuwa walipa kodi?

Labda Wassira angetueleza kuwa Mwangosi alikuwa nani hata asistahili kuundiwa tume ya uchunguzi.
Siendi haraka kumkebehi wala kumkejeli. Najua ana nia njema ya kile anachotaka jamii ijue lakini ninachomuomba aweke wazi ili kijulikane.

Simaanishi kuwa ilikuwa ni lazima kwa serikali kutoa ubani katika msiba wa Mwangosi, lakini nataka kujua Mkuu wangu wa Mkoa umefurahishwa na jambo hilo?

Nataka kujua Rais wangu Kikwete, wewe kama Mkuu wa nchi hii umependezwa na unyama aliofanyiwa dhidi ya Mwangosi?

Sisemi hili si kwa vile tu alikuwa kiongozi wangu, bali nasema hivi kwa vile naye ni binadamu mwenzangu mwenye hadhi na heshima kama mwingine yeyote ambaye uhai wake ulipaswa kulindwa kwa gharama yoyote ile.

Je, ni nani angependa kufanyiwa unyama kama ule aliofanyiwa Mwangosi na yule Ally Zuna aliyedaiwa kupigwa na kitu kizito pale Morogoro kwa mujibu wa uchunguzi wa polisi?

Ni nani anapendezwa na matukio ya kiyahudi kama hayo? Nafika mahala najiuliza, Rais wangu usalama wa watu wako uko wapi katika nchi hii inayodaiwa kuelea kwenye uhuru na amani?

Nitakulaumu bure Rais wangu kwa kuwa naamini bado upo katika safari, najua utakapokuwa umerejea nchini utaonesha hisia zako na kutoa tamko lako.



Najua uko katika majukumu ya Taifa huko uliko. Natamani urudi ili uje uwahakikishie watu wako usalama kwa kuwa najua wewe ndiye amiri jeshi Mkuu.

Huku nchini tangu uondoke inaonesha hujawaacha viongozi wengine ambao wanaweza kukemea mambo machafu na vitendo vinavyoweza kufanana na vile vya kigaidi.

Sijajua kama Mkuu wa Mkoa naye alimsindikiza Rais huko aliko maana naye sielewi kama yupo.
Naomba waungwana mnijulishe kama hayupo ili nisije nikamlaumu bure. Ila imani yangu ni kwamba hayupo japo huenda ikawa ni imani yangu binafsi.

Katika fikra zangu daima huwa nafikiri kuwa askari kabla hajapata ajira huwa anapimwa akili kwanza.
Sitoamini kirahisi kuwa jeshi la polisi linaweza kuajiri vichaa. Kama kuna mwenye imani hiyo, hakika ni kudanganyana.

Katika hali ya kawaida tu sioni kama askari aliyeajiriwa anaweza kuamua kwa makusudi au maamuzi yake kutumia silaha katika kundi la watu bila amri. Siamini kama aliyemfyatulia bomu Mwangosi aliamua mwenyewe.

Pamoja na mtuhumiwa kufikishwa mahakamani, kwenye tukio hakuwa pekee yake. Najiuliza kuwa wale wengine waliomshika Mwangosi wakati mwenzao anazima uhai wa Mwangosi kama vile wagawane nyama, wako wapi? Najiuliza Kamuhanda naye amejikausha kwenye kiti akimaanisha nini?

Naomba kumuuliza Kamuhanda, ni nani atafuata baada ya Mwangosi?

Waliopo kwenye idadi ni wangapi? Siamini kama kweli Kamuhanda bado upo kwenye kiti chako kwa sababu mikono yako haipo salama.

Ningekuona ni mtu wa maana kama ungeachia kiti hicho ili wenzako wakisafishe kwa kuwa wewe umekichafua. Kwa nini uwafanye wananchi waishi kama wakimbizi ndani ya nchi yao? Imani nayo imewekwa rehani!

No comments:

Post a Comment